Huwezi Ukaelewa Tabia Ni Nini Mpaka Usome Kwanza Hii...
Neno tabia huenda likawa siyo geni sana machoni pakao ewe mpenzi msomaji na sina shaka endapo utaulizwa ulitolee ufafanuzi utashindwa kulifafanua.
Ni Imani yangu kuwa, maana yako haitakuwa mbali na ile isemayo; tabia ni jumla ya matendo yote pamoja na vitendo mbalimbali avifanyavyo binadamu katika maisha yake ya kila siku pasipo hata kutumia ridhaa/hiari yake.
Hii ni sawa na kusema kuwa, mtu huyo hujikuta akiitikia kufanya baadhi ya vitendo na matendo mbalimbali automatiki pasipo hata kujua kuwa anafanya, kwa sababu siyo yeye anayetaka kufanya hivyo bali ubongo wake ndiyo unamchochea afanye hivyo.
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba ubongo humchochea mtu huyo, afanye tabia hizo kwa sababu anakuwa amezifanya kwa muda mrefu, kiasi kwamba tabia hizo zinakuwa zimepokelewa kwenye mfumo wake wa ubongo, matokeo yake ubongo huo huishia kumtengenezea mtu huyo mfumo wa kuratibu ufanywaji wa tabia hizo kila muda!
Kutokana na hilo mtu huyo hujikuta akiitikia kufanya tabia hizo automatiki pasipo kufikiri, ikiwa ni pamoja na kutokutambua kuwa anafanya tabia hizo. Na, hii ni kwa sababu kwa wakati huo tabia zake zinakuwa ni kitu ambacho kinatawaliwa na mfumo wake wa ubongo!
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, tabia ni jumla ya vitu vyote unavyofanya pasipo kutumia fikra wala nguvu bali unajikuta ukivifanya tu bila hata kudadisi.
Kwa mfano ukitaka kusimama huwezi ukaanza kufikiri kwamba utasimamaje bali utajikuta ukisimama tu, pia ukitaka kuanza kutembea huwezi ukafikiri utaanzaje kutembea bali utajikuta tu ukianza kutembea automatiki.
Unajua ni kwa nini unafanya hivyo pasipo kufikiri? …ndiyo upo sahihi ni kwa sababu matendo hayo yanakuwa yanatawaliwa na ubongo, kwa hiyo ubongo wako unapunguza wajibu wako wa kufikiri juu ya kufanya matendo hayo, bali utajikuta ukiyafanya automatiki!
Mpaka hapo ni matumaini yangu umeona nguvu ya tabia inavyoathiri mfumo wa utendaji kazi wa ubongo wako!
Ubaya kuhusu tabia ni kwamba humtengenezea utambulisho yule mtu anayefanya tabia hizo, na utambulisho huo hutegemeana na aina za tabia ambazo mtu huyo anakuwa amezichagua katika maisha yake!
Kwa mantiki hiyo endapo mtu huyo atachagua tabia njema atatambulika kuwa ni mtu mwema na endapo atachagua tabia mbaya atatambulika kuwa ni mtu mbaya!
Kwa mfano: kuna watu wanatambulika kuwa ni walevi kwa sababu ya tabia zao za kulewa, kuna watu wanatambulika kuwa ni Malaya kwa sababu ya tabia zao za uzinzi na uasherati, kuna watu wanatambulika kuwa ni wezi kwa sababu ya tabia zao za wizi, kuna watu wanatambulika kuwa ni wambea kwa sababu ya tabia zao za umbeya, kuna watu wanatambulika kuwa ni wazembe na wavivu kutokana na tabia zao za kutokuwajibika, n.k.
Unachopaswa kujua ni kwamba watu wanakutambua hivyo ulivyo kutokana na tabia zako zilivyo, kwa hiyo ninakupa wito siku ya leo jaribu kuwauliza watu wako wa karibu kuwa wewe ni mtu wa aina gani.
Kumbuka tabia zako ndizo zinazokutambulisha, kwa mantiki hiyo ukitaka kubadilisha utambulisho wako huna budi kubadili aina ya tabia zako kwanza kwa sababu ndizo zinazokutambulisha kwa watu!
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba aina ya tabia unayochagua kufanya ndiyo inapima aina ya mtu unayekuwa, na ndiyo maana mimi huwa naamini kuwa; “mafanikio ni kitu ambacho unakivuta kutokana na yule mtu unayekuwa kitabia”
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba nguvu ya kuchagua ipo mikononi mwako, na yule unayemchagua ndiye unayekuwa kiutambulisho!
Hivyo basi kutokana na watu wengi kuwa na tabia hasi wamejikuta wakipata matokeo mabaya maishani mwao, siyo kwa sababu wanatakiwa kupata matokeo hayo bali ni kwa sababu tabia zao ndizo zinawapelekea wapate matokeo hayo.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye hufanikiwa kutatua matokeo ya tatizo, isipokuwa kuna yule mtu ambaye hufanikiwa kutatua chanzo cha tatizo (tabia), na ukishatatua chanzo cha tatizo (tabia) basi huo ndiyo utakuwa mwisho wa tatizo lenyewe!
Unatakiwa kujua kwamba kuna baadhi ya matatizo yanahitaji kiwango kingine cha fikrza Zaidi ya zile zilizopelekea kutokea kwake, kwa maana huwezi kutatua tatizo kwa kutumia kiwango kilekile cha fikra kilichotumika wakati wa kupelekea kutokea kwake.
Hata hivyo tabia hizi zinapotengenezwa huanza kidogo kidogo lakini kadri zinavyozidi kufanyika ndivyo huzidi kukua na kukomaa Zaidi, kiasi kwamba zinatengeneza uraibu kwenye ubongo hali ambayo hufanya tabia hizo ziweze kuratibiwa kwa wepesi!
Utata huja pale ambapo watu hupuuza tabia hizo na kuona kwa sababu ni ndogo hazina athari, wasijue kwamba duniani hakuna mambo madogo hasa ukilinganisha na mambo makubwa yanayotokana na mambo madogo.
Na, ndiyo maana siyo rahisi kung’atwa na tembo aliye mkubwa ila ni rahisi kung’atwa na mbu aliye mdogo na ukaambukizwa na malaria.
Hii ni sawa na kusema ufanyaji wa tabia hatarishi ndogo ndogo ndani ya kipindi cha muda Fulani kwa kiasi kikubwa umaeleta athari nyingi maishani mwetu.
Kama unataka kubadili maisha yako, badili tabia zako kwanza. Kumbuka duniani hakuna mambo madogo kwa maana hata mambo makubwa hutokana na mambo madogo.
Yoshua bin sira 19: “Afanye hivyo hapati kuwa Tajiri, wala kibarua aliye mlevi. Anayedharau mambo madogo ataanguka kidogo kidogo”
Je, tabia hutengenezwaje kwenye mfumo wa ubongo?
Je, ni hatua gani ambazo hutumika ili kujenga tabia?
Je, nifanye nini ili niweze kuharibu tabia mbaya?
Je, nifanye nini ili niweze kujenga tabia mpya na nzuri?
Fuatana nami kwenye mwendelezo wa somo lijalo!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment