Fahamu Jinsi Ambavyo Mfumo Wa Malezi Humtengeneza Mwanadamu Kifikra...
Awali ya yote unatakiwa kujua kwamba, eneo la malezi ni eneo nyeti sana, ambalo ndilo kwa mara ya kwanza huhusika katika kumtengeneza au kumharibu mtu kifikra, kupitia taarifa zinazoingizwa ubongoni mwake!
Na, ifahamike kwamba hakuna mwanadamu ambaye huzaliwa akiwa na ufahamu au uelewa wowote ule, suala hili lilithibittishwa na David Hume kupitia nadharia yake aliyoipa jina la blank slate/taburalasa!
Hata hivyo kisaikolojia inaaminika kwamba, kile kitu ambacho mtoto hukutana nacho wakati wa ukuaji wake, ndicho humfanya awe vile alivyo! This is what we call the effect of conditioning...
Ukweli ni kwamba wazazi au walezi ndiyo watu wa kwanza, ambao huingiza taarifa kwenye ubongo wa mtoto!
Na, taarifa hizo huweza kuwa mbaya au nzuri! Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wazazi/walezi wengi huingiza taarifa hasi zaidi kwenye ubongo wa mtoto, na hii ni kwa sababu ya watu wengi kuwa na mitizamo hasi kuhusu maisha!
Hebu jaribu kurudisha kumbukumbu zako nyuma ulivyokuwa mtoto, halafu vuta picha kuhusu kauli, maneno na matendo uliyofanyiwa na watu wako waliokukuza!
Bila shaka umeshapata picha kamili juu ya yote uliyokutana nayo enzi za utotoni mwako!
Rafiki kama ulifanyiwa mazuri hongera, hata hivyo endapo ulifanyiwa mabaya nakupa pole, lakini pia nakupa hongera kwa sababu makala hii itakusaidia ufanye nini, ili ubadili mitizamo yako kuhusu wewe na dunia yako!
Ukichunguza suala hili kiundani utagundua kwamba watu wengi walifanyiwa mambo hasi na watu wao waliowazunguka! Na pengine labda waliambiwa mambo hasi kwa sababu wazazi wao walikuwa ni watu wa mitizamo hasi!
Mbali na hilo eneo hili pia huhusu masuala kadhaa kama vile:-
1.Kupuuzwa Kwa Mtoto (Neglect Of A Child)
Hapa mtoto anakosa muda wa kuwa na wazazi kwa kuachwa mpweke kwa kipindi kirefu, huenda wazazi waliumwa hivyo akatengana nao au wazazi waliachana, au wazazi ni watu wa kusafiri sana kuondoka alfajiri na kurudi ni usiku sana, au wengine hurudi baada miezi kadhaa.
Mtoto anakuwa mpweke muda mwingi hivyo anatengeneza fikra za kuona kuwa hapendwi na hathaminiwi na wazazi wake, ambapo ataanza kutengeneza fikra za kujichukia.
Mbali na hilo huenda mtoto akawa alilelewa kwa bibi na babu au ndugu wengine ambapo hawakumuonesha ukaribu wao kwake.
Malezi ya mtindo huu humuathiri mtoto na humfanya ajitengenezee fikra hasi za kujichukia na kujiona hana thamani juu ya lolote lile. Hali ambayo inafifisha kabisa kiwango chake cha kujitambua kwani amelelewa kwenye mazingira ya unyonge.
2. Mateso Kwa Mtoto (Child Abuse)
Hapa ni pale mtoto anapitia manyanyaso mbalimbali kama vile vipigo vya mara kwa mara ambavyo humsababishia ulemavu, kuchomwa kwa baadhi ya viungo vyao, wengine kukatwa baadhi ya viungo mfano vidole.
Mbali na hilo matukio kama vile kuingiliwa kimwili, ulawiti na ubaguzi wa kijinsia. Hata hivyo eneo hili pia huhusisha mambo kama vile mtoto kuitwa majina ya ajabu, kupewa vitisho, kukatishwa tamaa, kejeli na kuzuiwa kuongea.
Watoto kama hawa kiuhalisia hawawezi kukua na kuwa na kiwango cha juu cha kujitambua kwani fikra zao zimeshaharibiwa na wazazi.
Siyo kwamba kila kitu mtoto atakachokihitaji akifanye au apewe lahasha! Maana yangu ni kwamba je kauli zipi na mbinu zipi zinatumika kumkataza. Tusije tukadhani tunajenga kumbe tunabomoa.
Mwisho kabisa mtoto aliyepuuzwa na kunyanyaswa akishakua hawezi kuwa na fikra chanya hata mara moja, zaidi ya kuwa na fikra za kujichukia na kujiona ni mnyonge.
hili tumeshaliona kwa kile mwanafalsafa David Hume alivyolieleza kwenye nadharia yake ya tabula rasa (blank slate), kuwa mtoto hazaliwi akiwa na fikra hasi, bali fikra hasi zote ni jumla ya mambo yote yaliyoingia ubongoni mwake tokea utotoni mwake.
Hivyo basi kutokana na mtoto kukutana na majanga kama hayo, taarifa nyingi zitakazorekodiwa ubongoni mwake zitakuwa hasi, hali itakayomfanya mtoto ajione yeye hawezi kujiongoza, kujisimamia wala kujitawala, ambapo atashindwa kujitambua kuwa yeye ni nani!
Kutokana na kufanyiwa masuala hayo, wewe kama mtoto utajiona kama hastahili, huwezi, siyo Bora, wewe ni duni, hutofanikiwa na hutobadili kitu maishani mwako. Usijue kwamba kuna kamfumo wazazi wamekutengenezea ambako kamekuathiri..
Ukichimba ndani zaidi utagundua kwamba suala hili litaathiri fikra zako juu yako, kwa sababu kwa kiasi kikubwa ubongoni mwako zimerekodiwa taarifa hasi, rejea nadharia ya blank slate.
Kwa mantiki hiyo mtoto utakua akijua una upungufu sehemu... Hivyo basi utajiona wewe ni mdhaifu na huwezi hata kuishi maisha ya furaha, amani na mafanikio..
Rai yangu kwa wazazi/walezi popote pale mlipo muone mchango wenu ulivyo mkubwa katika kudidimiza au kumuinua mtoto, mategemeo yangu ni kumuinua mtoto kwa malezi bora ili kumjenga kifikra.
Rafiki unatakiwa kujua kwamba, malezi yasipoangaliwa ni chanzo cha fikra hasi ambazo zinapunguza kiwango cha kujitambua kwa mtoto huyo.
Na ikumbukwe endapo mtoto akaharibika ni sawa na jamii nzima imeharibika, kwani mtoto wa leo hii ndilo taifa la kesho. Swali je tunatengeneza taifa gani la kesho mimi na wewe?
Nini Kifanyike?
Kwa mtu ambaye ameshaathirika tayari na malezi na ameshindwa kabisa kutambua umuhimu wake, thamani yake pamoja na utu wake hana budi kuwasamehe wazazi/walezi wake kwanza.
Baada ya kufanya hivyo hana budi kutambua kuwa fikra hasi ni imani potofu juu yake, na huenda ndicho kimekuwa chanzo cha yeye kupoteza utambulisho wake.
Kwa mantiki hiyo wajibu wake mkubwa uwe ni kufuta hizo fikra potofu ambazo zilichangiwa na wazazi/walezi wake.
Ili kufuta fikra hasi kwa urahisi mtu huyo hana budi atumie kanuni ya ubadala yaani abadlilishe fikra hasi kwa kupandikiza fikra chanya akilini mwake.
Mbali na hilo hana budi kubadilisha mitizamo yake juu yake, kwa kujiona mwenye uwezo, mwenye thamani, mwenye nguvu, mwenye akili, mwerevu na mdadisi. Mwisho namkumbusha kuwa maisha ni kusudi hivyo atambue kuwa ana kusudi la kutimiza.
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji, Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment