Ukweli Unaotakiwa Kuujua Kuhusu Bahati…
Mhubiri 9:11
“nikarudi nikaona chini ya jua, ya kwamba siyo wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala si wenye ustadi wapatao upendeleo lakini wakati na bahati huwakuta wote”
Kifungu cha ufunguzi kimedokeza kwa lugha ya uwazi kabisa kwamba bahati na wakati huwakuta wote haijalishi wewe ni nani!
Kwa minajiri hiyo ni sawa na kusema kwamba, ukifanya jambo sahihi kwa namna sahihi na kwa wakati sahihi huku wewe mwenyewe ukiwa ni mtu sahihi kuna uwezekano mkubwa sana wa wewe kuvuta bahati katika jambo hilo…
Ngoja nikudokezee ukweli unaopaswa kuujua kuhusu bahati!
1. Kila Mtu Ana Bahati…
Mpenzi msomaji una bahati kubwa sana kuzaliwa ukiwa hai na mpaka sasa unaishi! Kwani siyo kila kinachozaliwa kinaishi!
Unatakiwa kujua kwamba kuzaliwa ni kitu kingine na kuishi ni kitu kingine! Tumshukuru Mungu kwa bahati ya uhai aliyotujalia!
Una bahati sana kupata wazazi wako waliohakikisha unabaki salama na mpaka leo hii bado uko hai.
Kwani endapo wazazi wetu waliotulea, wasingejitoa kwa ajili yetu huenda mimi na wewe tusingekuwa hai.
Una bahati kubwa sana kuzaliwa kwenye jamii iliyo na amani, hakuna vita, hakuna machafuko wala hakuna ghasia. Je wewe huoni bahati kuishi kwenye jamii iliyozungukwa na amani pande zote…
Mpaka hapo kuna haja ya kujiona huna bahati? Ama hakika una bahati kubwa sana! Umebahatika sana hata saa hii unasoma Makala hii!
Mpenzi unapolaumu na kuona pengine labda huna bahati, una mikosi au kuna jambo Fulani haliko sawa, kumbuka kuna mtu yupo mgonjwa kitandani na hajiwezi kabisa, na kuna mwingine ndiyo anapoteza uhai!
Mimi na wewe ni nani hasa? Ama hakika tumebahatika sana kuwa hai mpaka saa hii!
Kuwa hai ni bahati kubwa sana, kwani huu ndiyo mwanzo wa kuvuta bahati nyingine, kwani huwezi kuvuta bahati huku ukiwa haupo hai!
Linda sana uhai wako kwa maana huo ndiyo mwanzo wa kukusaidia uweze kuvuta bahati zingine!
2. Bahati Hutokea Pale Maandalizi Yakikutana Na Fursa...
Awali nilidokeza kuwa bahati haiji kama tukio la kufurahisha, bali huja kutokana na mchakato unaoufanya ili uweze kupata tukio hilo!
Kutokana na hilo huna budi kujua kwamba yale maandalizi utakayokuwa unayofanya ndiyo yatakayopelekea bahati yako.
Na, kama utakuwa hujajiandaa huwezi ukapata fursa ya bahati yako.
Kuna wakati unapitia magumu siyo kwamba huna bahati bali tatizo hufanyi maandalizi juu ya namna gani unaweza ukavuta bahati maishani mwako, na kama hutengenezi mazingira ya bahati yako utaivutaje hiyo bahati maishani mwako?
Tufanye unatafuta kazi, toka umehitimu chuo hujawahi hata kujiendeleza kwenye taaluma yako kwa ajili ya kujiongezea hata thamani yako tu.
Sasa basi imetokea siku umeitwa kwenye usaili ili ukajaribu bahati yako, ukafanya uwasilishaji lakini kwa vile hukujiandaa bahati yako ikapita kushoto, ukashindwa kwenye usaili huo, mwishowe ukaanza kujisemea, huna bahati, una mikosi, una laana na maneno mengine usijue tatizo siyo bahati bali tatizo hujafanya maandilizi ya kutosha ili uweze kuivuta bahati hiyo maisha yako.
Kwa mfano kama nina kipaji cha kucheza mpira sitakiwi nijifungie tu ndani huku nikisema; “mimi ni mchezaji mkubwa sana” endapo nitafanya hivyo nitaua kipaji changu.
Ninachopaswa kufanya ni kuendelea kunoa kipaji changu kila siku, kwani kadiri ninavyozidi kunoa kipaji changu, ndivyo ninavyozidi kuwa bora na kadiri ninavyozidi kuwa bora ndivyo ninavyozidi kutangaza uwezo wangu.
Na, kadiri watu wanavyozidi kuona uwezo wa kipaji changu ndivyo ninavyotengeneza nafasi ya bahati yangu, kwani kuna siku mtu atakuja kunipendekeza kuwa nastahili kuwa mchezaji na hapo ndipo bahati yangu itatokea.
Friend kaa ukiwa umejiandaa, na kama una uwezo wa kufanya jambo Fulani kaa ukiwa umejiandaa, siku fursa ya bahati yako ikifika ndiyo utakayoweza kuivuta bahati hiyo katikati ya maisha yako…
Kumbuka usipojiandaa siku ya bahati yako ikifika utaomba ukafanye maandalizi na bahati haitakusubiri wewe ukajiandae bali itaenda kwa yule ambaye tayari ameshajiandaa.
Ndugu, kaa ukiwa umejiandaa kwani hujui siku wala saa ambayo bahati yako itakujia.
Kwa mantiki hiyo ni muhimu ukawa umejiandaa ili siku ya bahati ikifika bahati hiyo isikukimbie bali uiweke katikati ya maisha yako!
3. Bahati Huja Zaidi Ya Mara Moja
Ni dhana potofu kuamini kwamba bahati huja mara moja tu, kwani bahati huja hata zaidi ya mara mia kikubwa uwe umejiandaa basi.
Na, ikumbukwe bahati haitakuja kama tukio bali itakuja kama fursa.
Na, uzuri wa fursa inapokuja huwa haimfuati mtu mwenye bahati bali humfuata yule aliyejiaandaa kwa ajili ya fursa hiyo.
Kwa mantiki hiyo huna budi kujua kwamba kila palipo na watu pana kila aina ya fursa, na fursa hizo zipo kwenye matatizo wanayokumbana nayo.
Na, ifahamike kwamba, tatizo la mtu Fulani ni fursa ya kutengeneza bahati yako, hata hivyo ni vema ukaweka akilini mwako kwamba utaziona fursa hizo endapo utakuwa umejiandaa kwa ajili ya kuzikabili ili upate matokeo unayoyataka…
Kwa upande mwingine Mungu ndiyo mtengenezaji wa fursa zote unazozijua wewe, na nyingine ambazo ushawahi kuzipata maishani mwako. Unatakiwa kujua kwamba,Mungu ndiye alikutengenezea fursa hizo.
Asili ya Mungu wetu ni kwamba kabla hata hajakuumba alishakutengenezea fursa za bahati yako tayari, ila shida ni wewe mara baada ya kuzaliwa umeamua kutomsikiliza na kuamua kufuata njia zako pamoja na kutumainia akili zako.
Hata hivyo linapokuja suala la kubahatika kupitia fursa alizokuandalia Mungu huku nako unapaswa uwe umejiandaa tayari!
Kwamba ni lazima umjue Mungu ni nani, umuamini na uweze kutimiza matakwa yake pamoja na kuzishika amri zake na siyo kuzishika tu bali uenende kwa kadiri ya zinavyokuongoza…
Yes, ndiyo maana huwa tunaambiwa tukeshe tukiomba kwa maana hatujui siku wala saa…
Kinachomaanishwa hapo ni kwamba tuwe tumejiandaa kwani saa yoyote ile na muda wowote ule lolote lile linaweza likatokea!
Hata hivyo ni vema ukafahamu kwamba vile utakavyojitoa kwa ajili ya Mungu wako ndiyo utakavyoenda mbali kimaisha.
Kutokana na ukweli huo ni kosa mtu kukuaminisha kwamba bahati haiji mara mbili kwani yeye si Mungu wako na hajui Mungu alikutengenezea fursa ngapi za bahati yako hapa duniani.
Bahati huja zaidi ya mara moja fungua jicho lako la kuangalia fursa utaziona fursa kibao ambazo zinakutaka wewe ufanye jambo Fulani!
Ahsante sana Kuwa mwanafamilia wa masomo haya!
Mwendelezo Wa Somo Hili Litaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment