Fahamu Hatua Tatu Ambazo Kila Tabia Iliyokomaa Hupitia Kabla Haijatengenezwa...

Hivi unafahamu kwamba kila tabia iliyokomaa ni lazima hupitia kwenye hatua kuu tatu ambazo hutumika katika kujenga tabia? 

Huenda hata wewe umekuwa ni yule mtu ambaye, umejaribu kujenga tabia fulani lakini umeishia njiani! Usijue shida ni nini, kumbe shida ni kutokujua hatua hizi kuu tatu ambazo kila tabia iliyokomaa hupitia!

Bila shaka unataka kujua hatua hizo muhimu, nami nakutoa hofu juu ya hilo kwani makala hii imedadavua suala hili kwa undani wake!

Unatakiwa kujua kwamba, endapo tabia haitapitia kwenye hatua hizi tatu katika kujengwa kwake basi tabia hiyo haitajengwa bali itakufa!

Ukweli ni kwamba hatua hizi tatu hutegemeana na na hukamilishana! Hata hivyo ukomavu wa tabia hutegemea na kiwango cha ufanywaji na urudiwaji wa tabia hiyo! 

Kwa ujumla zifuatazo ni hatua tatu ambazo hukamilishana katika kupelekea kutokea kwa tabia Fulani. 

1. Kuwepo Kwa Vichochezi (Cues)
Hivi ni vitu mbalimbali vilivyopo kwenye mazingira halisi ambavyo huuchochea ubongo umsukume mtu afanye tabia fulani!

Kwa mfano cues zinaweza kuwa: eneo ulilopo, chupa za pombe, gilasi, pesa, kitabu, muziki, marafiki Fulani, tv, simu, hali Fulani ya kihisia uliyonayo, maarifa au ufahamu pamoja na kitu chochote kinachoweza kutokea kitakachopelekea uweze kufanya tabia fulani!

Unatakiwa kujua kwamba kila tabia uliyonayo ipo kwa sababu kuna kichocheo kinachopelekea ufanye tabia hiyo ambapo mwisho wa siku tabia hiyo imefanyika kuwa sehemu ya maisha yako! 

Tuchukulie labda kwa mwanaume mzinzi cues zake zinaweza kuwa ni wanawake wenye makalio makubwa. Hii ni sawa na kusema endapo itatokea amewaona wanawake hao, basi ubongo wake utamchochea alale nao. Matokeo yake atajikuta kashakuwa malaya...

Jambo moja unalopaswa kujua kuhusu cues ni kwamba uwepo wake hukuchochea wewe ufanye tabia fulani aidha kwa kutaka ama kutokutaka!

Hata hivyo vichocheo hivi (cues) huweza kumchochea mtu afanye tabia Fulani kutegemeana na jinsi ya mfumo wake wa ubongo ulivyoathirika. 

Kwa mantiki hiyo cues moja inaweza kuchochea tabia mbili tofauti. Kwa mfano watu wawili wanaweza kuona cues moja wakaishia kufanya tabia mbili tofauti. Tufanye labda wameona gilasi! 

Kwa Mlevi atachochewa anywe pombe, huku yule ambaye siye mlevi atachochewa kunywa maji au juisi (sharubati)

Mara baada ya tabia hiyo kufanyika ubongo wako utarekodi tabia iliyofanyika pamoja na matokeo uliyoyapata!

 Na, endapo matokeo hayo yatakuwa mazuri utajikuta ukianza kuitikia katika kufanya tabia hiyo pindi ukiona cues katika kila mazingira utakayokuwa!

Hii ni sawa na kusema kuna baadhi ya tabia unazifanya siyo kwa sababu unatakiwa uzifanye ila ni kwa sababu kuna vichocheo vinavyokuchochea ufanye tabia hizo.

Unachopaswa kujua ni kwamba, endapo utajaribu kuacha kufanya tabia Fulani ilihali vichocheo vinavyokuchochea ufanye tabia hiyo, bado vipo mazingira uliyopo hutokuwa tofauti na mtu anayezima moto kwa kutumia petroli.
Unachotakiwa kufanya hapa ni kuvikwepa na kujiweka mbali na vichocheo hivyo.

2. Kuonesha Mwitikio Fulani (Response)
Hapa ni pale mtu unaonesha mwitikio wa kufanya kitendo au jambo Fulani, mara baada ya kuchochewa na cues zilizopo kwenye mazingira uliyopo!

Kama tulivyoona hapo awali kwamba vichocheo hivyo vinaweza kuwa: baa, bia, pesa, mazingira uliyopo, hali ya kihisia uliyonayo, marafiki ulionao kwa muda huo. Hivyo basi uwepo wa vichocheo hivyo vitakusukuma uoneshe mwitikio wa kufanya kitendo kinachotokana na vichocheo hivyo! 

Unatakiwa kujua kwamba kila mwitikio ambao mtu Fulani hufanya huchochewa na vichocheo mbalimbali. 

Kwa mantiki hiyo hata: ulevi, uvivu, ughairishaji mambo, uasherati, ulaji mbovu, kupuuza pamoja na uzinzi siyo tabia ambazo zimeshushwa kutoka mbinguni bali ni mwitikio unaounesha kutokana na uwepo wa vichocheo mbalimbali. 

Kitu unachopaswa kuelewa ni kwamba kichocheo hupelekea mwitikio, mwitikio hupelekea kitendo, na kitendo hupelekea tabia. 

Kutokana na hilo mchezo wa kutengeneza tabia Fulani unakuwa umeishia hapo.

Hivyo basi ubongo wako ukishachochewa, utakuchochea na wewe hapo uweze kuitikia kufanya vitendo hivyo.

3. Matokeo Ya Tabia Hiyo (Reward)…
Kila tabia ambayo hufanyika huweza kuleta matokeo Fulani aidha mazuri au mabaya. 

Unatakiwa kujua kwamba matokeo mabaya hukupa funzo Fulani juu ya madhara ya kufanya tabia hiyo, kwa mantiki hiyo ubongo wako hautakuchochea tena ufanye tabia hiyo hata kama utaziona cues hizo katika mazingira uliyopo. 

Hata hivyo endapo matokeo ya tabia hiyo yatakuwa mazuri yatakutimizia mahitaji yako. Kwa mantiki hiyo, ubongo wako utakuchochea ufanye tabia hiyo mara kwa mara kwa sababu inakidhi haja zako!

Hii inamaanisha endapo utaitikia kufanya tabia Fulani na ikaonesha ina matokeo mazuri basi matokeo hayo yatakuwa kama hamasa au kichocheo cha wewe kufanya Zaidi tabia hiyo.

Kutokana na hilo utajikuta unatengeneza hadi mtindo wa kuishi utakaokuwa unaratibu ufanywaji wa tabia hiyo.

Kwa mfano endapo utatembelea baa, utaomba bia utainywa, utajisikia kuburudika sana. (haya ni matokeo mazuri yanayotokana na unywaji pombe).

 Hivyo basi kutokana na tabia hiyo kukuletea matokeo mazuri, itakuwa ni kama kichocheo au hamasa ya kukuchochea uweze kunywa Zaidi mwisho wa siku utajikuta ushakuwa mlevi…

Kwa ujumla tabia yoyote ile iwe nzuri au mbaya katika kutengenezwa kwake ni lazima iweze kupitia hatua hizo kuu tatu. 

Na, endapo haitapitia hatua hizo haitweza kujengwa bali itakufa. Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba hatua hizo tatu za kujenga tabia ndizo hizo pia hutumika katika kubomoa na kuharibu kabisa tabia Fulani. 

Je, nifanye nini ili niharibu tabia mbaya?
Je, nifanye nini ili nijenge tabia mpya?

Usijalii fuatana nami kwenye mwendelezo wa somo hili...

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...