Njia 4 Tahisi Za Kupanga Bajeti Yako Ili Ufanikiwe Kifedha...
Hivi unajua asilimia kubwa ya watu hawana utaratibu wa kupangilia matumizi ya fedha zao hali ambayo huwafanya washindwe kufanikiwa kifedha huku wakilia hali ngumu muda wote?
Huenda hata wewe umekuwa ni yule mtu ambaye unatengeneza fedha kila leo lakini huna matumizi yanayoeleweka hali ambayo inapelekea upotevu wa fedha zako!
Rafiki unatakiwa kujua kwamba, usipojua namna ya kupangilia matumizi ya fedha zako, basi fedha zako zitakupangia uzitumiaje!
Na ndiyo maana kuna watu wakishapata fedha, huwa wanapatwa na hali ya mchecheto (fedha zinawawasha), hali ambayo huwafanya washindwe kutawala matumizi mazuri ya fedha zao, matokeo yake hujikuta wakifanya manunuzi kwa shinikizo linalotokana na fedha walizozitengeneza na siyo vile wao wanavyotaka kutumia fedha zao!
Ubaya huja pale ambapo unakuta mtu uliingiza kipato kikubwa tu cha fedha, lakini mwisho wa siku unajiona hujabakiwa na kitu na ukijaribu kuwaza umefanyia nini cha maana hauna.
Matokeo yake unajikuta ukianza kupatwa na msongo wa mawazo hasa pale unapokuta kuna eneo linahitaji fedha, halafu fedha yote imeisha!
Ukweli mchungu ni kwamba, hakuna kitu ambacho huwa kinaumiza hasa pale ambapo unakuta mtu umepokea pato fulani lakini mwisho wa siku unakuja kukuta pesa yako yote imeisha na hakuna cha maana ulichoifanyia!
Bila shaka umechoshwa sana na hii hali ya kuishi kimazoea, kama jibu ni ndiyo basi niko hapa kukusogezea habari njema...
Katika makala hii fupi utaoneshwa jinsi ya kupangilia bajeti yako hatua kwa hatua lengo likiwa ni kufanikiwa kifedha!
Kabla hujaoneshwa hatua muhimu za kuzingatia ili uweze kutengeneza bajeti yako, ngoja tufafanue maana ya bajeti!
Kwa Tafsiri nyepesi, Bajeti ni makadirio ya matumizi ya pato fulani lijalo, kwa kipindi cha muda fulani. ( Muda huo unaweza kuwa: mwezi mmoja, miezi sita au mwaka mzima)
Kwa mfano kama unatambua kwamba mwezi ujao utaingiza 200,000/=.
Unachopaswa kujua hapo ni kwamba utatakiwa ukadirie ni kwa namna gani utakavyoenda kuigawanya fedha yako katika maeneo muhimu unayotaka zitumike!
Hii ni sawa na kusema, bajeti ni kifaa ambacho kitakusaidia ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwenye pato lako utakalolitengeneza!
Unatakiwa kujua kwamba pasipo bajeti fedha yako itapukutika kama mti upukutishavyo majani yake wakati wa kiangazi ukifika!
Ndugu unahitaji bajeti ili ufanikiwe kifedha na kama hautapanga bajeti yako hakuna atakayekupangia!
HATUA ZA KUTENGENEZA BAJETI
Unatakiwa kujua kwamba kupanga bajeti ni kitu kingine na kuiishi bajeti yako ni kitu kingine.
Mbali na hilo ili kutengeneza bajeti huna budi kuzingatia hatua zifuatazo:-
1. Jua Matumizi Yako...
Huwezi kufanikiwa kupanga bajeti ilihali haujui matumizi yako kwa wiki au kwa mwezi ni kiasi gani!
Kwa mantiki hiyo hatua ya awali kabisa ambayo unatakiwa uanze kabla hujapanga bajeti yako, ni kukusanya taarifa zote za matumizi ya fedha zako kwa mwezi uliopita!
Hii itakusaidia uweze kufanya makadirio sahihi juu ya namna ya kupangilia matumizi ya pato utakaloingiza mwezi unaofuatia ili usitoke nje ya pato lako.
NB: ni muhimu kuanza kuandika matumizi yako yote ya fedha, kuanzia saa hii ili uje utumie wakati wa kufanya makadirio ya pato utakaloingiza mwezi utakaofuatia!
2. Jua Kipato Chako...
Unatakiwa utambue kwanza kiwango cha kipato unachokitengeneza. Kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kupanga bajeti ili hali hujui Unaingiza kiasi gani cha fedha!
Kwa mfano kama kwa mwezi Unaingiza 200,000/=, pato hilo ndiyo utakuwa ukomo wako, hii ni sawa na kusema bajeti yako haitakiwi izidi pato lako!
Rafiki ni muhimu kupanga bajeti kulingana na Pato lako, endapo utazidisha utaingia kwenye madeni!
3. Tengeneza Bajeti Yako Sasa...
Unatakiwa utengeneze bajeti yako katika hatua hii kwa sababu umeshajua pato lako ni kiasi gani, pia umeshajua matumizi yako kwa mwezi ni kiasi.
Kwa mantiki hiyo data hizo zitakuwa kama kiongozi cha wewe kupanga bajeti kwa usahihi!
Angalizo: unaweza ukatumia kanuni ya 30/70 ili kupanga bajeti yako.
Mchanganuo wake ni kama ufuatao:-
70% ya pato lako: (Tumia kwenye matumizi yako ya kawaida).
10% ya pato lako: (Tumia kwenye kuweka akiba).
10% ya pato lako: (Tumia kwenye kufanya uwezekezaji).
10% ya pato: (Toa sadaka, zaka na fungu la Kumi sehemu sahihi, kwani siyo kila sehemu wanayoabudu wanamtangaza Mungu!).
Kumbuka ili kupata fedha ni lazima utoe kwanza!
Watoaji huwa hawapungukiwi!
Ndiyo maana wahenga walisema: "mkono utakaotoa ndiyo utakaopokea"
4. Rejea bajeti yako kila mwezi...
Maisha ambayo hayana thamani hayana maana! Ili uweze kufanikiwa katika utekelezaji wa bajeti yako ni muhimu kuwa na utaratibu wa kujipa tathimini!
Ni muhimu ukafanya tathimini kwa sababu usipofanya hivyo unaweza ukajikuta unacheza nje ya bajeti, matokeo yake ukajikuta unashindwa kufikia malengo yako!
Unatakiwa kuhakikisha matumizi yako ya kila mwezi kama yameendana na bajeti yako!
Na, endapo itatokea yapo nje ya bajeti utatakiwa urekebishe suala hilo mapema iwezekanavyo!
Kumbuka wahenga walisema: "usipoziba ufa utajenga ukuta"
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho.
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment