Kwanini Watu Wengi hujiona vile wajionavyo?

Kila kitu hutokea kutokana na sababu! Kwamba kuna kila sababu iliyopelekea kutokea kwa kila matokeo unayoyaona kwenye maisha yako!
Unatakiwa kujua kwamba, hata hivyo unavyojiona ni kutokana na sababu ambazo zimekufanya ujione hivyo!
Zifuatazo ni sababu ambazo zimekufanya ujione hivyo unavyojiona:

1. Historia Ya Malezi
Sisi sote ni matokeo ya historia zetu, kwamba tumekuwa hivi tulivyo kutokana na kile historia imetufanya!
Kutokana na ukweli huo huna budi kufahamu kwamba, historia ya malezi ndiyo imewafanya watu wengi wajione wao ni duni, dhaifu na hawawezi! 
Na, ndiyo maana watu wengi tunajiona sisi ni wanyoge, hatuwezi, ni wadhaifu, hatustahili pamoja na kujiona kuwa hakuna kitu cha maana tunachoweza kukifanya hapa duniani!

Kwa mfano kama ulipokuwa mtoto:  ulikosolewa sana, ulidharauliwa sana, uliitwa majina ya ajabu pamoja na kufananishwa na viumbe vya ajabu, ulipigwa sana, ulipokea manyanyaso ya hapa na pale, ulizuiwa kuongea, uliambiwa huwezi kufanya jambo Fulani, uliambiwa huwezi kuwa mtu Fulani, n.k. 
Maana yake ulitengenezwa ujione wewe ni mdhaifu na hustahili!
Na, ndiyo sababu kubwa ambayo imekufanya Mpaka sasa ujione hivyo unavyojiona!

Hii inamaanisha huwezi ukafanya kitu kitakachokuwa zaidi ya hayo matendo uliyofanyiwa pamoja na kauli ulizoambiwa na watu wako waliokuzunguka, kwa sababu zimeathiri fikra zako. 
Kwa mantiki hiyo historia ya matendo ulofanyiwa pamoja na kauli ulizoambiwa wakati wa kukua ndiyo kwa kiasi kikubwa vimechangia katika kukufanya ujione hivyo.

Na, ifahamike kwamba sote huwa tunajifunza kwa kuiga na kufanya kile ambacho wanaotuzunguka wanakifanya, kutokana na hilo huna budi kutambua kuwa utajikuta ukifanya kile ambacho wazazi wako walikifanya!

Hivyo basi, endapo  wazazi wako walikuwa ni watu wa kujiona wao ni maskini, hawawezi kufanikiwa, waliumbwa wateseke, kwenye ukoo wao huwa hawafanikiwi pamoja na masuala mengine mengi kama hayo, utajikuta ukichukua mitizamo kama yao ambapo mwisho wa siku utaishia kujiona kama wao walivyojiona!
Na, ndiyo maana Wahenga Walisema; "mtoto wa nyoka ni nyoka"

Hivi ndivyo historia ya malezi ilivyokufanya ujione hivyo ujionavyo,  japo sioni unajionaje!

Nini kifanyike? Hutakiwi kuongozwa na historia tena bali badili mitizamo yako kwa kujiona wewe ni bora, unaweza na ulizaliwa uje uwe mtu mkuu!

 2. Marafiki
Kisaikolojia inamaanika kwamba akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine, kwa mantiki hiyo si ajabu ukajikuta ukifanya kile ambacho marafiki wanaokuzunguka wanakifanya! 

Na, kama akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine maana yake, ni rahisi hata wewe kuwa na mitizamo kama yao. 
Kutokana na hilo unatakiwa kujua kwamba vile watakavyokuwa wanajiona hata wewe utajikuta ukianza kujiona kama wao! 

Yaani, pasipo kujua utajikuta ukiwafanya marafiki zako wawe kama kioo cha wewe kujitizamia, na endapo itatokea utakuwa upo kinyume nao utajirekebisha ili uendane nao!

Hivyo basi utajikuta kila kitu utakifanya kwa kuangalia angle ya vile wao wanavyijiona mwishowe utajikuta ukijiona kama wao wajionavyo!

Wahenga walipata kusema, "ndege wanaofanana huruka pamoja". 
Hii inamaanisha kwamba watu unaoamua kushinda nao maana yake mnafanana nao kila kitu. 
Kumbe sasa endapo utashinda na watu fulani Kwa muda mrefu, utajikuta ukijitengeneza kimtizamo na kuanza kujiona kama vile wao wanavyojiona. 

Angalizo: endapo marafiki zako watakuwa ni watu wa kujiona wao ni: duni, hawastahili, hawawezi, dhaifu, waoga, n.k.
Nawe utaanza kujiona kama wao, mwisho wa siku utajitengenezea ukomo wa pale utakapofikia kimaisha kwa sababu marafiki zako wamekufanya ujione wewe ni wa viwango vile walinavyo!

Je huwa unajiona kwa kuakisi vile marafiki zako walivyo au kwa kuakisi vile ulivyo?
Unatakiwa kujua kwamba ni ngumu sana kwenda kinyume na kile marafiki zako wanakifanya, na hii ni kwa sababu akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine!

Ni vema ukabadili marafiki ili upate kuwa mtu bora na mwenye mitizamo chanya, endapo marafiki zako ni watu hasi!

3. Mazingira
Ni nguvu isiyoonekana ambayo humtawala mwanadamu kuanzia fikra zake, tabia zake, mwenendo wake pamoja na namna anavyojiona.
Unatakiwa kujua kwamba mazingira uliyokutana nayo ndiyo yamekufanya uweze kujiona hivyo unavyojiona.
Hii inamaanisha kwamba hivyo unavyojiona kama: huwezi, hustahili, wewe ni mnyonge pamoja na vyovyote vile unavyojiona. 
Ni kwa sababu mazingira yaliyokulea yamekukuza na kukufanya ujione hivyo.
Huenda ukawa unajiuliza mazingira haya ni kama yapi? 
Unatakiwa kujua kwamba sehemu uliyosoma imekuathiri, mahali unaposhinda kila siku pamekuathiri, mahali unaposali pamekuathiri, mahali unapoishi pamekuathiri pamoja na mazingira yote yanayokuzunguka kila wakati yamehusika sana katika kukutengeneza na kukufanya ujione hivyo unavyojiona.
Kadhalika ni muhimu ukatambua kwamba, mazingira yanaweza kukujengea fikra za uhaba mpaka ukaona hakuna kitu unachoweza ukakifanya na kukikamilisha hapa duniani.

Na, ifahamike kwamba mazingira yenye uhaba yatakufanya ujione kiupungufu, kidhaifu na kinyonge, ikiwa mazingira yenye utele yatakufanya ujione unaweza, unastahili na unaweza ukaibadilisha dunia yako.
Kuna wakati unajiona wewe siyo kitu kabisa, na siyo kwamba wewe siyo kitu bali mazingira yaliyokukuza ndiyo yanakufanya ujione hivyo.

Nini kifanyike? Ili uweze kubadili namna ya kujiona huna budi kuhama mazingira uliyopo ambayo yamekufanya ujitengenezee mtizamo duni kuhusu wewe mwenyewe!
Sababu kubwa ni kwamba, ukiendelea kubaki mazingira yaleyale utaendelea kupata athari zilezile kwa mantiki hiyo utaendelea kujiona katika viwango duni.
Ahsante sana kwa kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya!
Sababu zingine zitaendelea kudokezwa kwenye makala zijazo!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, mwandishi, muelimishaji katika eneo la maendeleo Binafsi, life coach and consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...