Je Unataka Kujua Mbinu Za Kuikabili Hofu? Hizi Hapa Usome Halafu Uzitumie...

 
Habari yako rafiki? Ni matumaini yangu u mzima wa afya!
Ahsante sana kwa uvumilivu wako na utulivu wako ambao umekuwa nao ukisubiri mwendelezo wa somo hili! 
Huu ni wakati muafaka wa kuendelea na somo letu linaloangazia kuhusu mbinu tisa za kuikabili hofu...
Awali nilidokeza mbinu mbili unazoweza kutumia kukabili hofu yoyote ile!
Ashukuriwe Mungu kwa neema zake nyingi, kwa maana unaenda kujifunza mbinu nyingine nne za kuikabili hofu kama ifuatavyo:-

3. Tafuta Maarifa Mapya Kila Leo…
Hosea 4:6
“watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umekataa maarifa, mimi nami nitakutakataa wewe…”

Friend kama hakuna kuduwaa pasipo sababu, basi hakuna hofu pasipo kuwepo kwa sababu inayopelekea hofu hiyo… 

Moja ya sababu ambayo huwafanya watu wengi wahofu ni kukosa maarifa pamoja na maandalizi ya kutosha hasahasa kwenye maeneo ambayo wanaenda kukabiliana nayo. 

Na, ifahamike kwamba endapo utakosa maarifa juu ya maeneo hayo kitakachofuatia hapo huwa ni anguko (kuangamia).
Kutokana na angamizo linaloweza kutokea endapo jambo hilo litafanywa, ndipo sasa utakuta mtu unaitengeneza hofu kuhusu jambo hilo!

Hivyo basi ili usiogope Tena unachopaswa kufanya  ni kutafuta maarifa muafaka pamoja na taarifa sahihi, kwani ni kupitia maarifa na taarifa sahihi ndipo utakapopata mbinu sahihi za kufanya jambo hilo, ambapo mwisho wa siku hofu ya kufanya jambo hilo itatoweka!

Na, ndiyo maana kuna usemi maarufu usemao “maarifa ni nguvu”, japo kwangu mimi huwa nasema kwamba maarifa yaliyotumika ndiyo nguvu kwani ukiwa na maarifa na ukashindwa kuyatumia maarifa hayo hayawezi kukupa nguvu… 

Unatakiwa kujua kwamba kadri unavyojua kuhusu eneo Fulani au jambo Fulani ndivyo na hofu ya kufanya jambo hilo inavyopungua, ikiwa kadri unavyokuwa hujui kuhusu eneo Fulani au jambo Fulani ndivyo na hofu juu ya kufanya jambo hilo inavyozidi kuongezeka...

Labda utakuwa unajiuliza nitajuaje sasa? …ndiyo upo sahihi utajua siku utakayoamua kutafuta maarifa, na uzuri ni kwamba dunia tuliyonayo sasa kila sehemu kuna wigo wa maarifa hivyo kutokujifunza ni kuamua tu! 

Ikumbukwe kuwa maarifa ni nguvu, hivyo ukikosa maarifa hutakuwa na nguvu ndiyo maana utajikuta ukihofu muda wote.

Ili kuishinda hofu inayotokana na kutokujua unatakiwa utafute kujua kwanza, na ukishajua hofu nayo itatoweka… 

Unatakiwa kujua kwamba ukiona kuna eneo unalihofia maana yake umepungukiwa maarifa juu ya eneo hilo, hivyo basi badala ya kuendelea kuhofu wewe tafuta maarifa sahihi,ambapo utapata nguvu kupitia maarifa hayo mwishowe hutahofia chochote kile...

Mithali 3:13 Neno la Bwana linasema:
“heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu”
Una heri wewe uonaye hekima na kupata ufahamu, kwa kuwa ufahamu utakupa ujasiri nawe hutaogopa tena...

4. Fanya Vitu Unavyohofia Kufanya… 
Friend siwezi kukufundisha kuendesha baiskeli bali utapaswa ujifunze kuendesha baiskeli wewe mwenyewe, na usipofanya hivyo hakuna atakayefanya hivyo kwa ajili yako…

Unatakiwa kujua kuna baadhi ya vitu vingine havihitaji nadharia ila vinahitaji vitendo kwani ni kupitia kufanya kwa vitendo ndivyo hutufanya tuwe wakamilifu katika utendaji… 

Mpenzi msomaji ni bora ukafahamu kwamba pasipo kufanya kwa vitendo huwezi ukaishinda hofu…
Kwa mfano kama ulikuwa na hofu ya kuzungumza mbele za watu anza kujizoesha kuzungumza kwenye vikao vya kifamilia, shiriki kwenye vikao vya vikoba, shiriki kwenye semina mbalimbali, jifunze kuanzisha mazungumzo na watu mbalimbali…
Tengeneza mazingira ya kuzoeana na watu wa hadhi zote, matajiri na maskini, wenye fahamu na wasio na fahamu hii itakusaidia uweze kujua hulka zao. 
Hivyo basi endapo itatokea siku umeulizwa ufanye jambo Fulani mbele zao utaweza kuishinda hofu yako kwa maana tayari unajua hulka zao ni zipi…

Vilevile kama huwa una hofu ya kuzungumza mbele za watu unaweza ukaamua kila siku kutafuta mada Fulani, halafu ukaenda eneo lililotulia. 
Baada ya hapo anza kufanya uwasilishaji wa mada hiyo ukiwa pekee yako lakini kifikra jifanye kama upo unazungumza mbele za watu… 

Unaweza ukaenda uwanjani, au unaweza ukafanyia ghorofani, ukafanyia chumbani mwako au popote pale ili mradi pakupendeze, halafu tumia muda huo kuzungumza mawili matatu kuhusu mada uliyoichagua! 

Friend hakikisha unaitengeneza akili yako ione upo mbele za watu na wanakusikiliza kwa umakini uliotukuka…
Fanya hivyo kwa muda mrefu utajikuta tayari hofu hiyo ishakutoka nawe utakuwa unazungumza mbele za watu pasipo kuhofu…

5. Badilisha Aina Ya Marafiki…
Mithali 13:20
“Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utapata hekima, bali rafiki wa wapumbavu ataumia”

Awali nilidokeza kwamba akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine kwa hiyo basi kama utakuwa umeamua kubaki na aina ileile ya marafiki ambao hawajakusaidia uweze kuishinda hofu ni ngumu sana kwako kuishinda hofu.

Na, ndiyo maana mwandishi wa kitabu cha mithali anataka tuenende na marafiki wenye hekima kwa maana kupitia wao tutapata hekima, na tutatumia hekima hizo katika kuishi kwetu hali ambayo itatupa ujasiri na kutufanya tuishinde hofu.

Kuna wakati mwingine kushinda hofu haihihitaji nguvu kubwa sana wewe chagua marafiki kadhaa wanaofanya vizuri katika eneo unalolihofia, jifunze kutoka kwao.
Baada ya kujifunza kutoka kwao anza kufanya kile wanachokifanya kwa namna ileile utajikuta ukipata matokeo kama yao (kutokuhofia chochote kile).

6. Amini Katika Uwezo Wako…
Wafilipi 4:13
“Nayaweza mambo yote katika yeye katika yeye anitiaye nguvu”
Hofu humpa mwandamu ukomo na kumfanya asikue zaidi ya vile alivyo pamoja na pale alipo kwa wakati huo. 

Na ndiyo maana mtu mwenye hofu, kiakili huwa anafahamu kabisa kuwa, inatakiwa aondoke kwenye hali aliyonayo lakini cha ajabu nafsi yake inamuambia my friend wewe ni kiwango hiki na huwezi ukavuka zaidi ya hapa…

Ushawahi kusikia kwamba roho hupingana na mwili? Basi hiki ndicho hutokea. 
Yaani hii ni vita ya ndani kwa ndani.
Kutokana na hilo mtu huyo hujikuta akibaki akiwa na hofu muda wote asijue afanye nini.
Ukweli ni kwamba ili uweze kushinda hofu ni lazima uweke Imani juu yako.

Ni lazima uaumini kwamba unaweza, unastahili, una uwezo wa kufanya mambo yatokee, ulizaliwa uje uwe mshindi na bado upo hai ukiwa unaelekea kwenye maisha yaliyojaa furaha, amani, matumaini na mafanikio…

Hata hivyo unatakiwa uongeze kiwango chako cha Imani kwa kujinenea mema muda wote...
Kwa mfano unaweza ukawa kila siku unajitamkia kwamba: “ninaweza’’, “mimi ni bora”, “nitakuja kuwa mtu mkubwa sana miaka mitano ijayo” n.k

Baada ya hapo weka tabasamu usoni mwako tembea kwa madaha na kwa maringo.

Kumbuka kile unachojitamkia ndicho kitakupa ujasiri na kuona kuna raha ya kuishi hapa duniani.
Endapo utajitamkia hivyo kwa muda mrefu utajikuta ukipata ujasiri nawe hutatishika na chochote kile tena…

Ahsante sana kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Kesho uteletewa Mbinu nyingine unazoweza kutumia kukabili hofu...

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...