Onyo Hata Usifikirie Kubahatika Mpaka Usome Kwanza Hii...
Hivi unafahamu kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watu wanasubiri bahati iwafike ndipo waweze kubadili maisha yao, pasipo kujua kuwa wanachosubiri ni upepo (usio kitu) na siyo bahati kama wao wanavyodhani?
Bahati ni neno dogo sana ambalo limewanasa watu wengi sana kwenye mtego, na wengi bado wanaendelea kunaswa kwenye mtego huo.
Na, hii ni kwa sababu katika maisha yao hakuna chochote kile cha maana wanachokifanya, zaidi ya kusubiri mungubahati awatembelee nao wapate kubadilisha maisha yao....
Hebu jaribu kufanya uchunguzi wa chinichini utagundua kuna kundi kubwa la watu ambalo limekaa tu, huku likiwa halijishughulishi na chochote kile.
Hata hivyo mbali na kutokujishughulisha, bado linaamini kwamba kuna siku ya bahati inakuja bado, ambayo itakuja kubadili mazima historia ya maisha yao...
Hali hiyo imewafanya watu wengi wajihesabie haki na kuona kubahatika ni haki yao, na hata wasipojishughulisha ni sawa tu kwa maana siku ya bahati yao haijaja bado!
Ukweli ni kwamba watu wengi hawajui bahati ni nini, na laiti wangejua bahati ni nini wasingekuwa wanapoteza muda wao kwa kukaa tu huku wakiwa wanasubiri upepo…
Lakini kwa vile wameshanaswa kwenye mtego tayari, wamejikuta wakiweka matumaini yao kwenye bahati na wanatarajia kuna siku bahati itabisha hodi milangoni mwao na kuwaambia; “mimi ndiye bahati uliyekuwa ukiningojea, nichukue nitumie”
Unachopaswa kujua ni kwamba, kutokuelewa maana kamili ya bahati kumewafanya watu wengi wawe na fikra mgando, kwani badala ya kuweka juhudi katika kupambana wao wameweka juhudi katika kusubiri siku za bahati zao.
Watu hawa wameshindwa hata kutambua kwamba, ili upate matokeo ambayo hujawahi kuyapata ni lazima ukubali kufanya kitu ambacho hukuwahi kukifanya.
Hii inamaanisha kwamba kama uko zako unasubiri bahati ilihali hakuna chochote kile unachokifanya, utaendelea kupata matokeo hayohayo ambayo umekuwa ukiyapata siku zote za maisha yako, na hii ni kwa sababu hakuna kitu cha tofauti unachokifanya ambacho kinaweza kubadili matokeo maishani mwako!
Cha kuchukua hapa ni kwamba, kuendelea kusubiri siku yako ya bahati ifike huku ukiwa hufanyi chochote kile, ni sawa na kutokula huku ukitegemea kushiba kitu ambacho hakiwezi kutokea!
Ngoja nikuulize swali la kizushi, ni muda mrefu nimekusikia ukijiambia; “ngoja siku yangu ya bahati ifike”, kwani hiyo siku ya bahati yako haifiki tu?
Ni mara ngapi umesema unasubiri siku yako ya bahati?
Mbona maisha yako, yako vilevile? Naona siku zinazidi kwenda mbele lakini maisha yako yapo vilevile, je, siku ya bahati yako itakuwa lini?
Au unataka kumaanisha kuwa bahati itakukuta uzeeni?
Friend, unatakiwa kujua kwamba hakuna kitu kinachoitwa bahati hasa linapokuja suala la kufanikiwa maishani mwako.
Kwanini nasema hivi, ninasema hivi kwa sababu hapa duniani hakuna mtu ambaye alizaliwa na bahati ya: gari, nyumba, pea tano za viatu, maisha mazuri, n.k
Bali sote tulikuja duniani tukiwa sawa, yaani, tulizaliwa tukiwa uchi, wajinga na hatujielewi huku tukiwa tegemezi kwa wazazi wetu.
Na, tunakuja kutofautiana kwenye hadhi kimaisha siyo kwa sababu ya bahati, bali ni kwa sababu ya machaguo tunayoyachagua.
Kwani ukishafanya machaguo Fulani, basi machaguo hayo yatakufanya uwe yule uliyemchagua.
Kwa mantiki hiyo kinachopelekea tofauti za maisha yetu siyo bahati bali ni machaguo tunayoyachagua.
Nilipokuwa nalichunguza hili nimekuja kugundua kwamba kuna makundi mawili ambayo hufanya machaguo mawili tofauti.
Na, utofauti wa machaguo hayo yanayofanywa ndiyo hupelekea tofauti za matokeo yanayopatikana…
Kundi la kwanza, ni lile linalochagua kusubiri siku za bahati zao zifike. Ikiwa kundi la pili ni lile linaloamua kutafuta vichocheo vitavyopelekea kutokea kwa bahati hizo…
Jaribu kuvuta picha kuhusu maisha yako, vipi kwenye hayo makundi mawili upo kundi gani?
Je na wewe ni miongoni mwa wale watu ambao wametulia tu huku wakingoja siku za bahati zao zifike?
Unatakiwa kujua kwamba, kutokana na utofauti wa machaguo hayo, ndiyo maana utakuta mwingine akienda mbali kimaisha huku mwingine akibaki palepale…
Mpenzi, kiuhalisia bahati kama bahati haipo, bali mchakato wa kutengeneza bahati ije itokee ndiyo upo, na huo mchakato ndiyo unatakiwa uitwe bahati, kwa maana ni kupitia mchakato huo ndipo bahati inapatikana...
Na, huwezi kupata bahati pasipo kuipitisha kwenye mchakato utakaopelekea kutokea kwa bahati hiyo!
Je bahati nini labda?
Asili ya bahati ni nini?
Nifanye nini ili niweze kuvuta maishani mwangu?
Usijalii yote haya utajifunza kwenye mwendelezo ujao wa makala hii!
Ahsante sana kwa kuwa mwanafamilia wa masomo haya!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment