Hivi Ushawahi Kujiuliza Kwanini Huwa Unapata Kinyume Na Kile Ukiombacho?...

Mbali na kuwa watu wengi tumefundishwa kuamini juu ya kile tukiombacho, lakini wengi wetu tumeishia kupata kinyume cha kile tukiombacho. 

Laiti kama kila sala ingekuwa huwa inajibiwa kama vile muombaji anavyotaka basi hapa duniani kusingekuwa na shida, taabu, mateso, mahangaiko, maradhi, magonjwa n.k. Na kila mtu angekuwa anafurahia maisha yake.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba asilimia kubwa ya watu hupata kinyume na kile wakiombacho, huku sababu kubwa ikiwa ni kutokujua kanuni ya sala inayojibiwa ni ipi!

Makala hii fupi inaenda kudadavua suala hili kiundani, na nina uhakika endapo utasoma mpaka mwisho, utaweza kujifunza jambo kubwa sana ambalo hukuwahi kujifunza hapo awali...

Mathayo 18:19; 
“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni”.

Uelewa hafifu wa kifungu hicho, umeleta utata sana linapokuja suala la kuomba. 
Kwamba mtu anajikuta akiomba jambo Fulani lakini matokeo yake anapata kinyume cha jambo hilo...

Kitu cha kwanza unachopaswa kujua ni kwamba hao wawili siyo watu wawili tofauti bali ni mtu mmoja. 

Kinachomaanishwa hapo ni kwamba unapoomba huwa kuna vitu viwili yaani: kile unachokiomba (kwa mfano unaomba uponyaji) pamoja na ile picha unayoitengeneza juu ya hicho unachokiomba (your imagination).

“Mpenzi msomaji Yesu anatufundisha mimi na wewe kwamba, katika kuomba kwetu ni lazima kuwe kuna upatanifu kati ya kile tunachoomba pamoja na picha tunayoitengeneza juu ya hicho tukiombacho”

Hii ni sawa na kusema, kama kutakuwa na upatanifu basi wawili hao watafanyiwa jambo hilo waliombalo na Baba yetu aliye mbinguni. 

Na, kama ni uponyaji basi utaupokea uponyaji. Lakini kwa sharti moja tu wawili kati yenu ni lazima wapatane katika jambo hilo waliombalo.

Na, endapo wawili hao hawatapatana basi, Baba aliye mbinguni hatakuwa na chochote kile cha kufanya juu ya jambo hilo waliombalo.

Unachopaswa kujua ni kwamba endapo picha utakayoitengeneza juu ya jambo hilo uliombalo itakuwa kinyume na jambo hilo, basi hicho unachokiona ndicho utakachokipokea.

Kwa mfano tufanye unaomba upokee uponyaji lakini akilini unaona bado ukiwa katika hali ya kuumwa, upo hoi kitandani na kama ni maumivu bado unayaona hapo huwezi ukapokea uponyaji! 

Na, hii ni kwa sababu unachokiona akilini hakiendani na kile unachokiomba. Maana yake (wawili kati yenu hawajapatana katika jambo hilo)

Nini ufanye sasa? Unachopaswa kufanya ni kuilazimisha akilini yako ione mwisho mwema wa hicho ukiombacho. 
Kama ni unaomba upokee uponyaji juu ya ugonjwa jione ukiwa ni mzima, yaani umepona kabisa, na kama ulikuwa umelazwa jione tayari ukiwa unatembea na unaendelea vyema na shughuli zako. 

Hapo wawili watakuwa wamepatana, naye Baba yetu wa mbinguni atawafanyia jambo wawili hao.
Epuka kauli kama vile sijui nitafanikiwa katika jambo hili, sijui nitapata kweli kazi, sijui kama nitapata njia sahihi ya kufanya jambo langu n.k. 
 
Endapo utaruhusu mawazo hayo hutokuwa tofauti na mpanzi aliyepanda mbegu na kuzifukua mbegu zote huku akitegemea kwamba, mbegu hizo zitaota kitu ambacho hakiwezi kutokea kamwe. Mfano huu unatuonesha kwamba hutaweza kupokea uponyaji.

