Ukweli Unaopaswa Kuujua Kuhusu Bahati. sehemu ya pili

makala iliyopita ilidokeza hoja tatu kuhusu asili ya bahati.
Kama ulivyoahidiwa toka juzi kwamba kutakuwa na mwendelezo wake basi leo utafahamishwa hoja nyingine zaidi kuhusu asili ya bahati!
Fuatana nami, ukajionee mwenyewe!

4. Bahati Huwakuta Wale Wanaoiamini Kuwa Ipo.
Huwezi ukakivuta kitu ambacho hujakiamini kwamba kipo kwa ajili yako! 
Sasa utaivutaje bahati katika maisha yako ilihali umeamini kwamba wewe una mikosi, una laana na huna bahati?

Mpenzi unatakiwa kujua kwamba kile unachokiamini ndicho unachokivuta katika maisha yako! 
Hivyo basi endapo utakuwa unafanya juhudi zako, huku ukiamini kwamba katika juhudi zako kuna siku utabahatika, ama hakika utavuta bahati katika maisha yako kutokana na imani ilile uliyoiweka kwenye juhudi zako!

Unatakiwa kujua kwamba kuamini ni kupokea kuwa jambo Fulani ni kweli hata kama jambo hilo siyo kweli.
Lakini msisitizo upo kwenye kufanya juhudi, kwamba utakuwa ni upumbavu kuamini kuwa siku yako ya bahati inakuja ilihali hakuna chochote kile unachokifanya.

Hebu jaribu kuvuta picha hujishughulishi na chochote kile sasa hiyo bahati itatoka wapi? 
Yaani upande upepo halafu uvune dhahabu? 
Ni kitu ambacho hakiwezi kutokea na hakijawahi kutokea tokea dunia hii iumbwe!

Wahenga walisema utavuna ulichokipanda. Kwa mantiki hiyo juhudi zako utakazozipanda ndizo zitakazopima kiwango cha bahati utakayoitengeneza.

Unatakiwa kujua kwamba ukiamini katika jambo Fulani, Imani utakayoweka juu ya jambo hilo itakuwa ndiyo mbegu ya bahati yako.
Fanya juhudi, amini katika bahati nawe utaweza kuvuta bahati katika maisha yako!
Kumbuka bahati ipo kwa wale wanaoiamini kuwa ipo kwa ajili yao!

5. Bahati Inatengenezwa
Kila mtu ambaye unaona anafanya vizuri katika jambo Fulani jua kwamba kuna mazingira aliyoyatengeneza kwanza ambayo yamemfikisha hapo alipofikia.

Mungu mwenyewe kwanza aliziumba mbingu na nchi akaifanya dunia hii iwe sehemu yake ya kuwekea miguu na mbinguni iwe ndiyo sehemu ya makao yake…
Sasa kama Mungu mwenyewe alitengeneza mazingira ya makazi yake mimi na wewe ni nani hasa tusitengeneze mazingira ya bahati zetu?

Friend usimuone mtu anafanya vizuri katika eneo Fulani ukasema hapa duniani kuna watu wana bahati. Lahasha! 

Unatakiwa kujua kwamba kuna muda alikaa akatengeneza mazingira kwa ajili ya utokeaji wa bahati yake. 

Sikiliza rafiki yangu tena kwa umakini uliotukuka, mtu huyo kwanza alikaa chini, akajitathimini juu ya pale alipo, akapima ni wapi anataka kufika, akakatafuta njia ya kufika huko, akatafuta chombo cha usafiri kitakachomfikisha huko, akafanya juhudi pasipo kukata tamaa akajikuta mambo yamejipa kwa upande wake kama alivyopanga.

Halafu unatokea mtu unaanza kusema kwamba jamaa ana bahati sana, usijue ni mangapi kayafanya ili kutengeneza mazingira ya bahati yake.
Kila mtu unayemuona akiwa amefika mahali Fulani pazuri usiseme kwamba jamaa angu ana bahati, nenda kamuulize alifanya nini mpaka akafika pale alipofika, ndipo utajua kwamba kile ambacho huwa tunakiita bahati siyo bahati halisi.

Kumbuka na wewe ukifanya kama vile yeye alivyofanya utapata matokeo kama yake.
Leo kabla hujasema unangoja siku ya bahati yako ifike jaribu kujiuliza hili, ninatengeneza mazingira gani kwa ajili ya kuvuta hiyo bahati katika maisha yangu.

Usisubiri kitu ambacho huna uhakika nacho, badala yake kitengenezee mazingira ya kukivuta kitu hicho katika maisha yako. 
Kumbuka kile unachokifanya ndicho kitapima umbali utakaoenda kimaisha…
Daima tengeneza mazingira rafiki yatakayovuta bahati ije katika maisha yako.

Je nifanye nini ili niweze kuvuta bahati maishani mwangu?
Usijalii utajifunza hili kwenye makala zijazo!

Ahsante sana kuwa mwanafamilia wa masomo haya mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
 

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...