Jinsi Ya Kuanza Upya Tena... mbinu ya 6&7
6. Badili Tabia Zako
Huwezi ukapata matokeo mapya kama hutabadili tabia zako.
Kwani ukiwa ni mtu wa kuendelea kufanya tabia zilezile huwezi ukapata matokeo ya tofauti na yale ambayo huwa unayapata siku zote.
Unatakiwa kujua kwamba mafanikio ni kitu unachokivuta kutokana na mtu unayekuwa.
Na, umekuwa hivyo kutokana na mjumuisho wa tabia zako zote uzifanyazo.
Hii inamaanisha kwamba umejitenegeneza mpaka ukawa hivyo ulivyo mbali na ukweli kwamba uliumbwa na Muumba.
Kumbuka kwamba tabia zako zikishakomaa huanza kukutambulisha kwa watu, hivyo watu watakutambua wewe ni nani kutokana na tabia zako.
Unatakiwa kujua kwamba hapo ulipo na hivyo ulivyo ni kwa sababu yako mwenyewe pamoja na tabia zako.
Huenda ulikuwa ni muumini wa kuweka visingizio, huenda ulikuwa ni muumini wa kughairisha mambo, huenda ulikuwa ni muumini wa kutokuwajibika ipasavyo, huenda ulikuwa ni muumini wa kulaumu na kutaka kuonewa huruma, huenda ulikuwa ni muumini wa kutumia muda wako vibaya, huenda ulikuwa ni muumini wa kusubiri mambo yakae sawa na hayajakaa sawa, huenda ukawa ulikuwa ni muumini kutokujifunza, huenda ulikuwa ni muumini wa kukaa tu vijiweni pasipokuwa na cha maana kilichokupeleka huko, huenda ulikuwa ni mtu unayeishi tu kwa sababu uko hai ila hujui kwanini unaishi…
Ndugu inatosha sasa, huu ni wakati wa kubadili maisha yako, huu ni wakati wa kuanza upya. Unachopaswa kufanya ili kubadili maisha yako huna budi kufutililia mbali tabia zote hatarishi ambazo zimekufanya upate matokeo mabaya na kuanza upya kwa kuanza kufanya tabia zifuatazo:
Acha tabia ya kughairisha mambo, acha tabia ya kuweka visingizio, tumia vema muda wako, pokea wajibu kuhusu maisha yako, jiboreshe kila iitwapo leo, fanya kazi kwa juhudi na bidii, jinenee mema, kuwa na mitizamo chanya, jitume, dumu katika fikra chanya muda wote, dumu katika kufanya tabia njema, jitengenezee Imani thabiti kuhusu uwezo wako…
Endapo utatengeneza tabia mpya utakuwa ni sawa na umeanza upya kwani hutakuwa wewe wa zamani tena, bali utakuwa wewe mwingine, hivyo utabadili kabisa historia ya maisha yako…
Kumbuka umefika hapo ulipo kwa sababu ya tabia zako, hii inamaanisha ukibadili tabia zako utafika mbali zaidi ya hapo uipofika!…
7. Sahau Ulichofanya Kipindi Cha Nyuma
Huwezi ukaanza upya kama utawekeza nguvu katika mambo yaliyotokea kipindi kilichopita.
Na, ifahamike kwamba, maisha ya binadamu yanaweza kugawanywa katika nyakati tatu yaani, wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao! Katika hali ya kawaida huwezi ukadhibiti wakati uliopita!
Mbali na ukweli huo bado kuna watu, ambao wamewekeza nguvu na juhudi zao kwa kujutia pamoja na kulaumu kuhusu wakati uliopita.
Kwa namna hii huwezi ukaanza upya…
Kuna watu wanatumia muda wao wa thamani kujutia: nafasi walizopoteza, bahati walizopoteza, nafasi walizochezea na mambo yote mazuri waliyopoteza wakati uliopita, nipo hapa kukumbusha kuwa hayo majuto hayabadilishi kitu.
Badili mitazamo yako juu ya kilichotokea na kuamua kuanza upya, kumbuka hakuna kiwango cha majuto kinachoweza kudhibiti kilichotokea.
Kwa kulitambua suala hili kindakindaki wahenga nao hawakuwa nyuma wakasema "yaliyopita sindwele tugange yajayo".
Kwanini unalaumu kuhusu nafasi ulizopoteza jana wakati kesho ipo? Kwanini usiitumie leo kutengeneza kesho yako?
Hata utumie muda gani kufikiri kilichotokea wakati uliopita huwezi kubadili kitu, huo ni ukweli mchungu upokee kama ulivyo.
Hata hivyo kama utakubaliana na mimi utaona kwamba wakati huu uliopo ndiyo fursa yako kubwa na ndiyo nafasi yako nzuri ya wewe kuitengeneza kesho yako kwa kuanza upya.
Kumbuka wakati mzuri wa kutabiri kesho yako ni kupitia kuitengeneza leo yako.
Hata hivyo wakati wako ujao kwa kiasi kikubwa unategemea sana kile unakifanya leo, je unafanya nini?
Usipoanza upya hakuna kitakachotokea, kutokana na hilo ndiyo maana nipo hapa kukusihi uanze upya, na usipoanza upya utaendelea kubaki kuwa wewe wa zamani…
Hitimisho: kuanza upya siyo kushindwa bali ni ushindi! Kwani asiyekubali kushindwa si mshindani.
Huenda ilikuwa ni biashara, huenda yalikuwa ni mahusiano, huenda ilikuwa ni kazi, huenda uliingia mkataba sehemu Fulani na huna tena tumaini kuhusu hilo, nipo hapa kukusishi uanze upya.
Ndugu kuanza upya ni uamuzi mzuri kwani ukibaki eneo lilelile huwezi ukabadilisha kitu…
Na ndiyo maana hata nyoka hujitoa ngozi yake ya nje ili apate ngozi mpya, hata wewe unaweza ukaamua kujitoa hapo ulipo kwa kuanza upya!
Unatakiwa kujua kwamba hakuna kitu kibaya kwenye kuanza upya.
Hivyo basi ikitokea kuna hatua umefika ukajikuta huelewi wewe anza upya tena…
Ahsante sana kwa kuwa mwanafamilia na mfuatiliaji wa masomo haya.
Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e; Mwandishi, Mwalimu, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life & Consultant!
Unaweza kuwasiliana name kupitia whatsapp no +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment