Je, Unataka Kujenga Tabia Mpya Zitakazobadilisha Maisha Yako? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...

Habari yako rafiki yangu? Ni matumaini yangu u mzima wa afya.
Karibu kwenye mwendelezo wa somo letu linaloangazia kuhusu jinsi ya kuharibu na kujenga tabia mpya.

Ikumbukwe makala iliyopita ilidokeza ni namna gani unaweza ukaharibu tabia yoyote ile kwa kutumia kanuni kuu tatu za kubadili tabia.

Makala yetu ya leo itaenda kukuonesha jinsi ya kujenga tabia mpya zitakakusaidia ubadili maisha yako kwa kutumia kwa kanuni kuu tatu za kubadili tabia!

Je, nifanye nini ili niweze kujenga tabia mpya ambazo awali sikuwa nazo? Usijalii fuatana nami...

1. Vichocheo Vya Tabia (cues)
➡️Fanya Vichocheo Vya Tabia Unazozitaka Viwepo Mazingira Uliyopo Ili Vikuvutie Zaidi. 

Unatakiwa utengeneze mazingira yako ya sasa ili kitendo cha baadae kifanyike kwa urahisi!
Kumbuka usipoandaa mazingira yatakayokusaidia ufanye tabia unazozitaka hakuna atakayekuandalia, badala yake sasa mazingira uliyopo ndiyo yatakayokuamlia aina gani ya tabia uzifanye.

Rafiki, unatakiwa kujua kwamba kila tabia unayoifanya inachochewa na uwepo wa cues/vichocheo katika mazingira uliyopo. 
Kwa mantiki hiyo ili ufanikiwe kujenga tabia mpya ni lazima uhakikishe unaandaa vichocheo vyote vitakavyokusukuma ufanye tabia hizo viwepo katika mazingira uliyopo!

Kwa mfano kama unataka ujenge tabia ya kujisomea ni lazima ufanye yafuatayo: nunua kiti na meza (sehemu maalumu ya kusomea), nunua vitabu vya kutosha, weka vitabu hivyo eneo la wazi chumbani mwako kwa mfano kitandani, mezani au sehemu yoyote ile itakayoonekana kwa urahisi ukishaingia tu chumbani mwako. 
Unatakiwa uweke sehemu ya uwazi ili ubongo wako ukuchochee uweze kufanya tabia ya kusoma, mara baada ya kuviona Vichocheo vya tabia hiyo!

Vilevile kama unataka ujenge tabia ya kutekeleza majukumu yako kwa mwendelezo pasipo kughairisha unaweza ukafanya yafuatayo: andika orodha ya malengo yako unayotaka kuyatimiza kwa lugha ya wazi na kwa kutumia wakati uliopo, baada ya kuandika yatengenezee picha kamili juu ya hatima yake.

Ukishaunda hatima yake, yabandike malengo hayo katika eneo lilio wazi chumbani mwako, kiasi kwamba kila ukiingia chumbani mwako yaonekane kwa urahisi.
Mara baada ya kufanya hivyo yasome kila siku asubuhi baada ya kuamka na jioni kabla ya kulala. 

Hata hivyo wakati wa kusoma hakikisha kuwa unayasoma kwa kuyarudirudia mpaka uhakikishe yamezama kwenye sehemu ya pili ya akili yako iitwayo subconscious mind ambayo ni mahususi kwenye kuchakata picha. Picha hizo zikishachakatwa zitachochea kiwango chako cha hisia. Hisia zikishachochewa zitakusukuma uweze kufanya bidii na juhudi zaidi ili uyafikie malengo yako!

Habari njema ni kwamba endapo utapata hisia kali juu ya malengo yako utapata hamasa na kiu ya kuyafikia malengo hayo. Kwa mantiki hiyo utajikuta ukihamasika uweze kufanya juhudi Zaidi ili kuyafikia malengo hayo. Kutokana na hilo hutajikuta ukihaghairisha tena mambo kwa sababu kuna mwisho mwema unataka kuufikia.

Angalizo: inafaa uyaandike malengo yako kwa kutumia lugha ya uwazi iliyo katika wakati uliopo. Hata hivyo ni muhimu ukayabandika malengo yako katika eneo lililo wazi ili iwe rahisi kuyasoma mara kwa mara. Kumbuka kadri unavyosoma ndivyo unavyozidi kutengeneza hisia za kutimiza malengo hayo.  

Hata hivyo endapo unataka kutengeneza tabia nyingine mpya unatakiwa uandae kwanza mazingira rafki kwa ajili ya ufanyikaji wa tabia hizo. 

Unatakiwa ujiulize kwanza ni aina gani ya mazingira yatakayokusaidia ufanye tabia hizo kwa urahisi. Kumbuka huwa tunafanya baadhi ya tabia si kwa sababu tunatakiwa tufanye tabia hizo, bali ni kwa sababu mazingira tuliyopo yanatutaka tuzifanye tabia hizo!

Daima andaa mazingira yako, ili kitendo kijacho kifanyike kwa urahisi! 

2.  Mwitikio Wa Tabia Hiyo (Response)
➡️Weka Urahisi Katika Kuitikia Kufanya Tabia Hiyo...

Hapa unatakiwa uoneshe mwitikio wa kufanya tabia hizo kwa urahisi. Kwa mfano kama unataka uanze kufanya mazoezi na hujawahi kufanya unatakiwa kununua nguo za mazoezi kwanza, halafu uandae muda utakaokuwa unatumia kufanya mazoezi.

Unatakiwa kujua kwamba ni ngumu sana kuanza kufanya tabia mpya ambazo hapo awali hukuwa nazo kabisa, kwa hiyo moja ya mbinu ambayo napendekeza uitumie hapa ni kanuni ya dakika mbili. 

Kanuni hii inasema; "fanya tabia mpya kwa muda wa dakika mbili tu, usiongeze wala usipunguze" Kwanini unashauriwa dakika mbili tu, sababu kubwa ni kutouchosha mwili wako ikiwa ni pamoja na kuepuka hatari ya ubongo wako kukutengenezea fikra hasi juu ya tabia hiyo.

Unatakiwa kujua kwamba endapo utafanya kwa muda mfupi utajisikia burudani, kwa mantiki hiyo kesho ikifika ubongo wako utakuchochea uende ukafanye tabia hiyo kwa mara nyingine tena. 

Unachotakiwa kufanya kwa siku ya pili ni kuitikia kwa urahisi katika kufanya tabia hiyo, lakini kwa siku ya pili unashauriwa uongeze muda utakaotumia kufanya tabia hiyo!

Kwa mfano kama siku ya jana ulitumia dakika mbili basi siku ya pili ongeza dakika mbili zingine. Fanya hivyo kwa kila siku utakayokuwa unafanya tabia hiyo, hakikisha unaongeza muda wa kufanya tabia hiyo.

Kosa kubwa la kuepuka: epuka kukosa kufanya tabia yako mpya mara mbili (never miss twice), kwa sababu endapo utakosa kufanya tabia yako mara mbili utajikuta ule muda uliokuwa unatumia kufanya tabia yako mpya unautumia kufanya kufanya tabia nyingine, matokeo yake utajikuta ukiacha kufanya tabia yako uliyoipanga kuifanya na kuishia kufanya tabia nyingine. 

Na hii ndiyo sababu kubwa utakuta watu wengi wanaanzisha tabia mpya lakini wanaishia njiani, hali hii inachangiwa na kukosekana kwa kwa sanaa ya mwendelezo katika ufanyaji wa tabia hiyo.

Rafiki, endapo utapanga kufanya tabia Fulani itikia katika kuzifanya kwa urahisi, kumbuka usipoitikia kwa urahisi huwezi ukapata hamasa ya kufanya tabia hizo.

Hata hivyo unaweza ukahusianisha ufanyaji wa tabia Fulani mpya na kitu ambacho huwa unakipenda sana bila kutumia nguvu, ili upate urahisi wa kuitikia ktika kufanya tabia yako mpya!

Kwa mfano kwangu mimi huwa nahusianisha kufanya tabia yangu ya kusoma na kusikiliza muziki. Ninapenda kusikiliza muziki, kwa hiyo kama sijisikii kusoma huwa nafungulia muziki na kuanza kusoma, kwa sababu muziki ni kitu ambacho situmii nguvu nikisikiliza mudi nzuri hunijia, matokeo yake nitajikuta ninaanza kufanya na tendo la kutumia nguvu (kusoma), kwa sababu nimehusuanisha ufanyaji wa tendo la kutumia nguvu na tendo la kutokutumia nguvu!

Matokeo yake nitahama kutoka kusikiliza muziki na kujikuta ninasoma kwa undani!

Hii ni sawa na kusema, kihisia nitakuwa nasikiliza muziki lakini kiufahamu nitakuwa ninasoma na kuulisha ubongo wangu kitu kipya! 

Hata wewe hapo ili uweze kufanya baadhi ya tabia unatakiwa uhusianishe na kile kitu ambacho unakipenda, ambacho huwa unakifanya pasipo kutumia nguvu, endapo utafanikiwa katika hilo utaweza kufanikiwa katika kutengeneza tabia zako mpya. 

3. Matokeo Ya Tabia Hiyo (Reward)
➡️Fanya Matokeo Ya Tabia Hiyo Yaridhishe (Yafanye Matokeo Hayo Yawe Na Manufaa)

Awali tuliona kwamba ile tabia ambayo huonekana ina matokeo mazuri ndiyo hurudiwa kufanywa, hii ni sawa na kusema endapo utafanya matokeo yanayotokana na ufanywaji wa tabia Fulani yawe mazuri ndivyo utakavyouchochea ubongo wako ukupe hamasa na motisha ya kufanya Zaidi tabia hizo. 

Kwa mfano endapo utaona kutakuwa na matokeo mazuri utakayoyapata endapo utatumia muda wako vizuri, utajikuta ukianza kutumia muda wako vizuri hali itakayokuletea manufaa maishani mwako!

Kumbuka chenye matokeo mazuri huchochewa ili kifanyike Zaidi, ikiwa kile kilicho na matokeo mabaya huzuiwa ili kisirudiwe kufanywa. Hii ni sawa na kusema kwamba ubongo wako utakuwa kama kichochoeo kitakakuchochea ili urudie kufanya tabia hizo mara kwa mara. 

Kwa mfano unaweza ukataja orodha ya manufaa yatakayopatikana mara baada ya kufanya tabia ya kujisomea vitabu kama yafuatayo: nitakuja kuwa mtu mkuu, nitakuja kuwa mbeba maono wa taifa na jamii yangu, nitakuwa mtatua matatizo ya watu, nitapata maarifa yatakanifanya niishi maisha mazuri, nitakuwa mtu maarufu na mwenye akili nyingi, nitakuwa mwandishi mkubwa, nitaweza kuwashauri pamoja na kuwaongoza watu wangu, nitaweza kutengeneza mamilioni ya fedha kutokana na kukua kimaarifa, kiujuzi na kiufahamu, n.k. 

Rafiki, kwa kila tabia mpya unayotaka kuifanya hakikisha unafanya matokeo yatakayopatikana mara baada ya kufanywa kwa tabia hayo yaridhishe yaani yawe na manufaa!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184339 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...