Fahamu Mbinu Kuu Moja Ambayo Hutatua Kila Tatizo...

Moja ya kosa kubwa ambalo watu wengi hufanya wakikumbana na shida, tatizo, maradhi, majanga au hali ya sintofahamu ni kulaumu!

Na, hapa ndipo utamkuta mtu akilaumu kuhusu tatizo lililotokea pamoja na kuwalaumu ndugu, marafiki, serikali na lawama nyingine ambazo huelekezwa kwenye kila kona!

Ukweli ni kwamba, lawama huwa haitatui shida/tatizo badala yake hulifanya liende katika hatua mbaya zaidi, kwani mtu ambaye anawalaumu wenzake, hujihesabia haki kwa kujiona yeye siyo chanzo na hajahusika kabisa kwa kilichotokea badala yake sasa huwaona  wengine ndiyo tatizo huku tatizo akiwa ni yeye mwenyewe!

Ndugu, unatakiwa kujua kwamba, hakuna kiwango cha lawama ambacho hubadili tatizo lililopo au shida iliyopo, bali unaweza kubadili mtizamo wako ulionao juu ya jambo hilo!

Sasa basi, badala ya kulaumu, unatakiwa ujipe tathimini ya kutosha juu kile ulichofanya mpaka hilo jambo hilo likatokea huku ukihusisha na kile ambacho Mungu kasema kuhusu jambo hilo kwenye neno lake!

Ukweli ni kwamba, kuna baadhi ya matatizo tunapitia, tukidhani hayajasababishwa na sisi wenyewe, lakini kiuhalisia sisi wenyewe ndiyo vyanzo vya yote hayo chini wa mwamvuli wa kutokujua! (Sikujua), lakini sheria humhukumu yeyote yule anayejikwaa haijalishi anajua au hajui, na hiki ndicho kinachotokea maishani mwetu!

Kutokujua ndiko kumefanya watu wengi tufanye kinyume na mapenzi ya Mungu, hali ambayo imetuletea majanga maishani mwetu

Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kwamba kukosekana kwa kwa uelewa juu ya masuala mbalimbali maishani mwetu, kumechangiwa na ujinga wa kutokujua Neno la Bwana linasemaje kuhusu masuala hayo! 

Kutokana na kukosekana kwa nuru basi giza limefunika fahamu zetu ndiyo maana matatizo hayakomi maishani mwetu…

Hivyo basi kuanzia leo hii kabla hujaendelea kulaumu kuhusu hali unayopitia unatakiwa ujiulize, Mungu kupitia Neno lake kasemaje kuhusu hali hiyo, na wewe wajibu wako ni upi kuhusu hali/jambo hilo! 

Na, endapo utapata ufahamu kuhusu hili utakuwa ushafahamu ukweli nawe utakuwa huru! 
Yohana 8:32 “Tena mtaifahamu kweli, na hiyo kweli itawaweka huru”

Kwa mfano kwa wale ambao tumechoshwa na masumbufu ya dunia hii, Neno la Bwana linatualika tumuendee yeye aliye muweza wa yote naye atatupumzisha na mizigo yetu! 
Mathayo 11:28 “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo name nitawapumzisha” 

(Ubaya ni kwamba wengi hawajui kabisa kwamba kuna andiko hili, hata hivyo kuna wengine wanajua lakini hawajui maana yake, ukiachiilia hilo kuna wengine wanajua lakini hawaliamini andiko hili kama kweli watapumzishwa au laah!!)

Hali hii imefanya watu wengi wawe watumwa wa matatizo na ndiyo maana watu wengi wanaendelea kutaabika, laiti wangejua ama hakika wasingeendelea kutaabika kabisa.

Hata hivyo ukienda kusoma kitabu cha kumbukumbu la torati 28 yote utagundua kwamba majanga mengi, shida, maradhi pamoja na adha mbalimbali zimesababishwa na sisi wenyewe kwa kutokuitii sheria ya Mungu! 

Hii ni sawa na kusema unakuta Mungu kwenye neno lake kaamuru tufanye hiki sisi tukafanya kinyume chake hali ambayo imepelekea laana maishani mwetu.

Usinielewe vibaya sina maana kwamba wewe ni mdhambi au mkosefu lahasha!

Ila ukweli ni kwamba ukiona umeandamwa na mabalaa pamoja na matatizo mbalimbali maana yake ulikosa kuelewa juu ya kile Mungu kasema, ukaamua kwenda gizani, na kwa vile anayakwenda gizani hajui kule aendako ukajikuta umepotea, na huenda leo hii unajiuliza kwanini imekuwa hivi, usijue kwamba umekosa kufanya kile ambacho Mungu kaamuru ukifanye kwenye Neno lake.

Kumbukumbu la torati 28:1-2, Neno la Mungu linasema;
“Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza na kufanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana atakapokutuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka zote zote hizi zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako”.

Kwa mujibu wa kifungu ni kwamba ukiitii sauti ya Bwana Mungu wako utapata Baraka, na endapo hutaitii sauti yake utapata laana, na ifahamike kwamba laana ndiyo huleta matukio hasi maishani!

Jiulize mwenyewe kama upo upande gani, kama unatii utakuwa unacheza kwenye upande wa baraka na kama hutii maana yake upo upande wa laana.

Vilevile katika kitabu cha Kumbukumbu la torati 30:19-20, Neno la Bwana linasema;
“Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, Baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai wewe na uzao wako. Kumpenda Bwana Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako..."

Mungu anakusihi uchague uzima, hata hivyo hauchagui uzima na baraka kama fungu, bali utachagua uzima na baraka pale utakapoamua kuitii sauti yake! Hili ni sharti, unatakiwa ulitii! 

Hivyo basi ili uweze kuepuka kupitia baadhi ya adha na shida unatakiwa ujifunze Neno la mwenyezi Mungu kwa nguvu zote, ukweli ni kwamba Neno la Mungu ni ngao itakayokukinga na kila balaa! 

Kwangu mimi nikiulizwa moja ya kitabu bora kuwahi kukisoma na kukipenda nitakuambia ni BIBLIA!
Hivyo basi ili uepukane na majanga, shida, maradhi pamoja na adha mbalimbali wewe tii tu sauti ya Mungu halafu Mungu atasimama upande wako!
Habari njema ni kwambaa Neno la Mungu ndiyo mbegu ya mafanikio katika kila eneo lihusulo maisha ya binadamu...

Ukiachilia mbali hilo, katika kuishi kwangu na watu nimebaini kwamba watu wengi wanajua wanachotaka lakini hawajui jinsi ya kukipata. 

Huenda hata wewe, ukawa unahangaika kutafuta namna ya kutatua tatizo unalokumbana nalo, labda unaumwa maradhi fulani, au unapitia hali ya sintofahamu kiasi kwamba hujui ufanye nini!

Na, huenda ushapoteza kabisa matumaini na huoni kama utapona tena, au umeona tatizo lako halitatatulika kabisa!

Ndugu, Muite Mungu naye atasikia kilio chako, elekeza macho yako kwa Bwana naye ataitoa miguu yako katika wavu…

Friend, unatakiwa kujua kwamba kuna baadhi ya changamoto zitakukoma mara baada ya kuamua kumtafuta Mungu na kumueleza changamoto zako!  

Na ndiyo maana Isaya 55:6, Neno la Bwana linasema: “mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni maana yu karibu”

Je ni mara ngapi umemtafuta Mungu ukamueleza changamoto yako, ni mara ngapi umelia na Mungu juu ya tatizo lako? 
Ndugu unatakiwa kujua kwamba katika kila pito unalopitia ukimtafuta Mungu, utampata na ukimuomba katika roho na kweli atafanya jambo juu ya kile ukiombacho. 

Hata hivyo ukienda kusoma katika, Yeremia 33:3 Neno la Mungu linasema;
“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua”

Cha kuchukua hapa ni kwamba kwa kila pito, changamoto, adha, ugumu, shida na tatizo lolote lile, unatakiwa umuite Mungu naye atakuitikia. Na ifahamike kwamba Mungu hataishia kukuitikia tu bali atatenda makuu juu ya jambo hilo. 

Sambamba na hilo huenda unapitia hali ya sintofahamu mpaka hujui uelekee wapi. Kwamba umebaki umeduwaa kwani akili zako zimefika mwisho kabisa. Ndugu mrudie Mungu wako kwani mawazo yake, akili zake pamoja na njia zake siyo sawa na zetu… 

Isaya 55:8 Neno la Mungu linasema: 
“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema Bwana” 

Njia ya Bwana ni ya kweli na ndiyo itakupeleka uzimani.
 Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba, yeye ni Mungu wa yawezekanayo na siyo Mungu wa yasiyowezekana, hii inamaanisha kwamba hakuna jambo litakalomshinda Mungu haijalishi ukubwa wa jambo hilo.
Hivyo basi ili uweze kutatua shida zako kirahisi, lijue neno la Mungu, pamoja na kumtafuta Mungu!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com 

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...