Hata hivyo ukirudi katika Mathayo 6:6 utaona kwamba Yesu anatufundisha tufanye nini wakati wa kusali.
Mathayo 6:6 Neno la Mungu linasema; 
“Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”

Chukua maneno, “ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini” halafu weka akilini mwako!

Bila shaka umefanya hivyo, nini maana yake? Unatakiwa kufunga akili yako ili isipitishe wazo baya juu ya kile ukiombacho! 

Kwa maneno mengine unatakiwa ufunge akili yako dhamiri (your conscious mind) isiingiliwe na mawazo hasi.

Unachopaswa kufanya ni kufunga kabisa akili yako isipitishe picha mbaya, kwa sababu ukipitisha picha mbaya juu ya jambo uliombalo tayari utaharibu, hapatakuwa na upatanifu baina ya wawili kati yenu, hivyo Mungu atakosa cha kuwafanyia.

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba sala huwa zinajibiwa kwa sababu akili yako inatawaliwa na kanuni ya kuamini.

Hata hivyo kanuni ya kuamini inasema kwamba “chochote utakachokiamini kuhusu wewe na dunia yako kitafanyika kwako kama uaminivyo”

Mpenzi msomaji unatakiwa uamini kwamba hicho ukiombacho umekipokea na kimeshakuwa chako tayari (yaani unakimiliki).

 Marko 11:24 Neno la Mungu linasema;
“Kwa sababu hiyo nawaambia: yoyote myoambayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu”

Kigezo tunachopewa hapa ni kusali kwa imani. Kwamba ulione tayari hilo jambo unaloliomba akilini unalo tayari. Kumbuka nawe utapokea kwa kadri ya uaminivyo.

Hata hivyo katika kitabu cha waebrania 11:1 Neno la Mungu linasema;
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”

Unachopaswa kuondoka nacho hapa ni “kuwa na hakika”, ndiyo, bosi kuwa na hakika kwamba jambo lako unaloliomba umeshalipata na ni lako tayari! 

Mbali na hilo unatakiwa kujua kwamba kuamini ni sawa na kupokea kuwa jambo Fulani ni kweli hata kama jambo hilo halipo hivyo, hii inamaanisha kwamba endapo utaendelea kuweka imani juu ya jambo hilo utakuja kulipokea kwa kadri ya ulivyoliamini.

Ndugu, natambua kwamba unapitia maumivu makali, unatakiwa kujua kwamba unapitia maumivu makali siyo kwa sababu unatakiwa upitie maumivu makali ila ni kwa sababu umetengeneza imani potofu juu ya pito lako. 

Badala ya kuamini katika kufanikiwa katika jambo hilo pamoja na ukuu wa wa Mungu wewe umeamini katika kuangalia ukubwa wa tatizo. Na kuona kwamba haliwezekani!

Mpenzi msomaji hata Yesu katika uponyaji alikuwa anaponya kwa kutumia imani aliyokuwa nayo yule anayehitaji kufanyiwa uponyaji. 

Mathayo 9:28-30
“Naye alipofika nyumbani wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, mnaamini kwamba naweza kufanya hili” wakamwambia naam Bwana, ndipo alipowagusa macho, akasema, kwa kadri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka.” Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, “angalieni hata mtu mmoja asijue”

Unachopaswa kujua ni kwamba Yesu hakuwaponya ila imani yao waliyokuwa nayo kwa Yesu ndiyo iliyowaponya kwa mujibu wa kifungu hicho.

Hata hivyo mstari wa mwisho tunaona Yesu akiweka msisitizo kwamba wahakikishe hata mtu mmoja asijue, hivi ushawahi kujiuliza kwanini aliwazuia wasijitangaze?

… usijali utaenda kuujua kweli, Yesu aliwazuia kwa sababu alijua wanaweza kuchangamana na watu wasioamini, kutokana na hilo wanaweza kuwabadilisha imani yao hali itakayowarudisha kwenye upofu.

Hitimisho: Ili usipate kinyume na kile uombacho hakikisha kunakuwa kuna upatanifu kati ya jambo unaloliomba na picha unayotengeneza akilini mwako.

Kama unaomba kuhusu uponyaji, jione ukiwa umepona tayari yaani ukiwa u mzima wa afya njema…

Ahsante sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho.

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329 au andika blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com 

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...