Kama Utaweza Kubadilisha Mfumo Wako Wa Kuamini Nitakuonesha Jinsi Ya Kumaliza Matatizo Sugu Kwa Kutumia Neno La Mungu...

Watu wengi wanajua wanachokitaka maishani mwao, lakini hawajui jinsi ya kukipata pamoja na kukivuta kitu hicho kije maishani mwao!

Ukweli ni kwamba watu wengi wamechoshwa na hali wanazopitia, lakini imani yao kuhusu hali hizo haijabadilika hali ambayo imepelekea matatizo hayo yaendelee kuwa sehemu ya maisha yao!

Makala hii fupi itaendelea kudadavua hili kwa undani, na nina uhakika endapo utasoma mpaka mwisho kuna kitu kitabadilika maishani mwako, nimekuombea kwa Mungu ili mapenzi yake yatimizwe katika maisha yako!

Rafiki kwa kila hali utakayokutana nayo hutakiwi kuangalia ukubwa wa tatizo lako (huo siyo wajibu wako), bali wajibu wako unatakiwa uwe kuangalia ukuu wa Mungu wako dhidi ya tatizo hilo. 
Kwa sababu kwake yeye kila jambo linawezekana. Naye ni Mungu wa yawezekanayo na siyo Mungu wa yasiyowezekana!

Kutokana na hilo ndiyo maana mwandishi wa kitabu cha Ayubu 22:21 anasema; 
“Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndivyo mema yatakavyokujia”

Kumbe kumjua Mungu ni chanzo cha mimi kupata mema. Hii inamaanisha kwamba hata: maradhi, magonjwa, maumivu, mateso na dhiki vitanipisha kwa maana nimemjua Mungu yeye aanzishaye safari njema.
Hivyo basi, endapo nitamjua Mungu, naye atabadilisha mabaya yote ninayokutana nayo na kuyafanya yawe mema kwa maana Mungu pekee ndiye aliye mwema… 

Marko 10:18
Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. 

Naona unajiuliza namjuaje Mungu sasa mimi? …Usijali muda siyo mrefu unaenda kupata jibu…

Utamjua Mungu kwa kuamini kwamba yupo pamoja na kujifunza Neno lake. 
Kwani Mungu ni Neno, hivyo ukilipokea Neno lake ni sawa na utakuwa umempokea yeye! 

Yohana 1:1, Neno la Bwana linasema:
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno,
Naye Neno alikuwako kwa Mungu,
Naye Neno alikuwa Mungu.

Kwa mujibu wa kifungu hiki unaoneshwa kwa uwazi kabisa kuwa Mungu ni Neno! Kwa mantiki hiyo endapo utalipokea Neno lake utakuwa ni sawa na umempokea Mungu mwenyewe matokeo yake nafsi yako itahuishwa upya! 

Habari njema ni kwamba Neno lake linaponya, linatakasa, linaokoa pamoja na kufanya miujiza mingi.

Hata hivyo, ili uwe muamini imara huna budi kulifanya Neno lake liwe kama kioo kwako. Hii ni sawa na kusema, huna budi ujitazamie humo na kuangalia kama unaenenda sawasawa na matakwa yake au laah!

Unatakiwa kujua kwamba kuna wakati unapitia baadhi ya maumivu, siyo kwa sababu unatakiwa upitie ila ni kwa sababu haujui agano ambalo Mungu kaweka dhidi yako wewe na maisha yako kwenye Neno lake! 

Kwa maneno mengine ni sawa na kusema, huna mwanga wowote kuhusu hilo. Na kama huna mwanga maana yake wewe upo gizani na si nuruni tena. 

Huenda ukawa unajiuliza kwamba huo mwanga ni mwanga wa jua au? Lahasha ni ile nuru iletwayo na Neno la Mungu. 

Yohana 1:4;
“Ndani yake ndimo ulikuwamo uzima, na ule uzima ulikuwa nuru ya watu” 

Je ndani yako kuna uzima? Je ule uzima uliopo kwenye Neno la Mungu upo ndani yako? Wakati wa kupokea uponyaji katika jambo lolote kupitia Neno la Mungu umekaribia sasa.

Na, ndiyo maana hata kuponya roho Mungu hutumia Neno lake, na hili limejitokeza katika Zaburi 107:19-20, ambapo Neno la Mungu linasema:
“Wakamlilia Bwana katika dhiki zao akawaponya na dhiki zao.
Hulituma neno neno lake, huwaponya, huwatoa katika maangamizo yao"

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba kulipokea Neno la Mungu ni kinga tosha kabisa na hakuna jambo litakalotishia amani yako! 

Na, ndiyo maana Yohana 15:7, Neno la Mungu linasema; 
“Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa”

Kumbe sharti la kujibiwa maombi ni lazima ujue Neno lake. Hata hivyo Mwenyezi Mungu hupendezwa na maombi yale ambayo muombaji anayeomba anajua Neno lake.

Unachopaswa kujua ni kwamba ili uweze kupokea nguvu za Mwenyezi Mungu ni lazima uamini kwamba Mungu yupo na anaweza.
Hatua ya kwanza wewe kuwa na afya njema ni kulipokea Neno la Mungu. Kwani ndani yake mna uzima…

Huenda unapitia hali ngumu, unasumbuliwa na maradhi, maumivu na mateso makali sana.
Unachopaswa kufanya kama hatua ya awali ni kulipokea Neno la Mungu na kutenda sawasawa na matakwa yake. 

Mpenzi, kumbuka ukilipokea neno lake utakuwa umempokea Mungu mwenyewe kwani Mungu ni Neno hai linaloishi! 
Ukishalipokea Neno lake litaenda kuponya roho yako kwanza. 

Na, ndiyo maana 3 Yohana 2, Neno la Bwana linasema;
“Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”

Unatakiwa kujua ili upone kimwili ni lazima uponye roho yako kwanza, unaponyaje roho yako? Ni kupitia kuilisha neno la Mungu! Kwani Neno la Mungu ndicho chakula cha kiroho wala hakuna kingine. 

Na ndiyo maana, Yohana 6:63, Neno la Bwana linasema: “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu, maneno hayo niliyowaambia ni roho tena ni uzima”

Mpenzi ili upone kimwili unatakiwa upone kiroho kwanza, je roho yako iko nzima? Unatakiwa kujua kwamba roho ndiyo itiayo uzima! Hii ni sawa na kusema endapo roho yako itakuwa imekufa na mwili nao utakufa kwani mwili hufuata roho!

Ndugu kama ni kuteseka, umeteseka vya kutosha, kama ni kuumia umeumia vya kutosha, kama ni ugonjwa umekutesa vya kutosha!

Leo Mungu anakukataka ubadili mfumo wako wa kuamini, kwa kuweka tumaini thabiti kwake pamoja na kuwa na kiu ya haki (njaa ya kujifunza na kutaka kulijua Neno lake).

Mpendwa ni muhimu ufahamu kwamba, Mungu atapita kwako siku ukilijua Neno lake. Na ukishalifahamu Neno utaifahamu kweli, na hiyo kweli itakuweka huru.

Ukweli ni kwamba kwake yeye hakuna: magonjwa, maradhi, dhiki, maumivu na mateso. Na huo ndiyo uhuru utakaoupata ukiwa kwake!

Awali nilisema kwamba ukiona mabalaa mengi yamekusonga maana yake upo upande wa laana, kwani matukio mabaya maishani huletwa na laana inayotokana na kutokutii sauti ya Mungu wetu!

Habari njema ni kwamba, Kristo alimaliza kazi pale msalabani kwani alifanyika laana kwa ajili yetu, ili  sisi tuokolewe dhidi ya laana inayotokana na dhambi!

Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti”

Ukweli ni kwamba, kwa mkristo unayeishi kwenye zama hizi, hutakiwi kuendelea kuteseka kwa magonjwa, dhiki, shida pamoja na maumivu ya hapa na pale kwa sababu hayo yote alikushindia Yesu Kristo alipotundikwa hadi kufa pale msalabani!

Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba laana zote zilizoandikwa kwenye Kumbukumbu la torati 28:15-68 ziliondolewa kutokana na kifo cha Kristo pale msalabani, kwani alikufa ili kuukomboa ulimwengu dhidi ya utumwa wa dhambi. Na laana hutokana na dhambi!

Kristo alilipa gharama zote ili wewe uishi maisha yaliyojaa furaha, amani, afya njema, mafanikio pamoja na matumaini kwa maana laana ya dhambi haipo tena.

Huenda ulikuwa hulijui hili, hata kama umekuwa ni mkristo kwa miaka kadhaa, na ndiyo maana mambo yamekuwa yakienda kinyume na matarajio yako. 

Maadamu umeshaujua ukweli unachopaswa kufanya saa hii ni kuweka imani katika Yesu Kristo, ukishafanya hivyo hutaishi kwenye laana tena bali utazungukwa na Baraka kila upande!

Unatakiwa kujua kwamba haki hupatikana kwa kuamini, ndiyo maana nimesema weka imani katika yesu kristo, ukishaweka imani kwake maisha yako yatabadilishwa na yule uliyemuamini!  

Wagalatia 3:6 “Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki, fahamuni basi wale walio wa imani, hao ndiyo wana wa Ibrahimu”

Mpenzi badili Imani Yako, usizitumaini tena akili zako, bali weka imani na tumaini kwa Mungu pamoja na mwanaye Kristo Yesu!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com  

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...