Usimtendee Mwenzako Yale Usiyependa Utendewe Na Wewe "The Golden Rule"...
Hivi unafahamu kwamba Moja ya sababu kubwa ya magumu ambayo wanadamu tunakutana nayo ni kwa sababu ya kukosekana kwa upendo baina yetu?
Ukweli ni kwamba, tungekuwa tunawatendea wenzetu yale ambayo tungependa sisi wenyewe tutendewe, basi kusingekuwa na chuki, hasira, vinyongo pamoja na visirani.
Lakini haya yote yametapakaa katika kizazi hiki cha leo, kwa sababu tunawatendea wenzetu yale ambayo sisi wenyewe hatupo tayari tutendewe, na endapo itatokea tumetendewa basi tunaanza kuchukia na kujenga hasira kali vifuani mwetu!
Mhubiri 7:9 Neno la Mungu linasema;
“Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, kwa maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu”
Rafiki unatakiwa kujua kwamba, hasira huwa haimletei madhara yule anayechukiwa bali humuumiza zaidi yule anayechukia.
Hii ni sawa na kusema, ukiwa na hasira maana yake una fikra hasi kichwani mwako, na hiyo fikra hasi ndiyo inakufanya uwachukie wenzako pamoja na kuwatendea yale ambayo wewe mwenyewe hupendi kutendewa!
Hebu jaribu kuvuta picha, hivi unavyonionea mimi hasira unafikiri kuna kitu kitanikuta kutokana na hasira yako uliyonayo juu yangu?
Katika hali ya kawaida mimi siwezi kuumia, bali hiyo hasira itakuumiza mwenyewe, na ndiyo maana mhubiri kasema kwa uwazi kabisa kwamba, “hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu”, hii ni sawa na kusema upumbavu wako wa kutokujua madhara ya hasira ndiyo unakutesa na kukuumiza.
Unachopaswa kujua ni kwamba, kutokana na hasira yako unakuwa unajiumiza mwenyewe kwa kujihukumu.
Hata hivyo ukienda kusoma Mathayo 5:22 Neno la Mungu linasema;
“Bali mimi nawaambieni: kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu”
Mpenzi unatakiwa kujua kwamba malipo ni hapahapa duniani, na hakuna anayekuhukumu bali unajihukumu mwenyewe kupitia hasira Yako.
Na, ndiyo maana unajikuta upo kwenye maumivu wakati wote kwa sababu hupendi mafanikio, furaha, amani, pamoja na raha ya watu wengine, na hiyo ndiyo hukumu yenyewe!
Unapoona hasira kwa sababu jirani yako yuko na afya njema maana yake ni sawa na unaikataa afya njema na unautaka ugonjwa, na kwa sababu ubongo wako una nguvu ya kuumba basi utaumba magonjwa, dhiki, shida pamoja na adha mbalimbali katika maisha yako!
Na, ifahamike kwamba unapomuonea hasira ndugu yako kwa sababu ya afya yake kuwa njema, au kuwa na maisha mazuri, unachokifanya ni sawa na unaikataa afya njema kwenye maisha yako pamoja na maisha mazuri.
Unatakiwa kujua kwamba kile unachokifikiri haijalishi ni juu yako au juu ya mwingine, basi kitapokelewa kama ombi kwenye subconscious mind nayo itachakata na kukuleteaa matokeo yanayolandana na kile kilichofikiriwa!
Kumbuka huwezi ukakivuta kitu ambacho unakilaani! Kwa maneno mengine ni sawa na kusema, unapochukia Fulani kuwa na hali nzuri maana yake ni sawa na unaikataa hali hiyo maishani mwako, jaribu kuwaza tu utawezaje kuivuta wakati unaailaani?
Na, ndiyo maana wahenga walipata kusema “chuki humchoma yule anayeihifadhi”
Rafiki unatakiwa kujua kwamba ubongo wako una nguvu ya kuumba!
Kwa mantiki hiyo kile unachokifikiri ni sawa na unakiumba, hivyo basi unavyomfikiria mwenzako mabaya na kumuonea wivu na chuki hiyo chuki unaitengeneza kwenye maisha yako matokeo yake utaanza kujichukia mwenyewe.
Kumbuka, kila kinachoingia ndani kupitia conscious mind hujidhihirisha nje kupitia subconscious mind…
Rafiki huna budi kuweka akilini mwako kuwa, kile unachokiwaza kwa kupitia conscious mind haijalishi unamuwazia nani, kitachukuliwa kama ombi linalotumwa kwenye subconscious mind, ambayo itakuletea matokeo yanayoendana na kile kilichowasilishwa.
Nini ufanye, ngoja tuangalie kile biblia inasema kuhusu kuwapenda ndugu zetu...
Mathayo 7:12 inasema;
“Basi yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii”
Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kile ambacho unapenda utendewe na mwenzako ndicho unachopaswa umtendee yeye.
Sasa unapomchukia mwenzako kwa sababu ana furaha, ana amani ana afya njema unataka kumaanisha kwamba na wewe unataka uchukiwe au?
Rafiki ukitaka uishi vizuri na watu punguza
chuki, punguza hasira, punguza wivu, kiache kila kitu kiende.
Halafu jitamkie napenda ningekuwa na mafanikio, furaha, afya njema na amani kama ya mtu Fulani.
Hapo utakuwa unavuta mafanikio, furaha, afya njema na amani katika maisha yako!
Kumbuka kile unachowaza na kukifikiri ndicho unachokivuta…
Mtakie Baraka za maisha kila mtu, wala usiwe na kinyongo na mtu, na kama mtu kakukosea msamehe kwani chuki humchoma yule anayeihifadhi.
Mpendwa Mungu ni upendo, tena apenda watu wake, na ndiyo maana alimtoa hata mwanaye wa pekee ili mimi na wewe tukombolewe, jaribu kufikiri juu ya pendo hilo la ajabu.
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe uzima wa milele”
Kwanini na wewe usiwapende majirani zako?
Ni wajibu wetu kuwapenda majirani zetu kwa kuwatendea yale ambayo tungependa tutendewe na sisi!
Na ndiyo maana ukienda kusoma, Mathayo 22:39 Neno la Mungu linasema;
“Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii: mpende jirani yako kama nafsi yako”
Chuki ya nini? Wivu wa nini? Hasira ya nini? Kinyongo cha nini?
Kwani hicho kinyongo unamuwekea nani? Unafikiri ni mimi? Hapana unajiwekea wewe mwenyewe!
Hebu jisamehe kwa kuanza kujipenda, ukishajipenda utawapenda wengine, ukishawapenda chuki, hasira na wivu itatoweka dhidi yao, ikishatoweka utawatakia wote Baraka za maisha…
Kumbuka kumtakia mwingine mema ni sawa na kujitakia mwenyewe mema.
Kwani kile unachokifikiri kuhusu mwingine akili yako itapokea kama ombi na kuanza kulichakata hadi upate matokeo.
Hakuna haja ya kumchukia mtu, we mpende, ukimpenda utavuta mafanikio maishani mwako!
Ni matumaini yangu Makala hii imekusaidia na imekufanyia uponyaji, ubaki na amani ya Bwana.
Nakutakia Baraka zote za maisha…
Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e; . Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment