Badili Fikra Zako Badili Maisha Yako...
Na Emmanuel Samuel King'ung'eHivi unafahamu kwamba maisha yako yamekuwa hivyo yalivyo kutokana na fikra zako mwenyewe?
Unatakiwa kujua kwamba katika maisha huwezi ukakivuta kitu ambacho hujakitengeza kupitia fikra zako!
Mbali na hilo unatakiwa kujua kwamba hata hatima ya maisha yako huanza kama fikra, yaani unapanda wazo/dhana unavuna kitendo, unapanda kitendo unavuna tabia, unapanda tabia unavuna utambulisho, unapanda utambulisho unavuna hatima ya maisha yako!
Na, hivyo ndiyo mduara wa maisha yako ulivyo, kwamba maisha yako yamekuwa hivyo kwa sababu, yalianza kutokana na dhana/mawazo uliyoyatengeza kupitia fikra zako mwenyewe..
Kutokana na ukweli huo, ndiyo maana ilishawahi kusemwa Kwamba maisha ya binadamu ni matokeo ya fikra zake mwenyewe!
Hii inamaanisha kwamba, umefika hapo ulipo kimaisha na umekuwa hivyo ulivyo kutokana na fikra zako mwenyewe!
Na, ndiyo maana kanuni ya kupanda na kuvuna inasema kwamba "utavuna ulichokipanda"
Kinachomaanishwa hapa ni kwamba, aina ya fikra unazozitengeneza ni mbegu unazozipanda ubongoni mwako, na ukishaipanda lazima utavuna, kwani ni yule apandaye tu ndiye avunaye...
Hata hivyo hakuna mbegu ambayo huzalisha tunda lisilo la asili yake.
Kwamba ukipanda mchele utavuna mchele...
Na ifahamike kwamba, endapo utapanda mbegu tegemea mavuno (hali mbalimbali utakazopitia maishani mwako mara baada ya mbegu kupandwa)
Sijui unapitia hali gani ila nipo hapa kukufahamisha hivi, unapitia hayo yote kwa sababu kuna aina ya fikra ulizozipanda ubongoni mwako ambazo zimekufanya uvune hayo yote!
Hata hivyo tafiti nyingi za kisaikolojia kuwahi kufanyika zimeonesha kwamba, watu wa kawaida huishia kutumia 3% tu ya ubongo wao!
Jaribu kufikiri mtu anapanda mbegu Kwa asilimia ndogo kiasi hicho je atapataje mavuno Kwa asilimia 100%?
Yaani mbegu yako unayopanda kupitia fikra ni sawa na hakuna kitu, sasa wewe utakuwaje kitu ilihali kile ulichopanda sikitu?
Unatakiwa kufikiri tena juu ya suala hili...
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba fikra ni kama injini ambayo huratibu maisha ya kila binadamu, na hii ni kwa sababu mawazo yakitengenezwa ndiyo hupelekea mambo yatokee!
Kwa mantiki hiyo kile unachokifikiri ni sawa na unakiumba.
Na, kama unakiumba basi nacho kitakuja kutokea siku moja, ni suala la muda tu...
Habari njema ni kwamba, kitu pekee ambacho mwanadamu unaweza ukakitawala hapa duniani ni fikra zako tu, kwamba unaweza kuchagua fikra zozote kuhusu jambo fulani lililopo mbele yako!
Kinacholeta faraja na tumaini kubwa ni kwamba, moja ya viumbe vilivyopendelewa na Muumba ni binadamu pekee yake, kwanini nasema alipendelewa?
Ni kwa sababu binadamu kapewa ubongo umsaidie katika kufikiri na ili aweze kuvumbua vitu!
Hii inamaanisha kwamba wewe kama binadamu una wajibu wa kutumia fikra zako ili upate matokeo unayoyataka..
Kutokana na hilo unatakiwa kujua kwamba utakuwa kwa kadri ya vile unavyojifikiria!
Ndugu, unatakiwa kufahamu kwamba ili uweze kubadili chochote kile katika maisha yako, ni lazima uanze kubadili fikra zako kwanza!
Na kama hutobadili fikra zako hutobadili matokeo yako, kwani ili upate matokeo ambayo hukuwahi kuyapata ni lazima ukubali kutengeneza fikra ambazo hukuwahi kuzitengeneza!
Watu wengi sana wamejikuta katika hali ya sintofahamu, hasa wakiangalia mienendo ya maisha yao pamoja na hali wanazopitia..
Kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, ndivyo na hali hizo zinavyozidi kwenda hatua mbaya Zaidi, wasijue shida ni nini...
kumbe, shida ni wao wenyewe kupitia aina ya fikra wanazozitengeneza!
Mbali na hilo ni kanuni ya ulimwengu mzima kwamba, "maji hutiririka kufuata mkondo, vivyo hivyo na maisha yako yatatiririka kufuatana na fikra zako mwenyewe"
Kwa mantiki hiyo kila fikra ni kisababishi na hali yoyote ile unayopitia ndiyo ni matokeo yake.
Kwa mfano: umaskini, hali ngumu ya maisha, mikosi, kipato, uhusiano tete, kutokuthaminiwa na mengine kama hayo...
Ukiachilia mbali hilo kanuni ya uvutano inasema kwamba "wewe ni kama sumaku inayoishi, kwamba unaweza ukavuta watu, matukio, hali, mafanikio na kitu chochote kile ambacho kitapatana na fikra zinazotawala maisha yako"
Kwa mujibu wa kanuni hii ni kwamba siyo kila kitu unaweza ukakivuta, ila utakivuta kile kitakachopatana na fikra zako!
Je ni kipi kinatawala fikra zako Kwa asilimia kubwa?
Unatakiwa kujua kwamba utavuta vitu vitakavyopatana na fikra zinazotawala mfumo wa maisha yako!
Mambo ya msingi unayopaswa kuyajua kuhusu uhusiano wa Fikra zako pamoja na kanuni ya uvutano:
๐น Fikra za uhaba huvuta uhaba...
๐น Fikra za mafanikio huvuta mafanikio...
๐น Fikra za umaskini huvuta umaskini...
๐น Fikra za kushindwa huvuta kushindwa...
๐น Fikra za furaha huleta furaha...
๐น Fikra za matumaini huleta matumaini...
๐นFikra za kuweza huvuta uwezo...
๐น Fikra za huzuni huleta huzuni...
๐น Fikra hasi huvuta matukio hasi...
๐นFikra chanya huvuta matukio chanya..
๐น Fikra za utajiri huvuta utajiri...
"Yule anayefikiri anaweza ataweza, ikiwa yule anayefikiri hawezi hataweza"
Kuweza au kutokuweza siyo kitu halisi, na hakuna ambaye aliumbwa hawezi au anaweza, bali sote tumezaliwa tunaweza ila aina ya fikra tunazotengeneza ndizo hututofautisha..
Mwingine ajione anaweza, ilihali mwingine ajione hawezi!
Je mpaka hapa ni aina gani ya fikra zinazotawala maisha yako?
Unatakiwa kujua kwamba, kile unachokifikiri ndicho unachokivuta...
Kwa mantiki hiyo huna budi kufahamu kwamba, hata hali zote unazopitia katika maisha yako umezivuta kutokana na fikra zako!
Je umechoka na hali unazopitia maishani mwako?
Kama jibu ni ndiyo basi huna budi kubadili fikra zako kwanza!
Yes boss, badili fikra zako badili maisha yako! Yaani (change your thinking change your life)
Kumbuka unachopata kwenye maisha ni uakisi wa kile unachotengeneza ubongoni mwako kupitia fikra!
Na ndiyo maana hata Neno la Mungu linasema kwamba "maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo" kasome mithali 23:7
Kwamba vile unavyojiona (kupitia fikra zako), ndivyo unavyokuwa (maisha yako halisi)...
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; mwalimu, mwandishi muelimishaji katika eneo la maendeleo Binafsi, life coach and consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329
Comments
Post a Comment