Fahamu Jinsi Mfumo Wa Elimu Unavyoweza Kumtengeneza Mwanadamu Kifikra...
Kanuni ya kinachoingia na kinachotoka inasema " kinachotoka huakisi kilichoingia"
Kwa mantiki hiyo kama kilichoingizwa kwenye ubongo ni cha kijinga, kitakachotoka kitakuwa ni cha kijinga vilevile!
Hii ni kwa sababu ubongo wa mwanadamu hufanya kazi ya kuchakata matokeo na kufanya mambo yatokee, kwa kutumia taarifa zilizoingizwa na kuhifadhiwa ndani yake!
Hata hivyo, enzi za nyuma sana, dunia haikuwa na maendeleo yoyote ya kisayansi na kiteknolojia kama ilivyo sasa, kutokana na hilo watu waliishi kwa kufanya shughuli za kawaida kwa kutegemea mfumo walioukuta.
Hata hivyo mara baada ya ugunduzi wa mashine zilizopelekea kuanzishwa kwa viwanda pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia ukahitajika ujuzi wa aina mbalimbali. Kutokana na hilo elimu ikaanzishwa kwa lengo la kuwaandaa na kupata wafanyakazi ambao wangeweza kuendesha mashine mbalimbali viwandani.
Hata hivyo, mara baada ya wasomi hao tu kuhitimu walipata nafasi za kuajiriwa pamoja na kupewa mishahara mizuri. Hii iliwafanya wayatoe maisha yao yote kwa ajili ya kutumikia ajira zao.
Matokeo yake, wakawalea watoto wao waongoze maisha kwa namna ileile ambayo wazazi hao walifanya! Hali ambayo ikawafanya watoto wao wapelekwe shule, wahitumu na wayatoe maisha yao yote kutumikia ajira. Hata hivyo nao pia wakawakuza watoto wao katika namna ileile!
Kama utakuwa ni mdadisi akilini mwako utakuwa ushapata picha kamili juu ya kilichotokea. Pasipo kipingamizi ni kwamba mfumo ukawa umeanzia hapo na kila mtu akaona kumpeleka mtoto shule ni jambo jema kwa sababu atakuja kuajiriwa.
Matokeo yake wakajikuta wakiacha kile walichokuwa wanakifanya hapo awali wakafokasi kwenye elimu.
Mbali na hilo hata sekta zingine zikajikuta zimeanzisha mfumo wa kuandaa watu watakaouhudumu katika sekta hizo kwa kuwapa mafunzo maalumu kupitia elimu iliyotolewa.
Kwa mantiki hiyo kigezo kilichotumika kupata wafanyakazi katika kitengo fulani kilikuwa ni elimu. Na, hiki ndicho kinachoendelea mpaka wa leo hii.
Hata hivyo ukija barani Afrika utajifunza kitu kikubwa sana. Mababu zetu walikuwa na mifumo tofauti sana ukilinganisha na ile inayofanywa siku za hivi karibuni.
Jambo moja la msingi unalopaswa kujua kuhusu historia ya Afrika ni hili hapa: babu zetu wa kale walikuwa wana roho ya ujasiriamali, hii ni kwa sababu wengi wao walikuwa wawindaji, wakulima, wagema mipira, wahunzi, watengeneza mavazi, wafanya biashara, wavuvi n.k.
Na, hii ndiyo sababu wengi walikuwa wanafanya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa. Kutokana na hilo walijikuta wakiishi vyema na kuwalea watoto wao kwa misingi bora.
Pia barani Afrika elimu iliyotolewa ililenga zaidi katika kuwafanya watu wajitambue wao ni nani hasa, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha somo la utamaduni wao, hali ambayo iliwafanya waijue asili yao vizuri!
Ukiachilia mbali hilo, vilevile elimu iliyotolewa iliendana na mazingira ambayo watu hao waliishi.
Kwa mfano kama eneo lako limezungukwa na maji utafundishwa na namna ya kuvua, kama kuna ardhi yenye rutuba utafundishwa namna ya kuzalisha mazao, kama ni jamii za wafugaji utafundishwa namna ya kufuga n.k.
Hii inamaanisha kuwa; waafrika hawakuandaa watoto wao waje waajiriwe, bali waliwaandaa ili wajiajiri kupitia shughuli zao pamoja na kuwafundisha jinsi ya kufanya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa.
Baada ya hapo wakaja wakoloni, na walipofika wakaua ile roho ya ujasiriamali ya waafrika kuwa watafutaji.
Wakaanzisha elimu ya kikoloni ambayo iliwaandaa waafrika kuwa wasomi, baada ya hapo wakapewa kazi nzuri na mishahara mizuri pamoja na kuwaahidiwa kupewa pensheni pindi wakistaafu!
Matokeo yake waafrika wakaona kuwa elimu ni kitu chema, wakaanza kuwapeleka watoto wao kwenda shule ili waje wapate ajira na hiki ndicho kinachoendelea mpaka leo hii.
Jambo hili limedumu kizazi hadi kizazi, yaani tumelipokea, tunalidumisha na litapokelewa na kizazi kijacho n.k.
Kutokana na hilo waafrika tunazidi kupoteza asili zetu kwa sababu hatufanyi mambo ya asili yaliyofanywa na babu zetu, bali tumezidi kudumisha taratibu na tamaduni zingine kabisa tulizozipokea kutoka nje.
Funzo moja tunalopaswa kuondoka nalo hapa ni hili, mkataa kwao ni mtumwa. Tumekuwa watumwa kwani mifumo hii imetuathiri kimawazo, kifikra na kimtizamo.
Hii inamaanisha wengi wetu tumejikuta tukionesha mwitikio mzuri wa kuwapeleka watoto wetu shule kwa kile tunachodai kwamba watakuja: kupata ajira serikalini, kuishi maisha mazuri, kupata ulinzi serikalini pamoja na kupata pensheni mara baada ya kustaafu.
Hali hii inatufanya tuue uwezo asilia kwa sababu tunawafanya watoto wetu waamini katika ajira zaidi na siyo kutumia uwezo wao katika kuishi kwao.
Mbali na hilo ukichimba ndani zaidi utagundua kwamba mfumo huu umekuwa ukiwaandaa wanafunzi kwa kuwafundisha masuala yasiyo halisi hasa ukilinganisha na dunia ya sasa, inayokua kwa kasi na kuendelea kisayansi na kiteknolojia.
Kadhalika mfumo huu umekuwa ukiwaandaa wasomi wawe tegemezi katika ajira tu na siyo kumfungua msomi kifikra, kiakili kimawazo, kimtizamo ili ajijue yeye ni nani na anaweza akafanya nini.
Hii inamaanisha mtu kichwani mwake anakuwa anawaza tu ajira muda wote na siyo kuwaza anaweza akafanya nini.
Hitimisho kama unatengenezwa kuja kuwa mtu fulani maana yake huwezi ukajijua wewe ni nani na unaweza ukafanya nini.
Bali utajijua wewe ni yule uliyetengenezwa tu. Na, ndiyo maana unaweza ukakutana na msomi au mhitimu hata wa shule ya msingi ambaye ana uwezo mkubwa sana ndani yake, lakini anashindwa kutumia uwezo huo kwa kile ambacho anadai kuwa hawezi, kwa sababu mifumo haijamuonesha kama anaweza akafanya hivyo.
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184339 au tembelea blog yangu kwa kuandika: ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment