Madhara Ya Kuamini Katika Imani Potofu... Sehemu ya Pili
Makala iliyopita ilidokeza Madhara manne yasababishwayo na kuamini katika imani potofu!
Kwa kukumbusha tuliona Madhara Yafuatayo:
Utampoteza Mungu Katika Maisha Yako.
Utaendelea Kubaki Na Hofu
Hutojijua Wewe Ni Nani
Utashindwa kubadili maisha yako!
Kwa siku ya leo tutaona Madhara Mengine Kama ifuatavyo:
5. Utavuta matukio Hasi Maishani Mwako
Ni kweli kabisa kwamba makwazo hayana budi kuja lakini ole wake yule ayasababishaye.
Sasa Kwanini ujisababishie makwazo kwa kuamini katika imani potofu?
Unachopaswa kujua ni kwamba, matukio yote uliyokutana nayo pamoja na hali zote unazopitia katika maisha yako ni mambo yanayotokana na mfumo wako wa kuamini!
Yamkini umaskini umekuzonga, huenda mahusiano yako ni tete, yamkini hali yako ya kiuchumi ikawa ni ngumu sana, yamkini biashara yako haifanyi vizuri, yamkini marafiki zako wamekutenga, yamkini upo gizani na umekata kabisa tamaa, yamkini unapitia maumivu makali sana wakati huu na huenda umepoteza kabisa mpaka hamu ya kuishi…
Nipo hapa kukufahamisha kwamba hayo matukio yametokana na wewe mwenyewe kuamini katika dhana potofu…
Friend, unatakiwa kujua kwamba imani hasi huvuta hali na matukio hasi IKIWA imani chanya huvuta hali na matukio chanya…
Na hicho ndicho kanuni ya uvutano hudokeza. Kwamba kile unachokiamini ndicho utakachokivuta…
Imetosha sasa kuamini katika Imani potofu… raha jipe mwenyewe kwa kutupilia imani potofu kuhusu wewe na dunia yako!
Badili mfumo wako wa kuamini badili maisha yako!
6. Utaishia Kukata Tamaa
Hebu jaribu kufikiri umeamini kwamba huwezi, hustahili na huwezi kuwa chochote kile, je utapata wapi ujasiri wa kuendelea kupambana zaidi ya kuishia kukata tamaa?
Hebu vuta picha, utafanya juhudi ili upate nini ilihali hakuna chochote cha maana ulichokiamini kukipata kwenye juhudi hizo…
Ni lazima tu utaishia kukata tamaa…
Wapo watu wengi ambao wamekata tamaa, na siyo kwamba inatakiwa wakate tamaa bali wamekata tamaa kwa sababu wameamini hawawezi, na siyo kwamba hawawezi kweli bali wameamini kwamba hawawezi!
Ndugu kama una mpango wa kutoka hapo ulipo anza kubadili mfumo wako wa kuamini kwanza! Usipofanya hivyo hakuna chochote kile kitakachotokea!
7. Kupoteza Uelekeo Sahihi Maishani
Hebu jaribu kuvuta picha umeamini katika imani potofu, sasa utapataje uelekeo sahihi ikiwa mfumo wako wa kuamini siyo sahihi.
Jaribu tu kuwaza na kuwazua…
Kwamba imani thabiti inakutaka wewe uende mashariki halafu wewe unaongozwa na imani potofu inayokupeleka magaharibi, jiulize hili swali je utafikaje mashariki?
Bila shaka hutaweza kuifikia mashariki hata kama upo safarini tayari. Na, hii ndiyo maana kamili ya kupoteza uelekeo.
Nina maana gani kusema hivi, maana yangu ni kwamba imani potofu itakufanya upoteze uelekeo wako, badala ya kukupeleka kwenye kweli ya maisha yako.
Kwa mfano tufanye, unaamini kwamba huwezi kufanikiwa, huwezi kuishi maisha yenye furaha na amani, huwezi kufikia uhuru wa kifedha, huwezi ukawa na familia nzuri, huwezi ukawa na maisha mazuri, huwezi kuwa mtu mkuu na daima utabaki kuwa na maisha duni!
Unachopaswa kujua ni kwamba kutengeneza imani hizo juu yako maana yake utakuwa unaendeshwa na imani hizo, mwishowe utajikuta ukielekea gizani badala ya kuelekea nuruni kadri ya siku zinavyozidi kwenda mbele...
Na, kama unaamini hivyo, huo siyo uelekeo wa mtu mwenye imani thabiti kwani mtu mwenye imani thabiti anatambua kwamba bado yuko hai, kwa vile anaelekea kwenye maisha yaliyojaa utele, furaha, amani na mafanikio.
Hivyo basi mtu huyo hawezi akapotezwa na imani potofu…
Yamkini upo hapo huoni nuru wala mwanga na hujui uendako ni wapi.
Ndugu huhitaji kitu kingine zaidi ya kubadili mfumo wako wa kuamini tu…
Badili mfumo wako wa kuamini badili maisha yako!
8. Kudumaa Kifikra
Huwezi ukakokamaa kifikra ikiwa unaamini katika imani potofu.
Unatakiwa kujua kwamba baadhi ya imani hudumaza kabisa fikra zako pamoja na kukuangamiza kabisa.
Kwa mfano unapoamini kwamba “siwezi” maana yake unalaza ubongo, kwa hiyo ubongo wako hautaweza kujishughulisha na chochote kile juu ya jambo hilo.
Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba ubongo wako uliumbwa ili ukue, hivyo basi unapokuwa unaulaza ubongo wako kupitia kuamini katika imani potofu, maana yake unaudumaza ambapo mwisho siku utaishia kufananishwa na mtu mfu aliye hai.
Na hii ni kutokana na ubongo wako kuzalisha mawazo ambayo hayaishi, kumbuka uko hapa kuishi maisha yaliyojaa utele wa furaha, amani na mafanikio…
Ndugu ili ubadili maisha yako inatakiwa ubadili mfumo wako wa kuamini na kujiona kuwa unaweza.
Kwa mfano badala ya kuamini “siwezi” unatakiwa uamini kuwa “naweza”, kwamba ukiamini unaweza maana yake utakuwa unailazimisha akili yako ifikiri ifanye nini ili ufanye hilo jambo, na kwa sababu akili yako haijawahi kushindwa jambo itakuletea majibu halisi juu ya kipi ufanye….
Na hii ndiyo maana halisi ya kuutumia ubongo wako.
Utatambua nguvu za ubongo wako siku utakayoamua kubadili mfumo wako wa kuamini…
9. Utabaki Kuwa Tegemezi
Kisaikolojia tunaamini kwamba kila mtu ni tegemezi, kwamba hakuna mtu ambaye hategemei wengine. Unachopaswa kujua ni kwamba kutegemeana ndiko huyafanya maisha yetu yakamilike.
Kwa mfano huenda ulikuwa unataka kufanya jambo Fulani, lakini unakosa mbinu sahihi ya kufanya jambo hilo, ukaamua kwenda kwa mtu mwingine kuomba ushauri, akakushauri nawe ukalifanikisha jambo hilo, maana yake utakuwa umetegemea mawazo ya mtu mwingine kufanikisha jambo lako.
Sasa kuna watu ambao wamezidi, wameamini kwamba wao ni fungu la kukosa hivyo wanaona ni halali tu kwao kutegemea kila kitu kutoka kwa ndugu jamaa na rafiki…
Watu hawa wanataka kuonewa huruma ilihali wao wenyewe wameshindwa kujionea huruma kutokana na kuamini katika imani potofu…
Sasa, kama wewe mwenyewe umeshindwa kujionea huruma unafikiri ni nani atakayekuonea huruma?
Ndugu, kuonewa huruma siyo hitaji lako la msingi bali hitaji lako la msingi ni kubadili mfumo wako wa kuamini, kwa kuamini kwamba, unaweza kufanya mambo yatokee na siyo kumtegemea mtu mwingine…
Unatakiwa ujihurumie kwanza ndipo sasa uonewe huruma. Jionee huruma kwa kutupilia mbali imani potofu…
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya, Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Kupitia Whatsapp No +255744284329 Au Tembelea Blog Yangu Kwa Kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment