Huwezi Kubadili Kilichotokea Pasipo Kwanza Kubadili Tabia Zilizopokelekea Kutokea Kwake…
Hivi unafahamu kuwa hivyo ulivyo, hali unazopitia pamoja na hapo ulipo kimaisha ni matokeo ya tabia zako mwenyewe?
Ukweli ni kwamba kuna watu wako leo hii wanalaumu kuhusu hali wanazopitia kimaisha, huku wengine wakiwa wanapambana kubadili matokeo yanayotokana na hali hizo, wasijue kwamba huwezi ukabadili kilichotokea kama hutaanza kwanza kubadili chanzo kilichopelekea kutokea kwake!
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba: umaskini, kutengeneza kipato cha chini, mateso, shida, taabu pamoja na maradhi mbalimbali yanayowakumba watu wengi ni matokeo ya tabia zao wenyewe.
Ukweli ni kwamba tabia ni kama panga lenye makali pande zote mbili, ambalo hukata kotekote. Kwa mantiki hiyo tabia zako zinaweza kukupaisha mpaka juu mawinguni na kukufanya ufikie mafanikio ya kiwango cha juu, hata hivyo tabia zako zinaweza kukudimiza na kukushusha katika viwango vya chini na ukaonekana si kitu!
Kwa mfano tabia ya kuishi bila bajeti inaweza kukuingiza kwenye madeni pamoja na kukuletea umaskini, tabia ya kukaa tu pasipo kufanya chochote kile inaweza kukusababishia umaskini pamoja na kutokutengeneza pato la kuridhisha, tabia ya kuendekeza anasa na starehe kwa mfano uzinzi na uasherati inaweza kupelekea kuambukizwa magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI pamoja kupata mimba zisizotarajiwa.
Hata hivyo tabia ya ulaji mbovu inaweza kupelekea baadhi ya maradhi na magonjwa yanayohatarisha afya yako ikiwa ni pamoja na unene uliopitiliza na kupata kitambi.
Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kwamba, tabia ya kutokudadisi inaweza kupelekea ushindwe kutumia fahamu zako katika kiwango cha juu na kupelekea anguko lako kimaisha.
Mbali na hilo tabia ya kutokupenda kujifunza inaweza kupelekea ukawa mjinga kiasi kwamba ukashindwa kujitambua wewe ni nani, uko wapi na unaenda wapi pamoja na ufanye nini ili upate kufika huko unakotaka kufika!
Mpaka hapo umeona unatakiwa upambane na matokeo au upambane na tabia tabia zako zinazopelekea matokeo hayo?
Ni wakati wa kuanza kutawala tabia zako kwanza ili ubadili matokeo yanayosababishwa na tabia zako.
Na, ndiyo maana kanuni ya kichocheo na matokeo inasema kwamba; “kila kitu hutokea kutokana na sababu”
Hii ni sawa na kusema kuwa, kuna kila sababu ambazo zimepelekea wewe kuwa hivyo ulivyo, kupitia hayo yote unayoyapitia pamoja na kufika hapo ulipofikia kimaisha.
Na, sababu hizo ni tabia zako, na hii ni kwa sababu tabia zako ndizo hupima hulka yako, mitizamo yako, fikra zako pamoja matendo yako unayoyafanya kila leo. Au kiufupi tuseme, tabia zako ndizo hupima kila kinachotokea katika maisha yako.
Hata hivyo kisaikolojia inaaminika kwamba tabia zetu ni mbinu tulizojifunza ili kutatua baadhi ya changamoto zinazotukumba. Na, mara baada ya kutatua changamoto hizo, ubongo wetu hurekodi tabia tulizozifanya ili kutatua changamoto hizo.
Hivyo basi endapo itatokea umekumbana na changamoto ile ile ubongo wako utakurejeshea ile tabia uliyoifanya awali ili kuikabili changamoto hiyo. Matokeo yake utajikuta ukiifanya tabia hiyo tena kwa mara nyingine haijalishi ni tabia nzuri au laah!
Kwa mfano tufanye mfukoni mwako huna hata mia mbovu, na ukawa una shida na kiasi Fulani cha fedha. Katika kuwaza kwako ukasikia fikra zako zikakuambia; “ndugu zako na rafiki zako wana fedha za kutosha, hebu omba kwao nao watakusaidia”
Kweli bwana ukaamua kuwaomba, na ukasaidiwa shida yako. Ubongo wako ukarekodi hilo, kwamba nikikumbana na shida ya fedha, nitapaswa kuomba kwa ndugu, jamaa na rafiki.
Kwa hiyo kila siku ukiwa una uhitaji wa fedha ukajikuta ukiwaomba ndugu, jamaa na rafiki, mpaka unataka ugeuke na kuwa ombaomba haha!
Na, ndiyo maana mpaka leo hii kuna watu hawajitegemei kiuchumi, mbali na kuwa umri wao umeenda na wana familia zao. Hii ni kwa sababu akili zao zimehalalisha kutafutiwa Zaidi kuliko kutafuta mbinu ambazo zinazoweza kutumika ili kutengeneza fedha.
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba huo ni mfano tu unaoonesha jinsi gani umeweza kutumia tabia Fulani kama mbinu ya kutatua baadhi ya changamoto, matokeo yake ukaishia kuwa kilema.
Hata hivyo unaweza ukatumia hata dakika moja kufikiri juu ya tabia zote unazozifanya halafu uhusianishe na changamoto ulizokuwa unazitatua pindi unafanya tabia hizo.
Ndugu, unatakiwa kujua kwamba mwenye afya anazidi kuwa na afya bora kwa sababu anafanya tabia zinazopelekea afya njema, tajiri anazidi kuwa tajiri kwa sababu anafanya tabia zinazopelekea utajiri na maskini naye anazidi kuwa maskini kwa sababu anafanya tabia zinazochoea umasikini!
Kwa mantiki hiyo kwenye maisha unapata matokeo kutokana na kile unachokifanya. Na, ndiyo maana Aristotle alishawahi kusema kuwa; “sisi sote ni matokeo ya kile tulichokirudia kukifanya”
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba tabia huwa haitengenezwi ndani ya siku moja bali ni mchakato unaohusisha ufanywaji wa tendo hilo mara kwa mara, kiasi kwamba tendo hilo linakuwa linaratibiwa na ubongo automatiki.
Kwa hiyo endapo kitendo Fulani kitafanywa sana maana yake utajikuta ukifanya pasipo kujua kwamba unafanya, matokeo yake utajikuta umeshakuwa sugu kwenye tabia hiyo.
Na hii ndiyo sababu kubwa tuna walevi wa kupindukia, tuna Malaya wa kutupwa, tuna ujinga wa kutosha, tuna watumia madawa ya kulevya pamoja na waghairisha mambo wa kutosha.
Watu hao hujikuta wakifanya tabia hizo siyo kwa vile wanapenda bali hujikuta wakiitikia kuzifanya automatiki pasipo hata kujua kuwa wanazifanya kwa sababu, tabia hizo zimeshapokelewa kwenye ubongo na ubongo nao unachochea ufanywaji wa tabia hizo kirahisi.
Je, tabia ni labda?
Je, tabia hutengenezwaje kwenye mfumo wa ubongo?
Je, nifanye nini ili niharibu tabia mbaya?
Je, nifanye nini ili nijenge tabia mpya na nzuri?
Usijalii fuatilia mwendelezo wa somo hili kwa siku ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment