Jinsi Ya Kuanza Upya Tena... mbinu ya 3&4
3.Jitambue Kwanza Wewe Ni Nani
Sizungumzii kujua jinsia yako, sizungumzii kutambua jina lako, sizungumzii utambulisho unaotokana na kazi unayoifanya na wala sizungumzii utambulisho unaotokana na kozi uliyosomea!
Unatakiwa kujua kwamba kuna utambulisho wa kutengenezwa kutokana na mifumo ya nje, pamoja na utambulisho unaojitengenezea mwenyewe mara baada ya kutambua kwanini ulizaliwa na kwa nini bado uko hai!
Vilevile unatakiwa kujua kwamba kujitambua ni kama kibali kitakachokuruhusu uishi maisha yenye hadhi fulani, kwamba utauishi ukuu au udhaifu wa maisha yako kutokana na vile unavyojitambua!
Na ifahamike kwamba, kujitambua wewe ni nani inaweza kuwa safari ndefu kidogo, kwani ili upate kujitambua itakulazimu uanze kutafuta sababu ya kuumbwa kwako pamoja na kusudi lililomfanya Mungu akuumbe!
Na, ndiyo maana moja ya tafsiri nyepesi ya kujitambua ni ile inayofafanua kujitambua kama ile hali ya mimi kufahamu sababu yangu ya kuishi pamoja na kuwepo hapa duniani…
Kitu kinachonisikitisha zaidi ni pale unakuta mtu, umepewa utambulisho bandia kutokana na mifumo ya kutengezewa na siyo utambulisho wako halisi na kibaya huenda umejiona wewe ndiyo ulistahili uwe hivyo kitu ambacho siyo sahihi…
Anyway maneno yasiwe mengi najua unajiuliza sasa nitajitambuaje mimi, usijali anza kujiuliza maswali yafuatayo:
Hivi mimi ni nani? Nimetoka wapi? Niko wapi? Ninaenda wapi? Ninamiliki nini ndani yangu? Ninaweza nikafanya nini? Kwanini nimekuwa hivi nilivyo? Nidhibiti nini katika maisha yangu? Pamoja na maswali mengine kama hayo.
Kwanini ujiulize maswali hayo? Unatakiwa ujiulize maswali kama hayo kwa sababu kuna mifumo imekuonesha wewe ni mtu wa aina Fulani, ilihali hukuumbwa uwe mtu huyo, ila umekuwa mtu wa aina hiyo kwa sababu umetengenezwa uwe hivyo!
Na huenda umeona kwamba huwezi ukawa mtu mwingine zaidi ya hivyo ulivyotengenezwa uwe kitu ambacho siyo kweli kabisa!
Sasa basi maswali hayo yatakusaidia uweze kujua wewe yule uliyepaswa uwe kabla hujaingizwa kwenye mifumo hiyo.
Habari njema nyingine ni kwamba maswali hayo yatakusaidia uweze kutengeneza ule utambulisho wako ulopaswa uuishi kabla hujatengenezwa…
Kumbuka huwezi kuanza upya kama hutojijua wewe ni nani!
Hivyo ni muhimu kuanza upya kwa kujitambua kwanza ili ujue unaanza na nani!
4. Weka Malengo Halisi Kuhusu Kesho Yako
Ni muhimu ukaanza upya kwa kuweka malengo mahususi, halisi, yanayowezekana, yanayopimika na yenye ukomo wa muda ili uweze kubadili maisha yako.
Unatakiwa kujua kwamba lengo ni kusudio, nia, tarajio au dhamira aiwekayo mtu ndani ya kipindi cha muda Fulani.
Unatakiwa uweke malengo ili uweze kupata matokeo ambayo hapo awali hukuyapata. Unatakiwa kujua kwamba ili upate kitu ambacho hukuwahi kukipata ni lazima ukubali kufanya kitu ambacho hukuwahi kukifanya.
Na huwezi kutimiza lengo kama hutoazimia lengo, hata hivyo huwezi kufanikisha lengo kama hakuna chochote kile ulichokiazimia!
Kitu unachopaswa kuondoka nacho hapa ni kwamba, malengo yatakufanya upate maono mapya, yatafanya juhudi zako kuongezeka, yatachochea nguvu zako zaidi, yatafanya maisha yako yawe na kusudi, pamoja na kukusaidia ujue unachokitaka hivyo hutavipa nafasi vitu usivyovitaka katika maisha yako!
Ndugu unatakiwa kufahamu kwamba, utaanza upya safari ya maisha yako, kwa kuweka malengo mapya ambayo hapo awali hujawahi kuyaweka!
Je ni kipi ambacho unataka ukikamilishe miaka kadhaa ijayo?
Je baada ya miaka mitano maisha yako yatakuwaje?
Je unataka uje uwe nani miaka ijayo?
Ndugu usisubiri mambo yawe sawa kwani haitatokea mambo yakawa sawa kama hutaamua kuyaweka yawe sawa!
Huu siyo wakati wa kusubiri mambo yatokee bali ni wakati wa kufanya mambo yatokee!
Azimia malengo mbalimbali tekeleza kwa kishindo kwani kupitia malengo ndipo mambo hutokea na maisha yako ndipo yataanza kubadilika!
Kumbuka kushindwa kupanga ni sawa na kupanga kushindwa!
Azimia malengo tekeleza kwa kishindo!
Anza upya kwa kuweka malengo halisi kuhusu Kesho Yako!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya!
Anyway Somo Lihusulo Jinsi Ya Kuanza Upya Tena litaendelea Kwa siku ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, mwalimu, mwandishi muelimishaji katika eneo la maendeleo Binafsi life coach and consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment