Fahamu Sababu Kuu Moja Kwanini Sala Na Maombi Huwa Hayajibiwi Kama Ulivyotarajia...

Hivi unafahamu kuwa dhambi ndicho chanzo kikuu cha maombi mengi kutokujibiwa kama yalivyotarajiwa na muombaji?

Ukweli ni kwamba hakuna kitu kingine ambacho huua mawasiliano baina ya mtu na Mungu zaidi ya kuliko, unatakiwa kujua kwamba dhambi huua kabisa ule muunganiko uliopo kati ya Mungu na mwanadamu, na endapo uhusiano baina ya pande hizo mbili utakuwa haupo inamaanisha kwamba pande hizi mbili haziwezi kusikilizana.

Kutokana na ukweli huo huna budi kuweka akilini mwako kuwa, hata kama utaomba kwa namna gani kama mawasiliano kati yenu yametenganishwa na dhambi Mungu hawezi kukusikiliza kabisa!.

Nini ufanye? Unachopaswa kufanya ni kuacha dhambi na kuanza kuuishi usafi wa roho. Na ndiyo maana katika kitabu cha Ayubu 22:23 Neno la Bwana linasema;

“Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa upya; ukiuondoa udhalimu ndani ya hema yako”.

Rafiki unatakiwa kujua kuwa, haumrudii Mungu kwa kutamka tu kwa mdomo wako, bali unamrudia mungu kwa kuondoa udhalimu (kuacha dhambi), ukishaacha dhambi tu utakuwa ni msafi na kwa sababu Mungu ni mtakatifu anayeishi patakatifu patakatifu atabisha hodi na kuja kufanya makao ndani yako!

Na, endapo Mwenyezi Mungu atafanya makao ndani yako wewe utakuwa ngome na mwamba ulio imara. Ukiendelea kusoma sura hii katika ule mstari wa 27-30 Neno la Bwana linasema; 

“Utamwomba yeye atakusikia, nawe utazitimiliza nadhiri zako.
Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako, na mwanga utaziangaza njia zako, Hapo watakapokuangusha, utasema, kuna kuinuka tena; naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.
Atamwokoa na huyo asiye na hatia; naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako"

Mpenzi, Mungu anamtaka mtu msafi kwa maana wale wenye dhambi huwa hawasikii. Kwa mantiki hiyo leo kabla hujaomba tafakari katika kuishi kwako kama unauishi usafi wa moyo au unafanya yaliyo kinyume na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. 

Unachopaswa kujua ni kwamba, ili uweze kujibiwa maombi yako unatakiwa uweze kuchukia kabisa dhambi.

Hata hivyo Mungu mwenyewe anachukizwa kabisa na sala za mtu mwovu. Ukitaka kuthibitisha hili angalia vifungu vifuatavyo:- 

Mithali 28:9 “Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, hata sala yake ni chukizo”

Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mwovu ni chukizo kwa Bwana, bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake”

Mithali 15:29 “Bwana yu mbali na wasio haki, bali huisikia sala ya mwenye haki”

Huenda huwa unatoa mpaka sadaka kuhusu maombi yako, usijue kuwa kutokana na uovu wako unamchukiza Mungu wako. Hivyo basi kuanzia leo hii kabla hujaanza kuomba fanya toba kwanza. 

Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”

Hakuna kitu ambacho humtenga mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu zaidi ya dhambi…

Ukirudi katika kitabu cha Mwanzo ile sura ya 3 utaona jinsi Adamu alivyokuwa anaongea na Mungu ana kwa ana, na Mungu alikuwa anawatembelea, lakini sote tunatambua kilichotokea mara baada ya Adamu kuasi.

Kwamba Adamu alikutana na hali ya sintofahamu kwa kujikuta anatakiwa aache maisha yaliyokuwa yamejaa furaha, utele, afya njema na raha zote alizozipata akiwa pale edeni kabla hajaasi!

Na, ikumbukwe chochote kile ambacho Adamu alikitaka alikipata, lakini mara baada ya kutenda dhambi alipoteza uzima wa milele (hapa ndipo magonjwa yalianza, taabu, mateso, mahangaiko, maradhi, dhiki, shida, pamoja na kifo)

Mwanzo 3:16; Akamwambia Adamu, “kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambayo nalikuagiza, nikisema, ‘usiyale’ ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi”

Unachopaswa kujua ni kwamba, kutokana na dhambi ndiyo ukawa mwanzo wa mateso kwa binadamu!

Sasa basi, kuna wakati mwanadamu unaweza ukawa unaomba lakini Mungu akawa hakusikii na siyo kwamba hatakiwi kukusikia ila hakusikii kwa sababu wewe u mdhambi, kuna sehemu katika mapito yako haipo sawa!

Nini ufanye, unatakiwa uungame dhambi zako ili upate rehema mbele za Mungu wetu aliye hai. Na endapo utatubu dhambi zako na kuziacha kabisa utapata rehema naye Mungu atakuja kufanya makazi ndani yako.

Nawe utahesabiwa kuwa ni mwenye haki machoni pake, ndipo sasa Bwana atakapounganika na wewe na kuanza kukuongoza.

Unachopaswa kujua ni kwamba ukiziacha dhambi zako utafanyika kuwa ni mwenye haki, na ukishakuwa mwenye haki kuna habari njema inapatikana katika 1 Petro 3:12, habari yenyewe ni hii hapa; 

“Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake husikiliza maombi yao…”

Habari njema haiishii hapo tu, unatakiwa kujua kwamba ukishafanyika kuwa mwenye haki utastawi sana. 

Na hili limejidhihirisha katika Zaburi 92:12-13, Neno la Bwana linasema; 
“Mwenye haki atastawi kama mtende, atakuwa kama mwerezi wa lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana watastawi katika nyua za Mungu wetu”

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba tunaposema mwenye haki maana yake ni yule mtu ambaye anajua Neno la Mungu na analiishi! 
Habari njema ni kwamba, mtu huyo atastawi katika kila eneo la maisha yake yaani kuanzia afya yake itakuwa njema…

Na, mwanadamu utauishi ukamilifu pale utakapozishika na kuzitenda amri  za Mungu, ukizishika amri vizuri utaishinda dhambi, ukiishinda dhambi utakuwa mkamilifu, ukishakuwa mkamilifu utahesabiwa kuwa ni mwenye haki, ukishakuwa ni mwenye haki lolote utakoloomba mwenyezi Mungu atakusikia naye atakutimizia mahitaji yako.

Kuna wakati mwingine hauhitaji kukesha na kuomba sana bali shika amri za mwenyezi Mungu. Kumbuka ukishika amri za Mungu utafanyika kuwa kamanda.

Hata shida, taabu, mateso, maumivu vyote vitakuacha nawe hautakuwa wewe tena, bali utakuwa wewe mwingine. Kwani utapewa moyo mpya, roho mpya pamoja na afya mpya.

Mpendwa jaribu kuchunguza mapito yako kama yako sawa, kumbuka maombi ya mwenye dhambi ni kelele mbele za mwenyezi Mungu…

Unaweza ukadhani unaomba kumbe Mungu anakuona unampigia kelele tu, na huenda huyo Mungu hata hayupo katikati yako!

Rekebisha moyo wako kwanza kwa kutubu ndipo sasa Mungu atakapokusikia!

Ndimi Mwl Emmanuel Samuel King'ung'e!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...