Umekuwa Hivyo Ulivyo Kutokana Na Aina Ya Marafiki Ulioamua Kuwa Nao...
Kwa mujibu wa tafiti za kisaikolojia kuwahi kufanyika zimeonesha kwamba, akili ya binadamu inajua jinsi ya kuendana na wengine.
Kutokana na dai hilo unatakiwa ukubali ukweli huo ya kwamba, hata akili yako inajua jinsi ya kuendana na watu wengine.
Hii ni sawa kusema kuwa, huwezi ukafanya kitu kitakachokuwa tofauti na kile ambacho marafiki zako wanakifanya!
Na, hii ni kwa sababu hautafanya mambo kwa sababu unatakiwa kufanya bali utajikuta ukifanya baadhi ya mambo kwa sababu watu wako wa karibu wanayafanya!
Nioneshe watu wako wa karibu nami nitakwambia wewe ni nani. Msemo huu unamaanisha kuwa, watu unaoshinda nao muda wote ni utambulisho tosha kabisa kuhusu wewe ni nani hasa.
Jambo moja unalotakiwa kuondoka nalo hapa ni kwamba, utajikuta ukitengenezwa automatiki kwa kuitikia na kufanya kile ambacho watu wako wa karibu wanakifanya.
Na, itakuwa ngumu sana kwako kutokufanya kile ambacho watu wako wa karibu wanakifanya.
Hata hivyo, madai yenye mashiko ya kisaikolojia yameonesha kwamba kila binadamu hujifunza kwa kuiga na kufanya kile kinachofanywa na wengine.
Hii ni sawa na kusema, utajikuta ukiiga kwa kufanya tabia, matendo pamoja na masula mbalimbali kutoka kwa marafiki zako unaoshinda nao.
Unaweza ukawa unajiuliza, kwanini sasa akili yako huwa inatafuta kuendana na wengine?
Ndiyo upo sahihi... ni kwa sababu akili yako huwa inakutengenezea mazingira ya wewe kukubalika na hao watu unaochangamana nao! Pasipo kujali kipi kitatokea kutokana na hicho utakachokifanya ili ukubalike na marafiki zako!
Unachotakiwa kuchuka hapa ni kwamba unapoamua kushinda na watu fulani maana yake upo tayari kufuata taratibu, kanuni na sheria ambazo zitakuwa zinatawala uhusiano wenu.
Kutokana na hilo utajikuta unaanza kupoteza ule upekee wako kwa vile unakuwa umeruhusu mfumo unaotoka nje kutoka kwa marafiki uweze kukutawala, kukuongoza na kukusimamia.
Matokeo yake utajikuta unaanza kutengenezwa na kuwa sawa kabisa na wale watu unaoshinda nao kila siku.
Na, ndiyo maana wahenga walisema; “ndege wanaofanana huruka pamoja”. Kitu unachopaswa kujifunza kutoka kwa msemo huo wa wahenga ni kwamba, watu unaowachagua kushinda nao maana yake mnaendana nao kitabia pamoja na kimienendo.
Unatakiwa kujua kwamba kuna watu wamejikuta wakishindwa kubadili maisha yao, wanafeli katika mipango yao, wanabadili mtindo wako wa kuishi, wanaangukia pabaya pamoja na kubadili mpaka tabia zao kutokana na marafiki.
Mbali na hilo unatakiwa kufahamu kwamba marafiki wanaweza kukujenga ama kukubomoa. Kujengwa ama kubomolewa kutategemeana na mifumo inayotawala mahusiano yenu.
Kubali usikatae kuna wakati utajikuta ukifanya tabia fulani ili kuwaridhisha marafiki zako.
Mbali na hilo kuna baadhi ya marafiki wanaweza kugusa maisha yako na kubadili kabisa maisha yako!
Jambo moja unalopaswa kufanya katika maisha yako hakikisha kwamba 60% ya watu wa karibu wamekuzidi kiuwezo, kiakili na kimaendeleo, kwa mantiki hiyo watakuhamasisha Zaidi na kukufanya na wewe uwe kama wao.
Ukiachilia hilo hakikisha 30% ya watu wako wa karibu ni watu ambao mpo kwenye kiwango sawa kimaisha, watu hawa mtashirikiana katika kupanga mipango kimaisha pamoja na kufuatiliana maendeleo yenu. Watu hawa wanaweza kuwa wafanyakazi wenzako, marafiki zako wanafunzi wenzako n.k, watu hawa wanakuwa ni watu wa kawida tu.
Mwisho kabisa hakikisha 10% ya watu wako wa karibu ni watu uliowazidi kimafanikio, kimaendeleo, kiuchumi na kiakili. Watu hawa hawapaswi kuwa wengi sana kwa sababu kiufupi ni watu ambao watakuwa wanakutegemea sana wewe.
Hata hivyo endapo watu hawa watakuwa wengi sana watanyonya nguvu zako na kukufanya uchoke haraka sana. Mbali na hilo watu hawa watakupa hamasa na kuchochea juhudi zako kwa sababu utakuwa unafanya juhudi nyingi kwa ajili yao.
Kwa ujumla mafanikio maishani mwako, pamoja na kesho nzuri imebebwa na watu wako wa karibu. Namaanisha watu wanaokujua pamoja na unaowajua ndiyo wamebeba mafanikio yako.
Unachoposwa kujua ni kwamba watu hawa watakushirikisha taarifa, njia, na mawazo mbalimbali ambayo yataingia ubongoni mwako.
Daima chagua watu hawa kwa umakini, tena ikibidi chagua ambao walishafanikiwa ili na wewe utumie mifumo iliyopelekea mafanikio yao.
Kumbuka endapo utafanya kile ambacho watu waliofanikiwa walikifanya, kwa namna ileile kama wao walivyofanya nawe utapata matokeo kama yao!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment