Fahamu Kuhusu Mifumo Ambayo Humtengeneza Mwanadamu...

Kwa tafsiri nyepesi mifumo inaweza kufafanuliwa kama, ni taratibu/njia/miongozo ambayo hutawala, huongoza au husimamia utendekaji wa jambo Fulani kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake. (Yaani matokeo yake).

Hii ni sawa na kusema mifumo hutawala jambo Fulani kutoka kuanza kwake hadi kukamilika kwake. 

Kwa mfano tokea umezaliwa kuna mifumo Fulani ambayo uliingizwa nayo, ambayo imekuwa ikikuongoza, ikikutawala na kukusimamia hadi imekufanya umekuwa hivyo ulivyo. 

Na, unaiona dunia kwa namna hiyo, kwa sababu kichwani mwako kuna taarifa zimeingizwa zinazokufanya uitafsiri dunia pamoja na vitu vilivyomo kwa namna hiyo. 

Hata hivyo, katika ulimwengu wa saikolojia kuna kitu kinaitwa archetypes, hii ni mifumo Fulani ambayo ambayo humfanya mtu awe vile alivyo. Mifumo hii huwa ni jumla ya tabia zote ulizonazo yaani utambulisho wako! 

Hii inamaanisha kwamba, mara baada ya kulelewa nayo kwa muda mrefu umejikuta ukianza hadi kutambulishwa kupitia mifumo hiyo. Na huenda usingepitishwa kwenye mifumo hiyo usingetambulika hivyo. 

Cha kuchukua hapa ni kwamba, unatambulika hivyo na unaonekana hivyo kwa sababu kuna mifumo ambayo imekutengeneza uwe hivyo ulivyo!

Ukweli ni kwamba umetengenezwa mpaka ukawa hivyo ulivyo, mbali na kuwa uliumbwa na Muumba!

Na pengine labda, umekuwa unasitasita katika kufanya maamuzi kwa kuona: huwezi kufanya jambo Fulani, huwezi kubadili maisha yako pamoja na kudhani kuwa hapo ulipo ndiyo mwisho wako!

Ndugu jambo moja ambalo unapaswa kujua ni kwamba kuna mifumo Fulani ambayo imekufanya ujione hivyo na uone dunia kwa namna hiyo.  

Je Ni Mifumo Ipi Ambayo Humtengeneza Na Kumtambulisha Binadamu?

Ipo mifumo mingi sana ambayo humfanya binadamu awe vile alivyo. Hivyo basi kutokana na uhaba wa nafasi nitafafanua mifumo michache tu kwa uweledi na ufasaha uliotukuka. Ifuatayo ni mifumo hiyo:

1. Mazingira 
Ni nguvu isiyoonekana inayomtawala binadamu kuanzia fikra zake, matendo yake, mawazo yake, tabia zake, mienendo yake pamoja na mitizamo yake kwa ujumla. Hii ni sawa na kusema kuna baadhi ya mambo unajiona huwezi kuyafanya kwa vile mazingira uliyopo hayajaandaa mifumo rafiki inayokusaidia ufanikishe mambo hayo!

Ukweli ni kwamba, mfumo huu umetengeneza wale watu ambao wanaona hakuna kitu wanaweza wakabadili maishani mwao. Hawa ni wale watu ambao hujiona hawastahili, hawawezi, hawatafika popote pale, pamoja na kuona ni kama wamefikia ukomo wa maisha yao. 

Ukichimba kwa undani zaidi utagundua kwamba suala hili linachangiwa na athari za mazingira yanayowazunguka watu hao. Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba ni ngumu sana kufanya jambo litakaloenda mbali zaidi ya mazingira uliyopo. 

Kutokana na athari za kimazingira watu wengi hubaki wakiwa na fikra mgando, hali ambayo huwafanya washindwe kubadili maisha yao!

Hebu tumia hata dakika moja tu kuchunguza maisha yako kwa undani, endapo utafanya hivyo utagundua kwamba, kuna baadhi ya vitu unavifanya na vingine unashindwa kuvifanya kutokana mazingira uliyopo. 

Mbali na hilo kuna wakati unawiwa kufanya baadhi ya vitu ili ubadili maisha yako, lakini unasikia mazingira yanakuambia hivyo havitawezekana kabisa, ilihali uwezo na nia ya kuvibadilisha unao.

Kutokana na hilo unajikuta ukishindwa kwa sababu mazingira yanayokuzunguka siyo rafiki.

Kitu unachopaswa kujua ni kwamba mazingira yanaweza kukujengea fikra za uhaba mpaka ukaona hapa duniani hakuna kitu unaweza ukakifanya na hutokaa ufanikiwe. 

Kwa mfano athari za mazingira ya kijijini ni tofauti na atahari za mazingira ya mjini. Vilevile athari za mazingira ya Afrika ni tofauti kabisa na athari za mazingira ya ulaya. 

Hii inamaanisha mazingira yanaweza kukudunisha sana kiasi kwamba ukajiona wewe siyo kitu. Habari za kusikitisha zaidi ni kwamba, huwezi ukachagua sehemu ya kuzaliwa. Na hukuandika barua ili uzaliwe hapo ulipozaliwa bali ulijikuta tu upo duniani!

Rafiki, usinielewe vibaya tafadhali; sina maana kwamba mazingira yanaishia vijijini, mijini na ulaya tu. Huo ulikuwa ni mfano tu. Haijalishi utakuwa wapi lakini athari za mazingira hutazikwepa. 

Kwa mfano mazingira unayoishi yamekuathiri, mazingira uliyosomea yamekuathiri, mazingira unayofanyia kazi yamekuathiri, mazingira unayosali pamoja na mazingira unayoshinda kila siku yamekuathiri. Kwa ujumla naweza kusema; mazingira hayo Yote yamechangia katika kukutengeneza na kukufanya uwe hivyo ulivyo!

Na, kama unataka uthibitisho ni kiasi gani mazingira humuathiri mwanadamu angalia kisa kifuatacho cha Papa! 

Endapo utamchukua papa ukamuweka kwenye chumba kidogo hawezi akakua zaidi ya chumba hicho, atabaki kuwa mdogo ili kulandana na ukubwa wa chumba hicho.

Lakini ukimchukua Papa huyohuyo ukamuweka baharini, atakuwa mkubwa sana kiasi cha kukustaajabisha, hii ni kwa sababu mazingira ya baharini hayajampa papa ukomo wa kukua. 

Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yako, kwamba kuna wakati unajiona mdogo kwa sababu mazingira uliyopo yamekupa ukomo wa kukua!

 Hii ni sawa na kusema, mazingira uliyopo yanaweza kukufanya uwe mdogo ilihali ndani yako una kitu kikubwa sana. 

Na, endapo ikitokea ukaenda mazingira mengine yaliyojaa utele utashangaa ule ukubwa wako ukidhihirika. Hivyo basi kuna wakati unaona huwezi kubadili jambo fulani, si kwa sababu huwezi bali mazingira uliyopo hayakupi hamasa na shauku ya kutosha ya wewe kufanya hivyo.

Kwa ujumla kuna wakati unajiona hakuna kitu unaweza kubadili maishani mwako kwa sababu ya mfumo wa mazingira uliyopo yamekutengeneza uone hivyo. Habari mbaya ni kwamba huwezi ukafanya kitu kikaenda mbali na mazingira uliyopo. 

Hivyo basi kuna vitu vingine ili uvifanye itakubidi utoke nje ya mazingira uliyopo sasa. Na, usipoweza kutoka mifumo iliyopo kwenye mazingira itaendelea kukupa matokeo hayohayo na hakuna kitu utabadili maishani mwako. 

Rafiki kuna wakati inakubidi utoke kwenye mazingira uliyopo kwanza! Kama unatakiwa utoke, huna budi kutoka! Kumbuka wewe siyo mti kwamba ulipandwa ubaki hapo ulipo tu!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...