Kwanini Watu Wengi Hujiona Vile Wajionavyo?... sehemu ya pili

Makala iliyopita ilifanikiwa kudokeza sababu tatu ambazo humfanya mtu ajione vile ajionavyo.
Sababu hizo zilikuwa ni kama zifuatazo:
👉Historia ya malezi
👉Mazingira
👉Marafiki
Makala hii ni mwendelezo wa somo lililopita!
Ninakukaribisha sana twende pamoja!
Tuendelee na sababu ya nne:

4. Elimu Uliyopokea/Uliyopewa
Kile unachokijua kupitia elimu uliyonayo ndicho kitakachopima umbali utakaoishia kujiona! 

Kwa mantiki hiyo endapo utajua vitu vingi utajiona katika uweza, ukuu na ubora, ikiwa endapo utajua vitu vichache utajiona wewe ni duni, dhaifu na huwezi, hivyo utaishia kuwa na mitizamo duni dhidi yako! 

Kwa namna moja ama nyingine elimu nayo, kama sababu ni moja ya kitu ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuwafanya watu wajione katika viwango duni.
Suala hili limechangiwa sana na kile wanachofundishwa shuleni! Yaani kile kinachoingizwa ubongoni mwao kupitia elimu wanayoipata!

Unachopaswa kujua ni kwamba, elimu nyingi za kitaaluma, hazina utaratibu wa kuwafundisha wajifunzaji wajijue wao ni nani, wanamiliki nini ndani yao na wanaweza wakafanya nini!

Badala yake sasa zinalenga katika kuwapa mafunzo ya kuwaandaa waje wawe wafanyakazi wa umma, watumishi pamoja na waajiriwa.
Na, endapo itatokea wamekosa hizo ajira wataambiwa wakajiajiri ikiwa elimu ya kujiajiri hawajapewa! Inasikitisha sana...

Nilipokuwa nikilichunguza suala hili kwa umakini ndipo sasa nikaona kile kilichodokezwa kwenye kanuni ya input and output kinajidhihirisha kwa uwazi kabisa! 
Kanuni hii inasema “kile kinachoingia ndicho kitapima kile kitakachotoka" 
Kwa mujibu wa kanuni hii, huna budi kufahamu kwamba kile kitakachoingia ndani ya ubongo wako ndicho kitakachotoka, na ni ngumu sana kutoa kitu kingine kitakachokuwa tofauti na kile kilichoingia! 

Hivyo basi endapo utaingiza taarifa zilizopitwa kupitia kile elimu yako inakufundisha, utajikuta unakuwa ni mtu wa kutoa mawazo yaliyopitwa na wakati vilevile.
Na kwa sababu elimu tunayopewa haitulengi sisi tuweze kujijua kiundani zaidi ya kutufanya tuwe waajiriwa, basi tutajikuta tukijiona sisi ni watu wa kuajiriwa na hatuwezi tukafanya kitu kingine nje na kuajiriwa.
Hii inamaanisha kwamba elimu yetu ndiyo imetufanya tuweze kujiona hivyo, kwamba tunastahili kufanya vitu vilivyopo ndani ya taaluma tuliyosomea tu. 
Na si vitu vingine kitu ambacho siyo kweli!

Ukiachilia mbali hilo, kuna watu hujiona wao kama siyo kitu eti kwa vile hawajasoma.
Kwamba kutokana na kushindwa kuendelea na ngazi za juu za masomo, basi hujikuta wakijona wao siyo kitu, hawawezi, hawastahili na hawana akili eti kwa vile walifeli mitihani.

Unatakiwa kujua kwamba hakuna mtu ambaye alizaliwa hastahili, hawezi, na mdhaifu bali tunajiona hivyo kwa kupitia angle ya elimu!

Endapo unataka ubadilishe namna unavyojiona huna budi kuanza kutafuta maarifa mapya hasa yale yanayolenga eneo la maendeleo binafsi hapo ndipo utakapojijua wewe ni nani na unaweza ukafanya nini.

5. Jinsia
Kuna watu wanajiona wao ni duni, dhaifu, wanyonge, hawastahili na hawawezi eti kwa vile wana jinsia Fulani.

Mpenzi, unatakiwa kujua kwamba kuwa mwanaume au mwanamke ni kama lebo tu ila unaweza ukafanya mambo makubwa tu!

Hivi aliyekwambia kwamba ukiwa mwanamke ujione huwezi ukafanya jambo Fulani ni nani? Kwani kuna uhusiano gani kati ya wewe kuwa mwanamke na kufanya jambo Fulani au kutokufanya jambo Fulani?

Au kuna uhusiano gani kati ya uanaume wako pamoja na kuweza kufanya jambo Fulani, au kutokufanya jambo Fulani?

Ndugu, kama ni akili sote tunazo, kama ni uwezo sote tunao, kama ni nguvu sote tunazo, kama ni maisha sote tunayo!
Hii inamaanisha pasipo kujali tofauti za jinsia zetu sote kwa pamoja tuna uweza wa kufanya mambo yatokee. 
Kwanini sisi ndiyo vifaa vya uzalishaji wa maisha yetu! Yafaa tujione hivyo na siyo kuhusisha na jinsia zetu!  

6. Upekee Uliozaliwa Nao!
Ni ukweli usio na kipingamizi kwamba hatuwezi kujiona sawa, kwa sababu ya upekee wetu. 
Kwamba kila mtu ana upekee wake na sisi wanadamu huwa hatufanani!

Unachopaswa kujua ni kwamba wewe ni wa kipekee sana, una kusudi la kipekee, una maisha ya kipekee, hakuna aliyewahi kuwa kama wewe na hatatokea mtu atakayekuwa kama wewe tena hapa duniani, hii inamanisha kwamba upo hai ili kuuishi upekee wako.
Kwa mantiki hiyo kujiona kipekee ni jambo la kawaida kabisa! 

Na, ifahamike kwa uwazi kabisa kwamba, mbali na kuwa upekee wetu haufanani, hautakiwi ufanye upekee wako kiwe kigezo cha wewe ujidharau, ujidunishe, ujione wewe ni mjinga, huna akili, huwezi na hustahili!

Unachopaswa kujua ni kwamba, upekee wetu upo kwenye uwezo wa kufanya jambo Fulani kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na watu wengine ambao nao wanafanya jambo hilohilo!

Kwa mfano mimi, huwa najiona kuwa ni bora, naweza, nastahili na nina uwezo mkubwa kwenye kuandika na siku moja nitakuja kuwa mwandishi mkubwa kuwahi kutokea hapa duniani!

Je wewe upekee wako ni upi? 
Kumbuka ukiweza kudokeza upekee wako, ndiyo utakuwa mwanzo wako wa kuanza kujua eneo ambalo uko vizuri hali ambayo itakufanya ujione wewe ni bora.
Na hii ni kwa sababu utakuwa unakadiria eneo hilo ulilo bora na jinsi ubora huo utakavyokutoa kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine!

7. Imani Uliyowekeza Juu Yako..
Imani uliyoiwekeza kwako ina nguvu sana katika kukuathiri jinsi unavyojiona! 
Kwamba endapo utaamini wewe huwezi, ni dhaifu, duni, huwezi, hustahili, huna akili, wewe siyo kitu basi utaishia kujiona hivyo na huwezi ukatoka ukaenda hatua ya juu zaidi ya hapo ulipoishia kujiona!

Ndugu unatakiwa kujua kwamba imani haijawahi kumsaliti muamini wake, kwamba ukiweka imani nzuri kuhusu wewe, utaanza kujiona katika viwango bora hali ambayo itakufanya ujipe ukuu na mamlaka ya kubadilisha maisha yako!

Kumbuka kile kanuni ya kuamini inachosema, “chochote kile unachokiamini kuhusu wewe na dunia yako kitafanyika kwako na dunia yako kama vile uaminivyo”. 

Hii inamaanisha kwamba ukijiwekea imani kwamba unaweza, unastahili, una nguvu, unaweza kubadili maisha yako, una akili nyingi na una uwezo wa kufanya mambo yatokee.
Hivyo ndivyo utakavyokuwa na utaanza kujiona hivyo kwa sababu umejiwekea imani nzuri kuhusu wewe na uweza wako!

Kuna wakati mwingine huhitaji ufanye mambo mengi sana, bali unatakiwa ubadili imani juu yako, kwani ukishabadili imani juu yako ndivyo utakavyobadili hata namna unavyojiona.

Habari njema ni kwamba endapo utaamini kwamba wewe unaweza nawe utaweza kweli kwa sababu umeamini hivyo kuhusu uweza wako! 
Kumbuka nawe utapokea kwa kadiri ya uaminivyo!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya!

Mwendelezo wa makala hii utaendelea tena kwa siku ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no 0744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...