Onyo! Hata Usifikirie Kubadli Hali Yako Ya Kifedha Mpaka Usome Kwanza Hii...


Habari rafiki! Ni matumaini yangu u mzima wa afya! Kwa upande wangu namshukuru Mungu, niko mzima wa afya na ninaendelea vyema kabisa!

Karibu sana kwenye mwendelezo wa somo linaloangazia kuhusu elimu ya fedha! Kama unakumbuka makala iliyopita ilishia kudokeza tafsiri kuu mbili za fedha!

Makala hii ni mwendelezo wa makala iliyopita, kwa leo utaenda kuoneshwa sifa za fedha.
Je ni zipi sifa bainifu za fedha? Usijalii ndani ya muda unaenda kuoneshwa sifa za fedha kama zifuatazo:

1. 𝐅𝐞𝐝𝐡𝐚 I𝐧𝐚𝐨𝐧𝐠𝐨𝐳𝐰𝐚 N𝐚 𝐊𝐮𝐭𝐞𝐧𝐠𝐞𝐧𝐞𝐳𝐚 K𝐰𝐚 𝐊𝐚𝐧𝐮𝐧𝐢.
Kila eneo linalohusu maisha ya binadamu hutawaliwa na kanuni fulani mahususi, na ifahamike kwamba kanuni hizo ndizo hupima na kupelekea matokeo fulani katika eneo hilo!

Ukweli ni kwamba kanuni huwa hazidanganyi, lakini endapo itatokea ukafanya kinyume na matakwa ya kanuni hizo basi utaishia kupata matokeo mabaya.

Unatakiwa kujua kwamba kuna kanuni zaidi ya 20 za fedha. Hii ni sawa na kusema utafanikiwa kifedha kutegemeana na namna utakavyotumia kanuni hizi!  
Ngoja tuangalie baadhi ya kanuni hizo!

➡️Kanuni Ya Kujilipa Kwanza...
Kanuni ya Kujilipa Kwanza inasema, "kwa kila pato utakalolitengeneza hakikisha unajilipa kwanza sehemu ya kumi la pato hilo"

Hapa haijalishi una bili ya kulipa, unadaiwa kodi, unadaiwa ada, n.k, unatakiwa uanze kwa kujilipa wewe kwanza, baada ya hapo unaweza kufanya malipo mengine!
Kanuni hii inakutaka uhakikishe kuwa kipaumbele chako kinakuwa ni wewe kwanza!

Moja ya sababu kubwa ambayo huwafanya watu wengi washindwe kufanikiwa kifedha, ni pale unakuta mtu anajilipa mwishoni au kutokujilipa kabisa.
Endapo utajiipa mwishoni unaweza kushangaa hakuna kilichobaki kwenye pato lako au ukawa umebakiwa na kiasi kidogo cha fedha, hivyo hata kama ukajilipa ukawa ni sawa na kama hujafanya kitu! 

Friend unatakiwa kujilipa kwanza kwa sababu umeajiri nafsi yako, na unafanya kazi kwa ajili ya nafsi yako!

Hata hivyo huna budi kufahamu kwamba, mshahara wako hauwezi kukufanya ufanikiwe kifesha bali ni rasimali unayotakiwa kutumia ili ufanikiwe kifedha!
Unatakiwa kujua kwamba, mshahara wako wa leo ni mbegu inayotakiwa kupandwa kwa ajili ya kesho yako Kifedha.

Kwa hiyo basi katika pato lako lijalo, hakikisha unatenga sehemu ya kumi kama sehemu ya malipo kwa ajili yako. 
Mara baada ya kujilipa kwa muda fulani unatakiwa uwekeze fedha uliyojilipa kwenye mradi unaojua vizuri!

Endapo utawekeza kitakachotokea uwekezaji wako utakuzalia watoto (faida) na ukishawapata watoto wa pato lako utapaswa uwawekeze ili wakuzalie wajukuu, na ukishawapata wajukuu wa pato lako wawekeze tena ili wakuzalie vitukuu, na kuendelea! 

Hivyo ndivyo chain ya kutengeneza fedha ilivyo, inaanzaa kwa kujilipa kwanza, halafu mwisho wa siku unaishia kutengeneza kiasi kingi cha fedha!

➡️Kanuni Ya Utunzaji Na Ukusanyaji...
Kanuni ya utunzaji na ukusanyaji inasema, "Sio kwa kiwango gani cha fedha unaingiza ndicho kitakachopima mafanikio yako ya Kifedha bali kwa kiwango gani cha fedha unachoweza kutunza"

Hii ni sawa na kusema,  kanuni hii inatutaka mimi na wewe tujenge nidhamu ya utunzaji angalau asilimia 10 au 20 ya kipato chetu! 
Endapo utafanikiwa kujenga tabia ya kutunza sehemu ya kipato chako kwa muda fulani utajikuta una akiba ya kutosha!
Kwa mantiki hiyo, unaweza ukatumia akiba yako kama mtaji, ukawekeza kwenye mradi fulani ili utengeneze fedha nyingine!

➡️Kanuni Ya Parkinson's...
Kanuni ya parkson's inasema, "daima matumizi yako hukua ili kufikia pato lako"
Hii ni sawa na kusema watu wamekuwa na tamaduni ya kuongeza matumizi yao pindi vipato vyao vinapoongezeka.

Kwa minajiri hiyo kanuni hii inatutaka kubakiza matumizi yetu pale pale pindi vipato vinapoongezeka ili tupate fedha nyingi za kutunza pamoja na kufanya uwekezaji.
Rafiki endapo utatumia kanuni hii, unaweza kufanikiwa kifedha, haijalishi ni kiasi gani cha fedha unachoingiza kama sehemu ya pato lako! 

➡️ Kanuni Ya Mlimbikizo...
Kanuni ya mlimbikizo inasema, "fedha nyingi ni matokeo ya mlimbikizo wa fedha ndogo ndogo zilizokusanywa kwa mwendelezo ndani ya kipindi cha muda fulani "
Unatakiwa kujua kwamba msisitizo upo kwenye kukusanya fedha kidogo kidogo kwa mwendelezo (siyo kwa kugusia gusia au kudonoa donoa)

Kwa mfano, unaweza ukaamua kila siku kuweka shilingi elfu moja ya kitanzania 1000/= (buku tu). 
Endapo utafanya hivyo kwa mwendelezo, ndani ya mwaka mmoja utakuwa na 365,000/=

Mpenzi Unatakiwa kujua kwamba kanuni ya mlimbikizo itakuwa inafanya kazi kwa ajili yako, yaani kwa kadri unavyozidi kulimbikiza fedha zako kidogo kidogo ndivyo unavyozidi kukuza kiwango chako cha fedha!

Na ndiyo maana wahenga walisema "haba na haba hujaza kibaba" 
Hii ni sawa na kusema mambo madogo ndiyo hupelekea mambo makubwa! 

Kwa upande wangu huwa siamini kwamba hapa duniani kuna mambo madogo hasa nikiangalia mambo makubwa (matokeo makubwa) yanayotokana na ufanywaji wa mambo madogo!

 ➡️Kanuni Ya Mabadilishano...
Kanuni ya mabadilishano inasema, "fedha ni nyenzo ya mabadilishano ambapo watu hutumia fedha ili kubadilishana na vile vitu wanavyovithamini"

Kutokana na kanuni hii ili utengeneza fedha za kutosha unatakiwa ufanye kitu ambacho watu  watu watakuwa tayari kukilipia na hii ni kwa sababu wanakithamini.

Na, ili watu waweze kuthamini kitu unachokifanya huna budi uchague kufanya kitu ambacho siyo rahisi kila mtu kukifanya, au ufanye kitu ambacho wengine wanakimbia kukifanya au unaweza ukafanya kitu ambacho wengine wanafanya ila wewe ukafanya kwa namna ya utofauti!
Sambamba na hilo ifuatayo ni sifa ya pili ya fedha!

2. 𝐅𝐞𝐝𝐡𝐚 Ina U𝐫𝐚𝐡𝐢𝐬𝐢 Wa 𝐊𝐮𝐢𝐭𝐞𝐧𝐠𝐞𝐧𝐞𝐳𝐚 Il𝐚 𝐔𝐠𝐮𝐦𝐮 W𝐚 𝐊𝐮𝐝𝐡𝐢𝐛𝐢𝐭𝐢 I𝐬𝐢𝐩𝐨𝐭𝐞𝐞.
Ukweli ni kwamba watu wengi tunatengeneza fedha kwa tunachokijua na tunapoteza fedha kwa kile tusichokijua! 

Unatakiwa kujua kwamba, kitu kigumu katika Kufanikiwa kifedha siyo kutengeneza fedha bali ugumu upo kwenye kuidhibiti fedha isipotee.

Hata hivyo watu masikini hawajawa masikini kwa sababu hawatengenezi fedha, bali ni kwa sababu wameshindwa kuzidhibiti zisipotee kwa kuwa na matumizi yasio na ulazima.

Unatakiwa ujifunze ujuzi wa kuzidhibiti fedha zako zisipotee!
Endapo utakosa ujuzi huu, utakuwa unatengeneza fedha kila leo lakini, zitakuwa hazikai!

Ahsante sana Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa Somo hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp No 0744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com



Comments

  1. Asante sana mkuu umefichua Mambo ambayo ni ya uhakika Sana kuhusu fedha.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...