Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Katika mfumo wetu wa sasa wa elimu, mwanafunzi anafundishwa kusoma ili afaulu mtihani. 

Mtihani unapimwa kwa kukariri na kujibu maswali yaliyoandaliwa na mtu mwingine. 

Hakuna anayemuuliza mwanafunzi: "Kwa nini upo hai?" au "Umetumwa kufanya nini katika dunia hii?"

Hii ni hatari. Kwa sababu tunazalisha wanafunzi wa alama, si wanafunzi wa maono. Tunalea waajiriwa wa mifumo isiyo na huruma badala ya kulea waongozaji wa jamii zenye uhai.

Tuna mashule, tuna vyuo, tuna mitihani... lakini hatuna somo la kusudi. Na hapa ndipo tulipoanguka. 

Mtoto anakua bila kujua anasoma ili awe nani au atumike kufanya nini. 

Matokeo yake? Anajitahidi apate kazi yoyote ilimradi alipwe, hata kama kazi hiyo inaharibu mazingira, inahujumu jamii au inampoteza yeye mwenyewe.

“Mwanadamu asiyejua kusudi lake ni sawa na meli isiyo na dira – itazunguka tu baharini hadi itakapogonga miamba.”

Vijana wetu wanafundishwa kutafuta kazi, si kutafuta athari chanya katika dunia. Hili ni kosa la kimfumo.

Wengine wanaingia katika ajira zinazochafua hewa, zinaharibu mito, misitu, hata afya za jamii, lakini kwa sababu ‘wanalipwa vizuri’ tunaona wamefanikiwa. 

Hii si mafanikio – ni maangamizi yaliyopakwa mafuta ya ustaarabu.

Mafanikio ya kweli siyo kuwa na kazi, bali ni kufanya kazi yenye maana inayotimiza kusudi lako na kuchangia uhai wa dunia.

Ukiangalia kwa karibu, utafahamu kwamba wizi, uhalifu, mauaji, uongo, ukahaba, na hata rushwa nyingi ni zao la njaa – siyo njaa ya chakula tu, bali pia njaa ya maarifa sahihi na fursa za kweli.

Mtoto anapomaliza shule hana stadi, hana uwezo wa kujitegemea, hana ardhi ya kulima, hana mtaji wa kuanzisha biashara – matokeo yake, njaa inamfanya atafute njia yoyote ya kuishi, hata ikiwa ni ya hatari.

“Njaa ni silaha ya utawala. Mtu aliye na njaa hawezi kufikiri kwa uhuru – anatafuta tu namna ya kuishi.”

Wakati dunia inahangaika na ajira, jibu linaweza kuwa karibu zaidi kuliko tunavyodhani.

Jukumu la kwanza kabisa la mwanadamu katika bustani ya dunia lilikuwa ni kushughulikia miti ya matunda– yaani kulima, kutunza, na kuzalisha chakula. 

Hii ni kazi ya asili kabisa. Lakini sasa, elimu yetu inamchukulia mkulima kama mtu duni – na hapa ndipo tulipoharibu msingi.

Vijana wafundishwe kilimo cha kisasa, wafundishwe ujasiriamali, wafundishwe kuanzisha miradi yao binafsi. Hapo ndipo watapambana na njaa, na hapo ndipo maadili yatarejea.

📌 Somo la Kusudi (Purpose Studies): Kila mwanafunzi afundishwe kujitambua, kujua vipawa vyake, ndoto zake na wajibu wake kwa dunia.

📌 Elimu ya Kujitegemea: Stadi za maisha, ujasiriamali, kilimo, ufundi na ubunifu viwe msingi wa mitaala.

📌 Maadili na Mazingira: Mwanafunzi ajifunze kufanya kazi yoyote kwa kujali uhai wa viumbe wengine na mazingira.

📌 Mtihani wa Maisha: Mitihani ipime uwezo wa kutatua matatizo, si uwezo wa kukariri majibu.

Tukibadilisha elimu, tutabadilisha jamii. Tukiwaandaa watoto wetu kwa ajili ya kusudi, si kwa ajili ya alama tu, tutakuwa tumewekeza kwenye kizazi kinachojua wajibu wake kwa dunia.

Tukiwawezesha kujiajiri na kuondoa njaa, tutapunguza maovu mengi bila kutumia mijeledi wala vifungo.

"Elimu ya kweli siyo kufaulu mtihani, bali ni kufaulu maisha." — Emmanuel Samuel King’ung’e

Je uko tayari kuona kizazi kipya kinachotembea kwa kusudi, kinachojiajiri, na kinachotunza dunia? Mageuzi hayo yanaanza leo – na yanaanza na wewe.

Wasifu wa Mwandishi

Emmanuel Samuel King’ung’e ni mwandishi, mnasihi wa utambuzi binafsi na mwanzilishi wa King Mentorship Program. 

Kupitia mafundisho yake, amekuwa msaada wa kweli kwa maelfu ya vijana, wazazi, na wale wanaotafuta mwelekeo wa maisha. 

Anaamini kila mtu ameumbwa kwa kusudi maalum, na kwamba jamii ya kweli hujengwa kwa watu wanaolitambua kusudi hilo.

Jiunge na King Mentorship Program Leo

Je unataka kugundua kusudi lako?
Unataka kutambua vipawa vyako?
Unataka kuanza safari ya maisha yenye mwelekeo?

👉 Jiunge na King Mentorship Program leo:
📞 0744 284 329
🌐 kingmentorshipprogram.blogspot.com

Mageuzi haya yanaanza na wewe.

Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e
Mwandishi | Mwalimu wa Utambuzi Binafsi | Mwasisi wa King Mentorship Program

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...