Furaha Huweza Kuponya Yote, Furahi Kwa Sababu Yote Ni Mapenzi ya Mungu...

Hivi unafahamu kuwa huzuni imeweza kuwamaliza watu wengi kwa kuwakosesha raha pamoja kuuondoa kabisa ule umuhimu wa maisha yao hapa duniani?

Huenda hata wewe ukawa ni yule mtu ambaye kwa muda mrefu umekuwa ukihuzunika na ushapoteza kabisa tumaini la kuishi tena!

Ukweli ni kwamba furaha ndilo lengo kuu la kila binadamu, na hii ni kwa sababu kila mtu hufanya jambo fulani ili kutimiza furaha yake. 

Kwa mantiki hiyo huzuni siyo jambo la kulivumilia kwa kuwa hakuna mtu mmoja ambaye hufanya jambo fulani ili apate huzuni, bali wote hufanya mambo mengi ili kutimiza furaha zao!

Hii ni sawa na kusema ili uweze kuwa na maisha yenye amani ni lazima uikatae huzuni kwa nguvu zote na uitafute furaha kwa juhudi zako zote!

Na ndiyo maana, Zaburi 37:4-5 Neno la Mungu linasema; 
“Nawe utajifurahisha kwa Bwana, naye atakupa haja za moyo wako,
Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini naye atafanya”

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba kuna baadhi ya mambo ili Mungu apate kukutendea hata huhitaji kufunga bali unatakiwa tu ujifurahishe kwa Bwana Mungu wako.

Unatakiwa kujua kwamba Mungu ameketi kwenye sifa, hivyo basi ukiimba, ukamsifu kwa furaha ya iliyo ya kweli (itokayo motoni) Mungu atakupa haja za moyo wako.

Ukweli ni kwamba Mungu hana cha kufanya juu ya watu wenye huzuni, wenye kuogopa na wenye wasiwasi, kwa maana watu hawa hawawezi kumsifu Mungu pamoja na kumshangilia Mungu katika ile dhati ya kweli itokayo moyoni!

Zaburi 35:27 Neno la Bwana linasema; 
“Washangilie na kufurahi wapendezwao na haki yangu, naam waseme daima Atukuzwe Bwana, apendezwaye na amani ya mtumishi wake”

Unapokuwa na huzuni maana yake hupendezwi na haki ya Mungu, na kwamba Mungu hatakuwa na chochote cha kufanya kwako wewe uliye na huzuni. 

Hata hivyo kisaikolojia inaaminika kwamba mtu anapokuwa na huzuni sana, mwili wake huzalisha kemikali, na hizo kemikali huweza kuathiri afya yake pamoja na mfumo wa ufanyaji kazi wa ubongo!

Mpenzi unatakiwa kujua kwamba mtu ukiwa una furaha kuna kemikali ziitwazo endorphins ambazo huzalishwa, na endapo zitazalishwa zitakufanya muda wote uwe na amani na ukiwa na amani na furaha hata Mungu ataachilia Baraka zake zije katika maisha yako! 

Wafilipi 3:1, “Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika bwana”.

Wafilipi 4:4 “Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini”

1 wathesalonike 5:16-18 “Furahini siku zote, ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo; kwa maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika kristo yesu”

Ndugu hayo siyo maneno yangu, ni maneno ya Mungu aliye hai. Hebu furahi, hata lini utafurahi? 

Rafiki katika hiyo shida furahi tu kwani ni kwa mapenzi ya Mungu. Kuna uponyaji mkubwa sana kwenye kufurahi…

Aristotle alishawahi kusema furaha ni lengo kuu la kila binadamu, sasa kwanini uende kinyume na lengo la kila binadamu kwa kuchagua huzuni?

Furahi, furahi, tena furahi, mshangilie Mungu Muumba wa mbingu na nchi. Kuna wakati mwingine unatakiwa ujipe raha kwa kufurahi. 

Kwanza ukiwa ni mtu mwenye furaha hata shetani atakuogopa kwani atajua kwamba, hapa pana amani na pale palipo na amani ndipo Mungu alipo!

Nitoe wito kwako, katika kila jambo unalopitia jaribu kufurahi, yes wewe furahi tu ndugu!

Unatakiwa ufurahi hata kama kuna sababu milioni zinazokufanya uwe na huzuni!

Furahi tu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu, kwa maana hata kuwa hai ni kwa mapenzi yake!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com 



Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...