Jinsi Ya Kupanga Na Kufanikisha Malengo Yako…
Kitu unachopaswa kujua ni kwamba kuazimia malengo ni kitu kingine na kufanikisha lengo ni kitu kingine.
Lengo likiazimiwa haimaanishi kwamba ndiyo limetimia. Hivyo basi ili kufanikisha lango lako hatua zifuatazo ni lazima zizingatiwe kwanza:-
➡️Andika Malengo Yako…
Ili kutimiza malengo uliyoyaazimia ni lazima uyaandike kwanza. Unachopaswa kujua ni kwamba ili lengo liitwe lengo sharti ni lazima liandikwe… hii ni kwa sababu lengo ambalo halijaandikwa huwa ni tamanio tu ambalo haliwezi kutimizwa.
Unatakiwa uandike kwa sababu akili yako huwa inaingiza taarifa nyingi, kwa mantiki hiyo lengo lisilioandikwa ni rahisi kusahaulika.
Hivyo basi ili kutimiza lengo lako ni lazima uliandike na kulisoma kila siku kabla ya kulala na ukishaamka.
Mbali na hilo unahitaji kuandika malengo yako kwa sababu kuandika kunakufanya utengeneze kitu Fulani unachoweza kukishika na kukisoma kila unapohitaji kukisoma.
Kadhalika unapoamua kuandika lengo lako utajikuta ukiunganishwa na kanuni ya uvutano, matarajio pamoja na kanuni ya matokeo na kisababishi, hii inamaanisha utajisimamia mpaka utimize malengo yako.
Hata hivyo akili yako itatingwa muda wote kukutafutia mbinu zitakazokufanikikishia malengo yako uliyoyaazimia.
➡️Andaa Mpango Kazi Wako…
Usiishie tu kuandika kwamba unataka kutimiza masuala kadhaa, kumbuka malengo huwa hayajitekelezi yenyewe.
Unachotakiwa kufanya ni kuandika mbinu, michakato, pamoja na hatua utakazochukua ili kuhakikisha malengo yako yanatimia.
Unachopaswa kujua ni kwamba mipango pasipo kuazimia mbinu za kuchukuliwa ili kutimiza mipango hiyo itabaki kuwa mipango tu. Andaa mpango kazi utakaokusaidia utimize malengo yako.
➡️Anza kutekeleza…
Mpango kazi hautajitekeleza wenyewe mpaka pale utakapoamua kuanza kuufanyia utekelezaji.
Unachopaswa kujua ni kwamba kitendo kimoja kilichotekelezwa kina thamani kubwa kuliko mipango elfu moja ambayo haijafanyiwa utakelezaji wowote ule.
Malengo hayatatekelezeka pasipo utakelezaji wake. Unachotakiwa kufanya ni kuanza kuchukua hatua zitakazokusaidia utimize malengo yako.
➡️Lifanikishe lengo lako…
Usianze kutekeleza malengo yako kama hakuna chochote ulichokusudia kukifanikisha kwenye malengo hayo.
Ndiyo maana ishawahi kusemwa kwamba siyo kila vita ni ya kupigana, bali unatakiwa upigane vita sahihi itakayokusaidia ufanikiwe maishani mwako.
Usishangae, iko hivi kuna baadhi ya watu hufanya baadhi ya vitu ili waingie tu kwenye rekodi ya kuonekana kwamba walifanya kitu Fulani lakini hakuna chochote walichokusudia kukifanikisha kupitia hicho wanachokifanya.
Kitu unachopaswa kujua ni kwamba hauishi kufanya majaribio, maana maisha siyo majaribio. Hivyo basi unapaswa ukusudie kile unachotaka ufanikiwe kutokana na kile unakifanya.
➡️Dumu Nalo…
Kufanikiwa lengo uliloliazimia inawezekana. Ila kulifanya lidumu na liwe sehemu ya maisha yako ni kitu kingine.
Hii ni sawa na kusema, sawa umefanikiwa kupata tuzo, umeshinda kombe pamoja na kuvikwa medali ni kitu kizuri sana na ni hatua nzuri mno. Lakini kuendelea kushinda mara zote ndiko huleta ukuu.
Usifanikishe lengo lako ili upoteze bali, lifanikishe halafu udumu katika hali ya mafanikio. Unachotakiwa kufanya ni kuendelea kudumu katika kufanya kile kilichopelekea mafanikio hayo kila siku.
➡️Kua Nalo…
Ikiwa kadri siku zinavyozidi kwenda kila mtu anakua kuuelekea uzee pamoja na utu uzima Zaidi, na wewe inatakiwa ukue na lengo lako.
Yaani likuze lengo lako kadri siku zinavyozidi kwenda. Unachopaswa kufanya ni kutanua wigo na mipaka ya kufanikiwa Zaidi. Fikiri nje ya boksi usiridhike na mafanikio kidogo.
➡️Washirikishe Na Wengine Mafanikio Yako…
Kufanikiwa kwa ajili yako tu hakuna maana. Unachopaswa kujua ni kwamba mafanikio yako hayapaswi kukunufaisha wewe pekee bali yawanufaishe watu wengine.
Mbali na hilo unatakiwa kufahamu kwamba maisha yako siyo wewe pekee bali ni namna unavyogusa maisha ya kizazi kilichopo.
Mafanikio maishani mwako yanatakiwa yawanufaishe wengi na yasiishie kukunufaisha wewe pekee.
Kitu kingine unachotakiwa ujue ni kwamba unaishi kwa ajili ya watu wengine, hivyo basi endapo utafanikiwa kutimiza melengo washirikishe na wengine pamoja na kuwapa mbinu zilikusaidia ukafanikiwa katika melengo.
Lengo likiwa ni kufanya jamii yote ifanikiwe. Kumbuka mafanikio yako yatakuwa hayana maana kama yatakunufaisha wewe pekee pasipo kuwanufaisha wengine.
Kwa ujumla unaweza kupanga malengo ya kifedha, kiafya, uwekezaji, ujifunzaji, kiroho, kielimu pamoja na malengo ya kazi na wajibu wako.
Hata hivyo unaweza ukapanga malengo ya muda mfupi au muda mrefu. Mwisho wa yote unapasawa kujua kwamba ili lengo liitwe lengo lazima liwe mahususi, lipimike, liwe halisi, liwe linawezekane kwa kadri ya uwezo wako na liwe na ukomo wa muda Fulani.
Ahsante sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673194329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment