Sababu Kuu Tano Za Kwanini Unatakiwa Usome ujumbe Huu Ikiwa Ni Mwanzo Kabisa Wa Mwaka...

Habari yako rafiki yangu! Karibu kwenye mwendelezo wa makala nyingine inayochambua kuhusu mambo ya msingi, unayotakiwa uyafahamu pamoja na kuyaishi kwa mwaka 2024 ili ubadili maisha yako!

Jana lilidokezwa jambo moja tu, kwa leo utaenda kudokezewa mambo mengine matano ya msingi unayopaswa uyafahamu na kuyaishi! 
Mambo hayo ni kama ifuatavyo:-

1. Unaweza Kuwa Yeyote Yule...
Umekuwa hivyo ulivyo siyo kwa sababu ulipaswa uwe hivyo. Bali umekuwa hivyo kwa sababu kuna mifumo iliyokutengeneza na kukufanya uwe hivyo ulivyo. 

Hii ni sawa kusema endapo utaamua, unaweza kuwa yeyote yule unayetaka uwe na hakuna mtu wa kukuzuia.

Rafiki, dunia ni mali yako, kuwa unachotaka! Hutakiwi kufungwa na utambulisho wa kutengenezewa tena, badala yake sasa unaweza ukajitengenezea utambulisho wako mwenyewe, na kuwa yule unayetaka uwe...

Unatakiwa kujua kwamba, hakuna kitu kitakachokusimamisha kuwa yule uliyeamua uwe.

Leo hii huenda ukawa unatambulika kwa sababu ya kozi uliyosomea au kwa sababu ya kazi unayoifanya. Unachopaswa kujua ni kwamba, unaweza ukawa mtu mwingine kabisa endapo utaamua kubadilisha utambulisho wako.

Ndugu, hakuna mtu ambaye huzaliwa akiwa hawezi au hastahili. Ukweli ni kwamba sote huja duniani tukiwa sawa, yaani: tukiwa uchi, wajinga, wenye kuogopa huku tukiwa hatujui kitu, lakini huwa tunaishia kupata matokeo tafauti katika maisha kutokana na maamuzi tunayoyafanya juu ya wale tunaotaka tuwe!

Je, unataka kuwa nani? Je, utafanya nini ili kuhakikisha unakuwa huyo unayetaka uwe? 

Rafiki, unatakiwa kujua kwamba watu wakuu huamini katika; “vichocheo na matokeo, ikiwa watu wa kawaida huamini katika bahati”.

Hutakiwi kuamini katika bahati, amini katika vichocheo na matokeo. 

Kwa mfano kama unataka kubadili maisha yako lazima uorodheshe ni aina gani ya matokeo unayoyataka, baada ya hapo tafuta vichocheo vitakavyopelekea matokeo hayo!

2. Umefika Hapo Ulipo Na Umekuwa Hivyo Ulivyo Kutokana Na Wewe Mwenyewe...

Hakuna aliyekupangia uwe hivyo ulivyo, ufike hapo ulipo, utengeneze hicho kipato unachoingiza, ufanye hiyo kazi unayofanya, uishi hapo unapoishi, uishi maisha ya hadhi hiyo unayoyaishi, uwe na huyo mwenzi uliyenaye pamoja na kila unachokifanya maishani mwako, pasipo uhusika wako mwenyewe!

Na, kama hukusika moja kwa moja katika kuamua, basi kuna mtu alikuamulia, na kwa vile hukuwa na chaguo lingine, ukakubali iwe hivyo, usijue matokeo yake yatakujaje. Mwisho wa siku umejikuta ukifika hapo ulipo na kuwa hivyo ulivyo! Rafiki, hata usishangae huko ndiko kunaitwa; “kuvuna ulichopanda”

Mwaka 2024 usimlaumu mtu wala usijialaumu! Badala yake sasa ukiona kuna pito au hali unapitia na huielewi vizuri, jiulize swali hili; “mimi nimehusikaje katika kusababisha hali hii au pito hili ninalopitia?”

Baada ya hapo sasa rudi kwenye visababishi vilivyopelekea hali hizo, halafu uviondoe, hapo ndipo utakuwa umeshabadili hali za mapito yako.

Rafiki, hayo ni maisha yako, halafu wewe ndiye inchaji wa kila kipengele kinachohusu maisha yako. 

Kwa hiyo kwa chochote kile kitakachotokea huna budi kutambua kwamba una wajibu wa kukiondoa. Kumbuka usipofanya hivyo hakuna atakayefanya hivyo kwa niaba yako!

3. Marafiki Ni Kama Ngazi Wanaweza Kukupandisha Ama Kukushusha...

Dokta David McClelland alifanya tafiti moja iliyotumia takribani miaka ishirini na tano (25). Katika kuhitimisha tafiti yake aliandika hivi; “watu unaoshinda nao wana uwezo wa kukufanya ufanikiwe au ushindwe maishani mwako”

Hata hivyo kwa mujibu wa tafiti nyingi za kisaikolojia kuwahi kufanyika zimeonesha kwamba, watu wengi hupata mabadiliko mazuri au mabaya maishani mwao kutokana na aina ya marafiki wanaokuwa nao!

Unajua ni kwanini? …hii ni kwa sababu akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine, hata hivyo akili yako hukusukuma uendane na wengine ili uweze kukubalika kwenye kundi unalochangamana nalo. 

Na, ndiyo maana kuna baadhi ya watu hujikuta wanakuwa walevi kwa sababu ya kutumia pombe, kama njia ya kukubalika kwenye kundi wanalochangamana nalo, matokeo yake hujikuta washakuwa walevi wa kupindukia! 

Rafiki, wahenga hawakuwa wapumbavu mpaka wakasema; “ndege wanaofanana huruka pamoja”, mimi simkatazi mtu asiwe na marafiki, lakini mtu mwenyewe lazima uangalie athari za marafiki hao maishani mwako! 

Ndugu, marafiki ni kama ngazi! Kumbuka wanaweza kukupandisha ama kukushusha! Kupandishwa au kushushwa kutatagemeana na marafiki unaowachagua uchangamane nao!

JAMBO KUU LA KUEPUKA 2024: epuka kushinda masaa matatu na mtu wa kushinda naye dakika tatu, epuka kushinda siku tatu na mtu wa kushinda naye masaa matatu, epuka kushinda wiki na mtu wa kushinda naye masaa saba, mwisho epuka KABISA kushinda mwaka mzima na mtu wa kushinda naye siku thelathini.

4. Maisha Pasipo Malengo Ni Sawa Na Mtumbwi Unaoelea Pasipo Mvushaji...

Kuishi pasipo malengo ni sawa na kuanza safari pasipo kujua hatima ya safari yako. Kibaya Zaidi ni kwamba, huwezi kujua kama umefika hata kama utakuwa umefika, ikiwa hujui hatima ya safari yako!

Watu wengi wapo safarini, lakini hawajui wanakoenda ni wapi, kutokana na hilo hujikuta wakiongozwa na kila njia, wakidhani watafika kule wanakoenda, kumbe njia hizo haziwafikishi kule wanakoenda, matokeo yake huishia kutokufika popote pale kimaisha. Rafiki, unatakiwa kujua kwamba; “kama hujui unakoenda kila njia itakuongoza”

Ndugu, huwezi kufikia lengo, kama hujaazimia lengo! Ni lazima uanze kwanza kuazimia malengo, halafu ufanye utekelezaji mwisho wa siku uatapata matokeo unayoyataka! 

Je, una malengo yoyote uliyoyapanga kuyatekeleza 2024 au na wewe unaamini ile falsafa isemayo; “liwalo na liwe?”

Rafiki, hakuna liwalo na liwe kwenye maisha, kwa maana hauishi ili kufanya majaribio, kumbuka maisha siyo majaribio bali maisha ni kuishi! 

Na, utaishi ukamilifu wa maisha yako siku utakayoamua kuazimia malengo mbalimbali kuhusu maisha yako yajayo! 

Rafiki, unatakiwa uandike malengo yako kwa lugha ya uwazi, huku ukidokeza na ukomo wa muda, yaani ni lini unataka malengo hayo yatimie! Unatakiwa kujua kwamba lengo huwa ni nia/kusudio/tarajio aliwekalo mtu ndani ya muda Fulani. 

Hii ni sawa kusema, mtu mwenye malengo huyafanya maisha yake yawe na kusudi Fulani. Kwa mantiki hiyo, mtu huyo hataishi tu kwa sababu yuko hai, bali ataishi kwa sababu kuna mambo yanayompa sababu ya yeye kuishi! 

Je, unajua hatima ya maisha yako baada ya miaka mitano itakuwaje? Je, unajua kule unakoelekea? Je, unajua ni kipi unachokitaka katika maisha yako? 

Ndugu, kila jambo linawezekana, unachopaswa kufanya ni kuazimia malengo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kudokeza njia utakazotumia ili kufanikisha malengo hayo, pasipo kusahau kufanya utekelezaji ili kufikia hatima nzuri ya malengo yako. 

Kumbuka hakuna lengo ambalo hujitekeleza lenyewe, kwa maana kuazimia lengo ni kitu kingine na kufanikisha lengo ni kitu kingine!

5. Watu Watakuwa Tayari Kukulipa Endapo Utatengeneza Thamani...

Rafiki, kama unataka fedha, unatakiwa kujua kwamba fedha ipo mifukoni mwa watu, wala haipo benki kama wengi mnavyodhani, kwa maana hata benki haimiliki pesa, bali benki ipo pale ili kuhifadhi fedha zinazomilikiwa na watu.

Sasa ili kuwafanya watu wakupe fedha, lazima utafute sababu itakayowafanya watu hao watoe fedha mfukoni mwako ili wakulipe! 

Na kama hakuna thamani unayotengeneza, maana yake huna sababu inayowafanya watu hao watoe fedha zao ili wakulipe. Ikumbukwe fedha ni mbadilishano wa thamani.

Na ikiwa fedha ni mbadilishano wa thamani maana yake, watu watatumia fedha zao ili kubadilishana na vitu wanavyovithamini, sasa kama huna thamani unayoitengeneza, huwezi ukalamba hata mia mbovu!

Mwaka 2024 jitahidi kuwa mtu unayetengeneza thamani, jaribu kufikiri ni kitu gani unachoweza kufanya kitakachowafanya watu watoe fedha ili wabadilishane na thamani inayotokana na kitu hicho!

Rafiki, unatakiwa kujua kwamba endapo utabaki kuwa mtu ambaye huna thamani unayotengeneza, huwezi kukuza pato lako.

Narudia Tena kwa msisitizo; "fedha ipo mifukoni mwa watu, lakini ili kuipata lazima uwape watu sababu itakayowafanya watoe fedha zao mifukoni mwao ili wakulipe"

Nimeona nikukumbushe hayo machache kwa mwaka 2024 ewe rafiki yangu kipenzi.

Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0744284329/0673184329 Au Tembelea Blog Yangu Kwa Kuandika; ekingunge.blogspot.com

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...