Je, Unataka Kudumu Katika Kufanya Tabia Nzuri Muda Wote! Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...
Ukweli mchungu ni kwamba tabia mbaya ni rahisi kuzitengeneza lakini ni ngumu kuishi nazo, ikiwa tabia nzuri ni ngumu kuzitengeneza lakini ni rahisi kuishi nazo...
Unatakiwa kujua kwamba kila tabia unayoifanya ni kisababishi cha matokeo fulani miaka kadhaa ijayo...
Na, matokeo hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Hata hivyo uzuri au ubaya wa matokeo hayo utategemeana na aina ya tabia utakayoifanya!
Rafiki unatakiwa kuweka akilini mwako kwamba, ukiweza kufanya baadhi ya tabia ndani ya kipindi fulani cha muda zitakutengenezea utambulisho.
Na kwa vile somo hili linazungumzia jinsi ya kudumu na tabia nzuri muda wote, basi endapo utadumu katika kufanya tabia hizo utadumu katika utambulisho ulio mzuri!
Ndugu, unaalikwa kuhakikisha kwamba unadumu katika kufanya tabia nzuri tu, ili zikusaidie katika kukufanya ubaki katika utambulisho ulionao, pamoja na kuendelea kupata matokeo mazuri ambayo umekuwa ukiyapata muda wote!
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba mafanikio siyo lengo la kulifikia, na kwamba ukilifikia ni mwisho bali ni mchakato endelevu wa kujiboresha usio na ukomo.
Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba kila kitendo unachofanya kinatawaliwa na tabia Fulani.
Kwa mantiki hiyo ili kuweza kufanya tabia nzuri na kuepuka kabisa tabia hatarishi huna budi udumu kuwa mtu chanya muda wote!
Habari njema ni kwamba, ukiweza kudumu katika kufanya tabia bora muda wote, hutoweza kabisa kufanya kitendo kiovu ambacho hakilandani na tabia zako!
Rafiki unatakiwa kujua kwamba, zitafika baadhi ya nyakati utajikuta hujisikii kufanya chochote kile; huku ukikutana na ugumu wa kukumbuka kufanya baadhi ya tabia ambazo zilikuwa zinakuletea matokeo chanya, utakachotakiwa kufanya ni kuziorodhesha tabia hizo upya; ili zikuvutie zaidi hali itakayokufanya uendelee kuzifanya tabia hizo.
Pia zitafika nyakati utajikuta, unapata ugumu katika kufanya baadhi ya tabia, unachopaswa kufanya ni kuweka urahisi katika kuitikia kufanya tabia hizo.
Mbali na hilo zitafika nyakati utajikuta hauna kabisa hamasa au motisha ya kuendelea kufanya tabia hizo, utakachopaswa kufanya hapo ni kuyafanya matokeo ya tabia hizo yakuridhishe.
Hiyo ndiyo siri ya kutengeneza matokeo yanayodumu.
Zunguka uwezavyo fanya yote lakini ukiweza kudumu katika kufanya kanuni hizo tatu ni lazima utapata matokeo yanayodumu maishani mwako.
Unatakiwa kujua kwamba siri ya kutengeneza matokeo yanayodumu ipo kwenye kujiboresha.
Fanya tabia zako zipatikane mazingira uliyopo , ili zikuvutie, weka urahisi katika kuitikia kuzifanya pamoja na kufanya matokeo yake yaweze kukuridhisha.
Ukiweza kufanya hivyo lazima utapata matokeo yanayodumu nawe hutofanya tena tabia hatarishi!
Hata hivyo unaweza kudumu katika kufanya tabia nzuri kwa kufanya jambo lifuatalo.
1. Saini Mkataba Wa Tabia (habit contract)...
Mbinu hii huhitaji watu wawili: yaani yule anayetaka kufanya tabia Fulani, pamoja na yule mtu atakayekuwa anamsimamia na kuhakikisha kuwa tabia hiyo inafanywa!
Kwa mfano unaweza kusema...
Mimi ___________ (weka jina lako), "ninataka niwe nafanya tabia ya kutumia muda wangu vizuri pamoja na kutekeleza mipango yangu yote pasipo kughairisha"
Endapo sitofanya tabia tajwa ninaahidi kumtumia mwalimu wangu 100,000/= kama adhabu ya kutokufanya tabia hizo ilihali nimeahidi kuzifanya!
Baada ya hapo wewe na msimamizi wako mtausaini mkataba huo tayari kwa ajili ya kuanza utekelezaji!
Unatakiwa uwe mwaminifu na mkweli kwako wewe mwenyewe, endapo itatokea hujafanya uwe muwazi na uwe tayari kulipa faini ili ikuume, na ukishaumia hutarudia tena kufanya kosa!
Kutokana na hilo utajikuta unakuwa ni mtu mwenye nidhamu ya kiwango cha juu, kwa sababu kuna mtu wa kukuadabisha endapo utafanya kinyume na yale uliyoahidi kuyafanya!
Rafiki, kama unataka ubadlishe tabia zako wasiliana nami ili niwe nakuadabisha, nakuahidi baada ya miezi mitatu utakuwa ni mtu mwingine kabisa!
2. Tumia mbinu ya kikumbushio yaani: baada ya______ tabia mpya_____eneo itakayofanyika_______
Kwa mfano baada ya kuamka Sasa 11 alfajiri nitasoma kitabu katika chumba changu cha maktaba.
Au...
Baada ya kumaliza kipindi na mwalimu wangu saa 12 jioni nitaenda zoezini kwenye uwanja wa mpira wa miguu.
Au...
Nikishaamka tu kesho saa 11 alfajiri nitapangilia ratiba ya siku nzima nikiwa chumbani mwangu.
Rafiki unatakiwa kujua kuwa ni lazima udokeze tabia unayotaka kufanya, muda utakaofanya pamoja na eneo utakalotumia kufanya tabia hiyo.
Endapo utaweza kutumia mbinu hii kwa muda wote utajikuta ukifanya zile tabia ambazo unataka kuzifanya tu, kwa mantiki hiyo hutapata upenyo mwingine wa kufanya tabia ambazo huzitaki.
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment