Jinsi Ya Kupata Matokeo Unayoyataka... Mbinu Ya 2&3
2. Tafuta Njia Zitakazokusaidia Ili Ufanikiwe Kupata Kile Unachokitaka...
Kujua unachokitaka siyo kigezo cha kukipata, bali ni lazima uweke wazi njia zitakazokusaidia ili upate hicho unachokitaka.
Rafiki, hakuna matokeo ambayo hujitengeneza yenyewe pasipo njia zitakazochochea matokeo hayo…
Na, ndiyo maana hata katika hesabu huwezi kupata jibu pasipo kutumia formula/njia fulani. Hebu jaribu tu kuvuta picha utapateje jibu (matokeo) pasipo kutumia njia fulani itakayokuletea jibu hilo (matokeo hayo)?
Hii ni sawa na kusema, katika kila utakachokitaka kuna njia utakayopsawa uitumie ili ikusaidie uweze kukipata kitu hicho!
Na, ndiyo maana niko hapa kukukumbusha kuwa ukishajua unachotaka lazima udokeze mbinu utakayopasawa uitumie ili ukipate!
Kwa mfano katika hoja ya kwanza nilisema kwamba ninachokitaka ni “kuongeza pato langu la mwezi lifikie 300,000/=” kwa mantiki hiyo itabidi niweze kuja na njia ambazo zitanisaidia ili niweze kuyapata matokeo hayo ninayoyataka.
Kwa mfano ninaweza kuja na njia zifuatazo: ➡️Kutafuta kazi nyingine/ kuongeza kazi nyingine ya muda wa ziada itakayonitengenezea pato la pili! (part time job)...
➡️Kuongeza mifereji ya kipato changu kwa kuwekeza pesa yangu katika maeneo mbalimbali, hali itakayoongeza pato nitakalolitengeneza...
➡️ Kutafuta elimu ya fedha na uwezekaji, elimu hii itanisaidia katika kuidhibiti fedha isipotee, niweze kutumia fedha yangu kwa usahihi pamoja na kunisaidia niweze kuifanya fedha yangu ijizalishe!
➡️ Kuweka akiba yangu binafsi, njia hii itanisaidia niweze kukuza pato langu!
➡️Kujiwekea utaratibu wa kuwa na bajeti, njia hii itanisaidia niweze kudhibiti mianya yote iliyokuwa inapoteza fedha yangu!
Unatakiwa kujua kwamba, kujua njia itakayokusaidia ili upate kile unachokitaka ni jambo la msingi, kwa maana njia ni muhimu zaidi kuliko hata kile unachokitaka…
Na, hii ni kwa sababu ni kupitia kutumia njia fulani ndipo sasa utapata matokeo ya kile unachokitaka, na endapo hautaazimia kuweka wazi njia utakazotumia huwezi kupata kile unachokitaka!
Jambo moja unalopaswa kuepuka hapa, ni kutaka kutumia kila njia.
Rafiki siyo kila njia itakuongoza na kukupeleka kule unakotaka ufike.
Unatakiwa uchague njia sahihi zitakazokusaidia uweze kupata matokeo unayoyataka.
Hata hivyo unaweza ukaja na orodha ya njia nyingi zinazoweza kukusaidia ili upate kile unachokitaka, hivyo basi kabla hujaichagua njia mojawapo miongoni mwa njia ulizoziorodhesha unatakiwa ujiulie hili; "je, hii njia itanisaidia kweli kupata yale matokeo ninayoyataka?"
Kumbuka siyo kila njia itakusaidia upate matokeo unayoyataka kwa urahisi na kwa wakati. Na, ndiyo maana umakini unahitajika katika kuchagua njia sahihi itakayokupa matokeo ya kile unachokitaka kwa urahisi na kwa wakati muafaka!
3. Badilisha Mfumo Wako Wa Kuamini...
Ukishaweka wazi kile unachokitaka ni lazima uamini kwamba utakipata.
Na, ndiyo maana kanuni ya kuamini inasema kwamba, “chochote kile utakachokiamini kuhusu wewe na dunia yako kitafanyika kwako pamoja na dunia yako kama uaminivyo”
Hii inamaanisha kwamba, ukiamini kwamba haya matokeo nitayapata, nawe utayapata kweli kwa sababu umeamini kuwa utayapata.
Kumbuka “nawe utapokea kwa kadri ya uaminivyo”
Hata hivyo ukija katika maandiko matakatifu mwinjili Marko 11:24 anasema kwamba;
“kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu”
Unatakiwa kujua kwamba sala ni jambo lolote lile unalolitamani uweze kulipata, hii inamaanisha kwamba hata yale matokeo unayoyataka ni kama sala kwa sababu ni jambo unalotaka ulipate…
Kwa mantiki hiyo ukiweza kubadilisha mfumo wako kuamini na kuona kwamba utalipata, nawe utalipata kwa sababu imani yako ipo kwenye kulipata jambo hilo na huenda umekuwa ukilitamani ulipate kwa muda mrefu!
Mbali na hilo ukisoma waebrania 11:1 Neno la BWANA linasema kwamba “Basi imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.
Chukua hili, “kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo” halafu weka kichwani mwako!
Mpenzi msomaji unatakiwa uwe na hakika juu ya kile unachokitaka kwamba utakipata!
Ukweli ni kwamba utaweza kukipata kwa sababu imani yako imeshaamini hivyo! Kumbuka imani haijawahi kumsaliti muamini wake!
My friend unatakiwa uamini katika kuamini! Kwani nawe utapokea kwa kadri ya uaminivyo!
Badili mfumo wako wa kuamini, baada ya hapo amini kwamba kile unachokitaka utakipata, na endapo utaamiini hivyo nawe utakipata!
Na, unatakiwa kudumu katika Imani hiyo muda wote!
Kwani ni wale wenye imani thabiti tu, juu ya kile wanachokitaka ndio hupata matokeo yanayoakisi imani yao juu ya kitu hicho!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya!
Somo Lihusulo Jinsi Ya Kupata Matokeo Unayoyataka Litaendelea kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza ukawasiliana na Mimi kupitia Whatsapp No +255673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment