Vile Unavyojiona Ndivyo Unavyokuwa…


Hivi unafahamu kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watu hujiona katika kiwango cha chini sana kiasi kwamba wanashindwa kuvuta hali nzuri maishani mwao?
Unatakiwa kujua kwamba hakuna mwanadamu yeyote yule ambaye huenda mbali zaidi ya pale alipoishia kujiona.

Hata hivyo huna budi ufahamu kwamba vile unavyojiona, ni sawa na unatengenezea ramani itakayokuongoza na kukufikisha pale ulipoishia kujiona.
Hii inamaanisha kwamba pale ulipoishia kujiona ndipo palipo na ukomo wako.
 Kwamba utakomea hapo na huwezi kwenda zaidi ya hapo katika kuishi kwako. 

Na, ndiyo maana ni muhimu sana kuwa makini na mitizamo unayoitengeneza kuhusu wewe na maisha yako kwani hizo ni sawa na ramani zitakazokutoa sehemu moja na kukupeleka sehemu nyingine kimaisha. 

Kwa mujibu wa tafiti binafsi nilizozifanya nimegundua kwamba watu wengi tunaongozwa na ramani zisizo na ukweli wowote ule, hali ambayo imetuponza wengi na kufanya maisha yetu yabaki duni na yasiendelee kabisa! 

Kwa mfano tuchukulie labda upo Kigoma na, hujawahi kufika Mbeya, ila umeamriwa ufike Mbeya… kwa sababu ya ugeni ukaamua kutafuta ramani ili uwe kama msaada, utakaokusaidia ufike Mbeya! 
Sasa yule aliyekukabidhi ramani akachanganya badala ya kukukabidhi ramani ya Kigoma-Mbeya, yeye akakukabidhi ramani ya Kigoma-Kagera. 
Nawe pasipo kujua ukatumia ramani hiyo ukajikuta upo Kagera na siyo Mbeya tena. 

Mfano huo unaonesha jinsi gani ramani tunazotengeneza kutokana na namna tunavyojiona zinavyotuchukua na kutufikisha kwenye vituo tofauti na vile tulivyopaswa tuvifikie! 

Na, ifahamike kwamba hali hii imechangiwa na sisi wenyewe kutokana na vile tunavyojiona! 
Kwamba pale tulipoishia kujiona ndipo palipo na ukomo wetu
Na, kama pale ulipoishia kujiona ndiyo ukomo wako, ni sawa na kusema ramani uliyoitengeneza haitakuchukua na kukupeleka mbali zaidi ya hapo ulipoishia kujiona! 

Kwa mantiki hiyo huna budi kuweka akilini mwako kwamba, vile unavyojiona ni ramani tosha ya kukuchukua na kukufikisha mahali pale ulipoishia kujiona. 

Sambamba na hilo, ni muhimu ukatambua kwamba, suala linalohusu kujiona lipo mikononi mwako.
Kwamba, unaweza ukaamua ujione kama mtu wa kawaida au kama mtu mkuu.

Na, pale utakapoishia kujiona ndipo patakuwav ukomo wako utakaofika kimaisha!  
Na, ndiyo maana kuna usemi maarufu usemao “yule unayemuona ndiye unayekuwa”

Hii inamaanisha kwamba endapo utajiona wewe ni mtu wa kawaida utaufikia ukawaida katika kuishi kwako, na endapo utajiona wewe ni mkuu utaufikia ukuu katika kuishi kwako, kwani yule unayemuona ndiye unayekuwa.

Fahamu Kuhusu Makundi Mawili Ya Watu…
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika kuhusu watu, hasa linapokuja suala la mitizamo yao pamoja na namna wanavyojiona makundi nawili ya watu yalipatikana.
Makundi hayo yaliyopatikana ni kama yanavyodokezwa hapa chini:-

Kundi La Kwanza Linaitwa Wapataji; hili hujumuisha wale watu ambao wanaamini kwamba walizaliwa waje wafanikiwe, waishi maisha mazuri yaliyojaa furaha amani na matumaini. 
Watu hawa kwa kawaida huwa hawana hofu wala wasiwasi bali wanatambua ukuu na nguvu zilizopo ndani mwao.
Kitu kingine kuhusu watu hawa ni kwamba hujiona wao ni wakuu na wapo duniani kuishi maisha yenye ukamilifu yaliyojaa furaha, amani na mafanikio!

Kundi La Pili Linaitwa Wapotezaji; hili hujumuisha wale watu ambao hujiona wao walizaliwa waje wateseke, hivyo kwao wao huona hawawezi wakaishi maisha mazuri yenye furaha, amani na mafanikio.
Kitu kingine kuhusu watu hawa ni kwamba wana hofu, wasiwasi na hawana tumaini lolote kuhusu maisha yao ya sasa hata ya baadaye.

Watu hawa hujikuta katika kuishi kwao hujikuta hali ya sintofahamu, na hii ni kwa sababu wamejiona katika uhaba na mateso hivyo hujikuta wakiduwaa hasa linapokuja suala la kuamua  juu ya kipi wafanye!

Kutokana na hilo hujikuta wakiyapa maisha ruhusa ya kuwafanya yanachotaka kuwafanya, nayo huwafanya kweli kwa maana maisha ni mwalimu wa yote…

Mpenzi, unatakiwa kujua kwamba hakuna mwanadamu ambaye huvuka kiwango kikubwa zaidi ya kile alichoishia kujiona.

Mithali 23:7 Neno la Mungu linasema; “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”
Unachopaswa kujua ni kwamba, vile unavyoona ndani ya nafsi yako ndivyo unavyokuwa nje ya nafsi yako!
Na hauwezi ukaenda Mbali zaidi ya pale ulipoishia kujiona!
Badili mitizamo yako Badilli maisha yako! 
Kwani ukibadili mitizamo yako, ndivyo na mambo hayo yatakavyobadilika vile unavyoyaona!

Na huu ndiyo mwisho wa sehemu ya kwanza ya somo hili!

Je ni sababu zipi ambazo huwafanya watu wajione vile wanavyojiona?

Je nifanye nini ili nibadili jinsi ninavyojiona?
Usijalii haya yote utayafahamu kwenye mwendelezo ujao wa makala hii!

Ahsante sana kwa kuwa mwanafamilia wa masomo haya!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...