Je, Mshindi Wa Bahati Nasibu Akitangazwa Mshindi Ile Nayo Ni Bahati?


Makala iliyopita awali ilidokeza baadhi ya mitizamo ya watu wengi kuhusu Bahati. 
Hitimisho lake lilionesha kwamba watu wengi huishia kuona bahati kama tukio, na siyo kuona bahati kama mchakato wa kupelekea tukio la kufurahisha!

Unachotakiwa kujua ni kwamba, kiuhalisia bahati kama bahati haipo bali mchakato wa kutengeneza bahati ije itokee ndiyo upo na huo mchakato ndiyo bahati yenyewe sasa! 

Kwa leo naenda kujibu swali litakalokupa uelewa kuhusu maana halisi ya bahati. 

Je Mshindi Wa Bahati Nasibu Akitangazwa kuwa Mshindi huwa anakuwa amepata bahati?
...Imenibidi nitumie mfano usio rasmi ili kukuelewesha zaidi kuhusu maana ya halisi ya bahati!

N.B usiende kufanya kile ninachoenda kukidokeza kwenye mfano huu… 
Bali tumia kama muongozo kwenye eneo unalotaka bahati ikukute! 

Bila shaka umeshasikia kuhusu washindi wa bahati nasibu, na huenda hata wewe mwenyewe mwenyewe umejaribu mara kadhaa kushiriki kwenye michezo hiyo!
Sijui kama ushawahi kushinda au laah!  Lakini leo tungalie nini huja akilini mwa watu wengi pale mshindi wa bahati nasibu akitangazwa...

Endapo mshindi wa bahati nasibu akitangazwa kashinda mamilioni ya fedha, watu wengi hupatwa na hali ya tamaa na kutamani kwanini wasingekuwa wao...

Na katika kufanya majadiliano ya hapa na pale, wengi wao huishia kuona kwamba kuna watu hapa duniani wana bahati kubwa sana... 

Ukiendelea kufuatilia mazungumzo yao kwa kina utasikia wakisema, huwezi kuamini jamaaa yetu kalala jana maskini leo kaamka tajiri, yaani natamani bahati kama yake ingenikuta na mimi ningefurahi sana...

Hata wewe huenda ukisikia mshindi wa bahati nasibu akitangazwa, huwa unaishia kuona kama amepata bahati kubwa sana kuwahi kutokea hapa duniani.

Usijue kilichopo nyuma ya pazia, kwa sababu akili yako imesetiwa ione bahati kama tukio, na, ukafunga ubongo ushindwe kudadisi ni kipi amefanya mpaka akaifikia bahati yake...

Makala hii itakudokezea mambo kadhaa unayotakiwa kujifunza kutoka kwa mshindi wa bahati nasibu, ili kesho na keshokutwa ukisikia mtu kashinda bahati nasibu usiishie kuwaza kuwa ana bahati sana… 

Ukweli ni kwamba mpaka mshindi wa bahati nasibu anaifikia bahati yake, nyuma ya pazia huwa kuna mambo yafuatayo aliyoyafanya...

Kwanza, aliamini kwamba ipo siku atapata bahati kupitia michezo hiyo ya bahati nasibu. 
Unatakiwa kujua kwamba hatua ya kwanza ya wewe kufanikiwa katika jambo lolote la ile ni kuweka Imani katika jambo hilo! 
Hivyo basi, hata yeye alianza kwa kuamini kwanza na ndiyo maana akabahatika. 
Wengi huwa wanapambana lakini hawajeweka imani yoyote ile kwenye mapambano yao, ndiyo maaana wanashindwa kuvuta bahati ije maishani mwao!

Pili, alishiriki katika kucheza kila mchezo wa bahati nasibu pasipo kukata tamaa. 
Unachotakiwa kujifunza hapa ni ni hiki; mshindi huyo alijua fika kabisa kwamba, ili aweze kufanikiwa ni lazima awe na tabia ya kufanya jambo lilelile kwa mwendelezo! 

Hali ambayo ilimsaidia katika kupata uzoefu na namna ya kufanya jambo hilo kwa usahihi. 
Mwisho wa siku akachukua akaweka… mambo yakaitika! Tayari kashaibuka mshindi hahahah…! 

Tatu, alikuwa tayari kulipa gharama.  Na, alifahamu fika kabisa kwamba ili aweze kubahatika katika eneo Fulani ni lazima ajue gharama zitakazohitajika katika eneo hilo.
Na, hakuishia tu kujua gharama bali alikuwa tayari kulipa gharama ili aivute bahati kwake. 

Nne, hakukata tamaa. Kukata tamaa siyo njia ya kufanikisha bahati, huenda aliliwa kwenye michezo hiyo kwa mfululizo wa miaka mitano hata kumi lakini hakuwahi kukata tamaa!

Mwisho anakuja kushinda, watu mnaanza kusema jamaa ana bahati kweli usijue kilichomo nyuma ya pazia!

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba bahati siyo lile tukio jema unalolipata, bali kile unachokifanya ili upate tukio hilo ndiyo bahati yenyewe, kwani pasipo kufanya hicho hata tukio hilo la kufurahisha (bahati) huwezi kuipata!

Kwa mantiki hiyo kabla hujaanza kutamani bahati ya mtu Fulani jaribu kuvaa viatu vyake kwanza, kwamba ungekuwa wewe ungeweza kufanya kile alichofanya mpaka akabahatika au viatu vyake visingekutosha?

Mpaka hapa najaribu kukuonesha asili ya bahati ilipo, kwamba bahati haiji kama tukio bali inakuja kwa sababu kuna mchakato Fulani ambao umeshauandaa utakaoivuta hiyo bahati katika maisha yako.

Unatakiwa kujua kwamba hata kama utakuwa ni mtu mwenye bahati kiasi gani huwezi ukaokota nyumba, kwani nyumba hujengwa, vivyo hivyo unatakiwa na wewe uanze kujijenga kwanza ndipo uweze kuivuta bahati Yako! 

Kadhalika hata kama utakuwa na bahati kiasi gani huwezi ukaokota mamilioni ya fedha yamemwagwa sehemu, kwani kila mtu huwa anaidhibiti pesa isipotee!
Jaribu kuangalia wewe mwenyewe unavyoidhibiti pesa yako isipotee utafikiri hiyo ndiyo roho yako...
Afu kichwani una mawazo ya kupata bahati ya kuokota pesa ili ufanikiwe, basi dondosha za kwako nami niziokote hahahaha…! 

Mpenzi unatakiwa kujua kwamba huwezi kupata kitu pasipo kufanya chochote kile, kwa minajiri hiyo badala ya kusubiri bahati ya kuokota pesa au kupata fedha jitengeneze kuwa kama sumaku ya kuvuta pesa.

Unakuwaje sumaku ya kuvuta pesa? ...Ni rahisi sana jitengeneze kuwa mtu wa thamani kwani pesa ni mbadilishano wa thamani!
Na asili ya fedha hufuata maeneo yenye thamani!

Vilevile hata kama ungekuwa ni mtu mwenye bahati kiasi gani huwezi kubahatika katika jambo lolote lile pasipo kufanya chochote kile! 
Kwa mfano huwezi kupata bahati ya kupata kazi kama hutafanya maombi ya kuomba kazi hiyo!

Hata Mungu mwenyewe hawezi kukupa kitu ambacho hujamuomba japo anajua mahitaji yako hata kabla hujamuomba. Lakini ili akupe ni mpaka  pale sharti la kumuomba litimizwe. Nenda kasome mathayo 7:7

Ninachokifanya hapa najaribu kukuonesha kwamba bahati haiji kama pakeji ya tukio bali inakuja kama matokeo ya mchakato Fulani.

Kwa hiyo leo kabla hujaanza kujiwazia kuwa una mikosi, huna bahati, una laana, una mabalaa na vitu vingine, jaribu kujiuliza unafanya nini? 
Au upo zako umetulia tu unasubiri muujiza wa bahati ukutembelee! My friend utasubiri sana kwa kweli…

Hata Ibrahim mwenyewe hakubahatika tu kubarikiwa na Mungu bali, bahati ya Baraka zake zilikuja mara baada ya kuitii sauti ya Mungu! 
Na alitii kwa kutenda, Mungu alipomuamuru aondoke akaondoka. 
Maana yake Ibrahim alitenda jambo (kuondoka) lililopelekea bahati yake (kutimia kwa ahadi yake aliyoahidiwa). Kasome mwanzo 12:1

Vipi kama asingeonesha utii na kuamua kuondoka! Bila shaka mpaka leo hii angekuwa anasubiri hizo Baraka si eti…
Huenda hata wewe ukawa unasubiri siku ya bahati yako ifike huku ukiwa hufanyi chochote kile! 

Mpenzi nasisitiza tena, huwezi kupata kitu kizuri pasipo kufanya chochote kile! Aliye na masikio ya kusikilia na asikie!
Badala ya kukaa tu, fanya jambo Fulani litakalokusogeza kwenye bahati yako. 

Ahsante sana kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya!

Je Asili Ya Bahati Ni Nini?
Nifanye Nini Ili Niweze Kuvuta Bahati Maishani Mwangu?
Usijalii haya yote utajifunza kwenye mwendelezo wa somo hili!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com


Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...