Fahamu Jinsi Ambavyo Tabia Hutengenezwa Kwenye Mfumo Wa Ubongo..
Katika ulimwengu wa saikolojia inaaminika kwamba hakuna binadamu hata mmoja ambaye huzaliwa akiwa na tabia!
Dai hili ni kwa mujibu wa nadharia kongwe iliyoanzishwa na mwanafalsafa maarufu sana kuwahi kutokea duniani akifahamika kwa jina la David hume. Nadharia hiyo ilipewa jina la “blank slate/tabularasa”.
Kwa mujibu wa nadharia hii ni kwamba hakuna binadamu ambaye huzaliwa akiwa na tabia, ufahamu au uelewa wa jambo lolote lile.
Kutokana na ukweli huo madai ya nadharia hiyo kongwe yakahitimishwa kwa kuona kwamba vile mtu atakuwa kitabia, kimtizamo pamoja na kimienendo ni kumbukumbu za mambo yote yaliyoingia ubongoni mwake mara baada ya kuzaliwa kwake na kuanza kuishi hapa duniani.
Unachopaswa kuchukua hapa ni kwamba kila tabia yoyote ile uliyonayo imetengenezwa na wewe mwenyewe. Yaani mbali na ukweli kuwa uliumbwa huna budi kukubali kwamba umejitengeneza mpaka ukawa hivyo ulivyo.
Kitu kingine cha kuongezea hapa unatakiwa kujua kwamba hakuna binadamu ambaye alizaliwa akiwa: mlevi, muasherati, mhuni, mjinga, mghairisha mambo wala muoga na hakuna binadamu aliyeandikiwa kwamba atakuwa na tabia zote hizo maisha yake yote.
Bali mtu atabaki kuwa na tabia zote hizo hatarishi maisha yake yote endapo atabaki katika kiwango kilekile cha ufahamu pamoja na kubaki katika mazingira yaleyale.
Mbali na hilo unatakiwa kujua kwamba kama mpanzi apandavyo mbegu shambani na zikaota na kustawi ndivyo na wewe unavyopanda tabia mbalimbali katika maisha yako.
Yaani unapanda wazo unavuna kitendo, unapanda kitendo unavuna tabia, unapanda tabia unavuna utambulisho, unapanda utambulisho unavuna hatima.
Jambo moja unalopaswa kuondoka nalo sehemu hii ni kwamba umejitengeneza mwenyewe mpaka ukawa hivyo ulivyo. Yaani Umekuwa Mlevi/mzinzi/mhuni kwa sababu ulipanda mbegu za za tabia hizo jana, na ndiyo maana leo umejikuta ukivuna mavuno mabaya ya mapando yako...
Je Tabia Hutengenezwaje Katika Mfumo Wa Ubongo?
Kwa mara ya kwanza mtu ukitembelea mazingira mapya ambayo hukuwahi kufika akili yako huwa ipo pale kwa ajili ya kujifunza.
Hivyo basi unapofika eneo hilo na kuanza kufanya baadhi ya matendo pamoja na ishara mbalimbali akili yako itarekodi jambo ulilolifanya pamoja na matokeo uliyoyapata.
Kutokana na kumbukumbu hiyo kubaki kichwani mwako hii inamaanisha siku ikitokea umeenda mazingira yaleyale na kukutana na vitu vilevile akili yako itakachokifanya ni kukurudisha kwenye kitendo ulichokifanya kwa mara ya kwanza pamoja na matokeo uliyoyapata mara baada ya kufanya kitendo hicho.
Kutokana na hilo utajikuta unaitikia automatiki kwa kufanya kitendo kilekile ulichokifanya mara ya kwanza. Hivyo basi endapo utafanya kitendo hicho kwa muda mrefu utajikuta unaanza kuwa mraibu katika kufanya tabia hiyo.
Kwa mfano siku ya kwanza ulijikuta unaenda baa, ukaagiza kinywaji, ukanywa ukajisikia vizuri. Hivyo basi akili yako ikarekodi kitendo ulichokifanya pamoja na matokeo uliyoyapata mchezo ukawa umeishia hapo.
Siku ya pili katika mishe zako ukajikuta unakutana na mazingira yaleyale. Kilichofanyika hapo akili yako ilichakata na kukurudisha kwenye kitendo ulichokifanya mara ya kwanza pamoja na matokeo uliyoyapata.
Kutokana na hilo ukajikuta unaitikia automatiki katika tena kuagiza kinywaji kama kawaida ili upate kuburudika, ujihisi fahari.
Siku nyingine tena ikafika ukafanya vivyo hivyo. Sasa basi, hebu jaribu kuvuta picha umefanya hivyo kwa mwaka mzima. Je ni kweli ulevi utaukwepa?
Kiufupi tunaweza kusema kwamba kuwa mlevi hakutazuilika na utashindwa kujizuia kutokulewa kwa sababu ulevi utakuwa umefanyika kuwa sehemu ya maisha yako.
Unatakiwa kujua kwamba hakuna muda maalumu kwa ajili ya kutengeneza tabia Fulani bali kiwango cha kurudia katika ufanyaji wa tabia hiyo, ndicho hupelekea tabia hiyo iwe sehemu ya maisha yako, ambapo mwisho wa siku utajikuta ukitengeneza mpaka mtindo wa maisha kabisa unaoratibu ufanywaji wa tabia hiyo.
Je, ni hatua zipi ambazo Kila tabia iliyokomaa hupitia?
Usijalii, fuatana nami kwenye mwendelezo wa somo hili...
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment