Huwezi Ukawa Mtu Ambaye Hujamuona...
Awali kwenye makala iliyopita niliishia kudokeza kuhusu andiko lililopo kwenye methali 23:7 "maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo"
Sasa tuendelee...
Unatakiwa kujua kwamba vile unavyojiona ndani ya nafsi yako, ndivyo unavyokuwa nje ya maisha yako!
Na, ndiyo maana kisaikolojia inaaminika kwamba, kila kitu huanzia ndani ya nafsi kwanza, ndipo sasa hujidhihirisha nje.
Hivyo basi, endapo ndani ya nafsi yako utajiona wewe ni fungu la kukosa, mnyonge na si kitu nawe utakuwa hivyo nje ya maisha yako.
Na ndiyo maana kanuni ya mwitikio na vitendo inasema kwamba; “matendo yako ni mwitikio wa fikra zako mwenyewe"
Hii inamaanisha kuwa, utaonesha mwitikio fulani kutegemeana na fikra ulizoziwasilisha juu ya namna ulivyojiona, na mwitikio huo unaweza kuwa wa kipumbavu au wa kikuu!
Na, ifahamike kwamba upumbavu au ukuu wa mwitikio wako, utategemeana na aina za fikra utakazokuwa umeziwasilisha kukuhusu wewe mwenyewe!
Kutokana na hilo huna budi kufahamu kuwa maisha yako ya nje yanategemea sana kile unachokiona ndani ya nafsi yako!
Na, ndiyo maana kanuni ya uakisi wa mambo inasema; “ulimwengu wako wa nje huakisi ulimwengu wako wa ndani"
Kwa mantiki hiyo ni muhimu ubadili namna unavyojiona, kwani vile unavyojiona ndani ya nafsi yako ndivyo unavyokuwa nje ya maisha yako!
Je unajionaje wakati huu?
Je unajionaje baada ya miaka mitano ijayo?
My friend unatakiwa kujua kwamba yule unayemuona ndiye unayekuwa, na huwezi ukavuka ukamfikia yule ambaye hujamuona…
Ukiona huwezi kufanikiwa, ni kweli hutaweza kufanikiwa, kwa maana vile unavyoona ndivyo ulivyo…
Ukiona huwezi kupata mahusiano sahihi, ni kweli hutaweza kuyapata, kwa maana namna aonavyo nafsi mwake ndivyo alivyo.
Ukiona huwezi kufanikiwa kiuchumi ni kweli kabisa hutaweza kufanikiwa kiuchumi, kwa maana umejiona hivyo.
Ukiona huwezi kupata kazi nzuri hutaweza, kupata ndiyo kwa sababu umeona hivyo…
Ukiona utaishia kuwa maskini, nawe utaishia kuwa maskini kwa sababu umejiona hivyo.
Ukiona huwezi ukavuka kiwango cha juu zaidi ya hapo ulipo, hutaweza ndiyo kwa maana yule unayemuona ndiye unayekuwa…
Ukiona huwezi kuwa mtu mkuu hutakuwa mtu mkuu ndiyo, kwa maana huwezi ukaenda mbali zaidi ya pale ulipoishia kujiona.
Ukiona uliumbwa uje uteseke, ni kweli utaishia kuteseka maisha yako yote kwa sababu umejiona hivyo.
Ukijiona huwezi, ni kweli hutaweza kwa sababu umejiona hivyo.
Ukiona wewe ni mnyonge utabaki kuwa mnyonge kwa maana ni wewe mwenyewe umejiona hivyo.
Ukiona wewe ni fungu la kukosa, utaishia kukosa maisha yako yote kwa sababu umejiona hivyo.
Ukiona hustahili, ni kweli hutastahili hata mara moja kwa sababu umejiona hivyo.
Unachopaswa kujua ni kwamba, maisha ya binadamu ni matokeo ya fikra zake mwenyewe.
Yaani kama vile ilivyo kwenye kanuni ya mtiririko wa maji kwamba, maji hutiritrika kwa kufuata mkondo pamoja na mkao wa kijiografia vivyo hivyo na maisha yako yatatiririka kutegemena na vile unavyojiona!
Na, ifahamike kwamba unaona dunia na vyote vilivyomo kutokana na wewe ulivyo na siyo kwamba vitu hivyo viko hivyo, na vinapaswa vionekane hivyo!
Mbali na hilo unaipa dunia na vyote vilivyomo tafsiri Fulani kutokana na wewe ulivyojipa tafsiri, na siyo kwamba vinastahili kupewa tafsiri hiyo.
Hii inamaanisha kwamba ni mengi umeyaona kuwa yapo vile na mengi umeyapa tafsiri kwamba yapo hivi ama vile ilihali hayapo hivyo!
Na, ndiyo maana kuna wakati unajikuta upo hauna uhuru na huwezi ukafanya mambo Fulani, kumbe tatizo siyo kukosa uhuru bali tatizo ni namna unavyojiona.
Kwamba unajiona katika kiwango cha chini sana ndiyo maana unajikuta dunia yako ni ndogo sana kiasi kwamba huwezi ukaifanyia mambo makubwa!
Kwanini Watu Wengi Hujiona Katika Udhaifu Na Siyo Ukuu?
Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba hakuna binadamu hata mmoja ambaye huzaliwa akiwa na mtizamo Fulani kuhusu maisha au akuhusu dunia yake.
Suala hili lilithibitishwa na nadharia ya blank slate iliyoelezwa na Mwanafalsafa mmoja kuwahi kutokea hapa duniani, akifahamika kwa jina la David Hume.
Kwa mujibu wa nadharia hiyo ni kwamba “hakuna mwanadamu ambaye huzaliwa akiwa na wazo, mtizamo au uelewa wowote juu ya jambo Fulani”.
Madai ya nadharia hii yakahitimishwa kwa kuona kwamba vile mwanadamu atakuwa (jinsi anavyojiona), ni kutokana na masuala kadhaa aliyokutana nayo wakati wa ukuaji wake mara baada ya kuanza kuishi hapa duniani!
Kutokana na hilo unatakiwa kujua kwamba hivyo ulivyo huenda hukupaswa uwe hivyo; ila umekuwa hivyo na unavyojiona hivyo kwa sababu ya mambo yote uliyoingiliana nayo wakati wa ukuaji wako, kwamba kuna taarifa Fulani zimeingizwa kichwani mwako ambapo mwisho wa siku zinakufanya ujione hivyo!
Na, unatakiwa kujua kwamba sisi sote tumejitengeneza mpaka tukawa hivi tulivyo mbali na kuwa tuliumbwa na Muumba.
Na, hii ni kwa sababu na vile tunavyojiona ndivyo tunavyojitengeneza tuwe hivyo na tumeshakuwa hivyo tayari!
Je ni sababu zipi ambazo huwafanya watu wajione kama walivyo?
Usijalii makala ijayo itachambua hilo!
Ahsante sana kuwa mwanafamilia wa masomo haya!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329 au unaweza kutembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment