Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...
Aliyetupa Uhuru, Ndiye Aliyerudi Kuuchukua...
Afrika tulipewa uhuru, lakini hatukuachiwa uhuru wa kuwa huru.
Tulipatiwa uhuru wa kupeperusha bendera, lakini hatukupatiwa uhuru wa kujitegemea kiakili. Tulipewa serikali, lakini hatukuachiwa mamlaka ya maamuzi huru.
Tulipewa katiba, lakini hatukuachiwa utambulisho. Kwa hiyo leo tunaposherehekea uhuru, tunasherehekea nini hasa?
Je, tunasherehekea kile tulichodhani tumepata, au tunasherehekea kivuli cha kile tulichonyang’anywa?
Je, Ni nani aliyewanyang’anya uhuru wenu? Uhuru wenu ulikuwa upi? Ulichukuliwaje? Ulikuwa wapi? Na mliporudishiwa, mlipatiwa nini hasa?
Kwa sababu uhuru wa kweli hauishi kwenye vitabu, wala kwenye hotuba, wala kwenye kumbukumbu za historia, unaishi katika akili aa WATU.
Maana ya uhuru ni hali ya kiakili.
Lakini kama fikra zako bado zinamilikiwa na mifumo ile ile iliyokuja kukuteka, unaweza kweli kusema kuwa wewe ni huru?
Leo hii watu bado hawaamini kilichotokea. Wamebaki wakishangaa, midomo wazi, kwa sababu hata ule uhuru wanaouhubiri hawana.
Maamuzi yao, dira yao, na falsafa zao zimechorwa na wengine. Wanapewa cha kuamini, cha kufuata, na cha kutetea.
Wanachotetetea ni maamuzi yaliyotungwa kwa niaba yao; wanachoamini ni falsafa zilizotengenezwa kwa ajenda za mbali; wanachofuata ni njia ambazo si zao.
Lakini kilicho cha kusikitisha zaidi ni hiki: Mifumo ile ile iliyokuja kuwavuruga, kuwatenganisha, kuwapunguza thamani, na kuwafutia utambulisho, ndiyo leo mnaikumbatia huku mkitangaza uhuru.
Ni sawa na mtu anayepigania kitu ambacho hajawahi kukielewa wala kukihisi.
Mungu aliumba mwanadamu kwa hiari - hiari ya kuchagua, kufikiri, kuamua na kuishi.
Lakini kama maisha yako, falsafa zako na maamuzi yako vimeandikwa na mtu mwingine, unaweza kweli kusimama na kusema wewe ni huru?
Mnawezaje kutangaza uhuru huku bado mnaitukuza mifumo iliyokuja kuwaweka chini ya kivuli cha ukimya na utiifu?
Elimu ile ile iliyotumiwa kuwafanya mjikane, muache kujiamini, muachane na asili yenu, na muone thamani ndani ya tamaduni za watu wengine, ndiyo leo imegeuka kuwa mwanga wenu.
Lakini mwanga gani huu unaozima kumbukumbu zenu?
Mwanga gani huu unaowafundisha kujiona duni mbele ya mataifa ambayo mliyoyafundisha utu?
Ukweli mchungu ni kwamba, elimu tuliyorithishwa haikutengenezwa kutuendeleza, ilitengenezwa kututuliza.
Ilitengenezwa kutufanya tuwe wasikivu, si wabunifu. Ilikuja kutuambia kuwa maendeleo yanaonekana kwa kuiga, si kwa kuunda.
Mababu zetu waliishi na hekima, umoja, na mifumo yao ya uongozi.
Leo tunaiambia dunia kuwa hatuna chochote kutoka kwao, kwamba kila kitu chema ilikuwa lazima kije kutoka nje. Hii si KWELI!
Bado mnasema mnaadhimisha uhuru?
Dini zilizotumiwa kuwavuruga kiakili, kuwasahaulisha urithi wa mababu, na kuwasambaratisha katika makundi na alama, ndizo leo mnazibeba kama nembo za kujivunia, wakati umoja wenu unazidi kuyeyuka kama barafu juani.
Na ifahamike kuwa katika Afrika dini hazikuja kama nuru pekee; zilikuja pia kama chombo cha utawala wa kimawazo.
Zilitwaa umoja wetu, zikatutenganisha, zikatufanya tuamini kuwa mababu zetu hawakuwa na maarifa ya kiroho.
Leo tunashindana dini kwa dini, tukiwa tumepoteza cha msingi: utu, usawa, upendo na umoja.
Mnawezaje kusema mmekombolewa kiroho ilihali bado mnaambiwa wachawi, mapepo, majini na nguvu za giza ambazo zinadaiwa kukuzuia kukua?
Kiuchumi, bado hamjasimama.
Kijamii, mna vipande vipande.
Kimataifa, mnapigiwa makofi ya uwepo wenu lakini hamna sauti yenu.
Na bado mnasema huu ni uhuru?
Mifumo ya kisiasa iliyokuja kuondoa tawala za mababu zenu - tawala za umoja, maadili, adabu na usawa - ndiyo leo imegeuka kuwa dira ya mgawanyiko.
Siasa za Afrika leo zimekuwa uwanja wa mashabiki badala ya uwanja wa fikra.
Vyama vimewagawa kuliko ukoloni ulivyowagawa.
Sera zimewagawa kuliko mipaka ilivyowagawa.
Ili taifa lisishikamane, lazima ligawanywe katika itikadi zisizoisha.
Na sisi tumeendelea kuziendeleza kwa mikono yetu wenyewe.
Je, mnawezaje kufikia umoja wa kweli mkikumbatia chanzo cha mgawanyiko wenu?
Sasa jiulizeni: Kipi ni chenu? Umoja wenu uko wapi? Mnasherehekea uhuru gani ambao hata maana yake hamna?
Ukoloni uliletwa kwa ridhaa ya wachache, kama ilivyo leo ambapo ukoloni mamboleo unaendelea kwa ridhaa yenu wenyewe.
Leo mmegeuzwa mashabiki wa kila jambo, mnaishi bila kutafakari, mnaamini bila kufikiri, mnafuata bila kuuliza.
Afrika haihitaji kupewa uhuru tena, haihitaji tena risasi, maandamano, wala mapinduzi makubwa.
Afrika inahitaji jambo moja tu: Kujiweka huru kiakili.
Kujiweka huru kutoka kwenye elimu inayotutawala.
Kujiweka huru kutoka kwenye siasa zinazotugawa.
Kujiweka huru kutoka kwenye dini za kusambaratisha.
Kujiweka huru kutoka kwa hofu zisizojengwa katika ukweli.
Kujiweka huru kutoka kwa maskini wa fikra wanaotegemea maelekezo.
Kwa sababu taifa lolote ambalo akili za watu wake ziko huru, halishindiki.
Mwisho wa siku, uhuru wa Afrika hautaletwa na nguvu ya nje.
Utaletwa na kizazi cha ndani, kizazi kinachojua kujitambua, kufikiri, kuamua na kuongoza.
Na mimi ni miongoni mwa kizazi hicho.
Na ninyi mnaosoma makala hii leo, ni sehemu ya kizazi hicho.
Na Afrika tunayojenga, itakuwa kazi ya mikono yetu sisi wenyewe.
Kumbuka, "huna chako kama akili yako haijawa yako."
Asanteni sana.
Ndimi, Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment