Je, Siku Kuu Ya Krismasi Inatambuliwa Kwa Mujibu Wa Maandiko Matakatifu?...


Bila shaka ulishawahi kujiuliza kwanini tarehe 25 disemba ilitengwa iwe ndiyo sikukuu ya krismasi, yaani iwe siku maalumu kwa ajili ya kusheherekea kumbukizi la kuzaliwa kwake Yesu, na huenda mbali na kujiuliza hivyo hukupata jibu. Na kama hujawahi kujiuliza basi leo tuuangalie uhalali wa maadhimisho ya siku kuu hii! 

Angalizo: Sipingani na Imani ya mtu na wala sitaki mtu aachane na imani yake, hata hivyo sikulazimishi uamini kile ninachokiamini mimi. Lengo langu ni kuleta mjadala utakaoibua mtizamo mpya kuhusu mahusiano ya tarehe 25 disemba na kuzaliwa kwake Yesu! 

Ukweli ni kwamba hakuna andiko lolote lililotuamuru tufanye kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu tarehe 25 Disemba kila mwaka! Na kama hakuna andiko maana yake siku hii iliamriwa tu na mwanadamu mwenyewe. 

Na ikiwa mwanadamu ndiye aliyeitenga tarehe hii, maana yake Mungu hayatambui maadhimisho haya. Ninasema Mungu hayatambui maadhimisho haya kwa sababu hakuna sehemu kwenye maandiko yake ambayo katuamuru tufanye!

Naona unashtuka na unajiuliza hivi huyu kijana anapingana na kile wakristo wanakifanya? Lahasha! Sipo kinyume na ukristo, kwanza mimi mwenyewe ni mkristo pure kabisa! Lakini ukristo hauna mamlaka kuliko Biblia, kwa maana Biblia ndiyo katiba yetu sisi wakristo. Na hakuna mamlaka iliyo kuu Zaidi ya Neno la Mungu yaani (Biblia)!

Mteule unatakiwa kujua kwamba uhalisia wa maisha ya Yesu mwenyewe ulishaandikwa na Manabii. Kwa minajiri hiyo Yesu aliishi sawa sawa na unabii ulioandikwa kumhusu yeye. Na hii ndiyo sababu kubwa ambayo hunifanya mimi nimuamini Yesu kama mesia.

Na, kama Yesu (Mwana wa Mungu) aliishi sawa sawa na maandiko. Maana yake hata sisi tunatakiwa tujifunze kutoka kwake kwa kufanya maisha yetu ya Imani kufuatana na kile maandiko yameamuru tukifanye! 

Na endapo tutafanya mambo ambayo Mungu hajatuamuru maana yake tutakuwa tumependa Zaidi utukufu wa mwanadamu kuliko utukufu wa Mungu. 

Na endapo tutafanya ibada zetu kwa kufuata mapokeo na maagizo ya mwanadamu Mungu hatakakuwa na cha kufanya juu ya maadhimisho haya!

Na, ndiyo maana Isaya 29:13, Neno la Mungu linasema; “Bwana akanena, kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya binadamu waliyofundishwa”

Fundisho tunalopaswa kuchukua kwenye andiko hili ni kwamba unaweza ukajua unamwabudu Mungu, kumbe Mungu hayuko pamoja na wewe kwa maana haufanyi mapenzi yake, bali unamtumikia huku ukifanya mapenzi ya binadamu!

Hata hivyo moja ya andiko ambalo linathibitisha kuwa Yesu Kristo aliishi sawa sawa na maandiko ni lile linalopatikana katika injili ya Luka 24:44 ambapo Neno la Mungu linasema; “Kisha akawaambia, haya ndiyo maneno yangu niliyowaambia nikiwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi” 

Hapa tunapata fundisho kwamba hata Yesu mwenyewe hakufanya kila jambo kwa matakwa yake, bali alifanya yote yaliyoandikwa kuhusu yeye kama yalivyoandikwa na manabii ambao walinena yale waliyofunuliwa na Mungu kuhusu nyakati zijazo! 

Na, ndiyo maana kuanzia kuzaliwa kwake Yesu, mahali alipozaliwa, kazi yake, kifo chake na kufufuka kwake vilikuwa ni vitu ambavyo vilishaandikwa, kwa mantiki hiyo Yesu alikuja kuvitimiliza!  

Nabii isaya alishatabiri kwamba kuna mtoto mwanaume atazaliwa na bikira, lakini wakati wa unabii hakutaja tarehe wala mwezi ambao huyo mtoto angezaliwa, hata hivyo nabii Isaya hakumtaja huyo bikira jina lake anaitwa nani.

Isaya 7:14 “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanuel”

Kutokana na unabii huo wa nabii Isaya utimilifu wake ulikuja ukatimia kupitia injili ya Mathayo na hapa ndipo tunapooneshwa jina la huyo bikira aliyetajwa na Isaya alikuwa nani.
Hii ni sawa na kusema, pasipo utimilifu huwezi kuelewa unabii, na ndiyo maana mara baada ya bikira kuchukua mimba ule unabii ulionenwa na nabii Isaya ukatimilika. 

Mathayo 1:18 “Kuzaliwa kwake Yesu kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu. Kabla hawajakariabiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu”

Rafiki, Mwinjili Mathayo anatuonesha jinsi utimilifu wa unabii wa Isaya ulivyoweza kutimizwa kupitia bikira Mariamu. Lakini hapa Biblia haijatuonesha tarehe wala mwezi ambao Yesu alizaliwa, hata hivyo Biblia haijatuamuru tufanye sherehe za kuzaliwa kwa Yesu, na lingekuwa jambo la muhimu bila shaka maandiko yangetuonesha! 

Hata hivyo sote tunajua kwamba Yesu Kristo alikuwa mnazareti, hivi ushawahi kujiuliza ni kwanini alizaliwa Bethlehemu? Unatakiwa kujua kwamba kulikuwa tayari kuna unabii ulioonesha kuwa Yesu atazaliwa Bethlehemu, ngoja nikuoneshe...

Mika 5:2 “Bali wewe Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”

Kumbe Yesu hakuzaliwa Bethlehemu kwa bahati mbaya, bali alizaliwa Bethlehemu ili kutimiliza unabii aliokuwa amefunuliwa nabii Mika.

Je, unataka kujua ilikuwaje mpaka Yesu akajikuta akizaliwa Bethlehemu? Usijali ngoja nikuoneshe.

Luka 2:1-7 “Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda Kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa alipokuwa huko siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”

Umeona jinsi gani Mungu alivyo fundi? Yeye humpa nabii utabiri lakini atakayetimiliza hatajwi ila unabii ukitimia ndiyo tunajua kwamba aliyetimiliza ni nani. 

Kwa mfano amri ya kaisari Augusto ndiyo iliyomfanya Yusufu atoke na mkewe aende Bethlehemu, na alipofika huko, siku za mariamu kuzaa zikafika akazaa akiwa Bethlehemu na hapo ndipo andiko likatimizwa.

Hata hivyo, kukimbilia Misri mara baada ya Yesu kuzaliwa haikutokea kwa bahati mbaya bali ni jambo ambalo lilikuwa lishaandikwa tayari, na ndiyo maana ninasema kila kitu ambacho Yesu alikifanya kilikuwa kimeandikwa.

Ngoja tuone andiko hilo. Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”

Unajua nini, linapokuja suala la Mungu kutimiza unabii huwa hana mchezo, kwa mfano mwinjili Mathayo amelionesha hili katika injili yake, kwamba kuna baadhi ya Watoto waliuawa na Mfalme Herode ili ipatikane sababu ya wao kukumbilia Misri ndipo andiko likatimizwa…

Mathayo 2: 13-16 “Nao walipokwisha Kwenda zao, tazama, Malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko, hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, kutoka Misri nalimwita mwanangu”

Mpaka hapa ni matumaini yangu umeona kwamba Mungu huandaa mazingira ya kila kitu kabla hakijatokea ili kikitokea tupate kuamini unabii, lakini katika haya yote bado hatuoni andiko linalotutaka tufanye maadhimisho ya siku ya krismasi tarehe 25 disemba kila mwaka.

Mbali na hilo ukija kuangalia hata kazi yake Yesu ilishaandikwa tayari katika kitabu cha nabii Isaya.
 
Isaya 61:1 “Roho ya Bwana i juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu Habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, na kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao”

Na utimilifu wake ukawa kwenye injili ya Luka 4:16-21, ambapo Neno la Mungu linasema; “akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, ‘Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao. Na vipofu kupata kuona tena, na kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Kumbe Mungu anaweza kutumia jina la mtu wakati wa unabii, lakini wakati wa utimilifu ndipo tunamuona mtu halisi aliyemaanishwa. Kwa mfano hapa tunaona kwenye unabii Isaya ndiye anatajwa lakini kwenye utimilifu tunakuja kumuona Yesu akitimiza unabii.

Mbali na hilo hata mahali alipoanza kufanya kazi hapakutokea kwa bahati mbaya bali palishaandikwa. 

Isaya 9:1-2 “Hapo kwanza aliingia nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya tukufu, karibu na njia ya Bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokuwa katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza”

Utimilifu wake tunauona kwenye injili ya Mathayo 4:13-16 ambapo neno la Mungu linasema; “Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya, akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani mipakani mwa Zabuloni na Naftali, ili litimie neno liliolenenwa na nabii Isaya, akisema: nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali. Njia ya Bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa; watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti umewazukia”

Rafiki nimekuonesha baadhi ya mambo machache kuhusu kuzaliwa kwa Yesu pamoja na kazi yake, ili ujue kwamba kila kitu alikifanya kama vile kilivyonenwa na manabii wa agano la kale, na hakuna kitu ambacho alikifanya kinyume.

Hata hivyo sote tumeona unabii na utimilifu wa mambo hayo lakini hakuna hata agizo moja linalotutaka sisi tufanye sherehe hii!

Lakini kwanini iwe 25 disemba, kwanini isingekuwa tarehe nyingine na mwezi mwingine? Je, kihistoria ni tukio gani lilikuwa likifanyika tarehe na mwezi huo?

Simkatazi mtu asile pilau, ila maana yangu ni kutaka kujua uhalali wa sikukuu hii. Rafiki kama ulikuwa hujui ni kwamba: Yesu alizaliwa, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka, akapaa mbinguni akaahidi kwamba atakuja tena.

Kwa hiyo ukiwa unaendelea kusheherekea fikiria pia kuhusu ujio wake wa pili, kumbuka katuachia agano ambalo tunatakiwa tulitunze halafu akatuahidi kuwa atarudi tena! 

Mathayo 24:29-30 “Lakini mara baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbingu zitatikisika. Ndipo itaonekana ishara ya mwana wa Adamu mbinguni, ndipo mataifa watakapoomboleza, nao watamwona mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi”

Rafiki, tumia muda wako mwingi kufikiri juu ya ujio wa pili wa Yesu Kristo. Kwa maana, Yesu alishazaliwa na kuishi miaka 2000 iliyopita, ila ile ahadi ya kuja tena itatimilika muda si mrefu, na lazima itatimilika.

Kwanini lazima itatimilika ni kwa sababu Mungu si mwanadamu ambaye huwa hatakelezi ahadi zake, bali yeye hutimiza ahadi zake!

Hesabu 23:19 “Mungu si mtu aseme uongo; wala si mwanadamu, ajute; iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena hatalifikiliza?

Ukweli ni kwamba Yesu atakuja tena, kwa hiyo huna budi kujianda kwa ajili ya ujio wake wa mara ya pili. Hakikisha taa yako inawaka, hakikisha una mafuta ya kutosha, hakikisha una vazi la harusi tayari kwa ajili ya arusi ya mwanakondoo!

Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya mwanakondoo imekuja, na mkewe amajiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi”

Rafiki usifanye jambo pasipo kudadisi, bali fanya jambo hilo kwa sababu unajua kwanini unalifanya, ikiwa ni pamoja na kujua umuhimu wa kufanya jambo hilo!

Zaburi 32:9 “Msiwe kama farasi wala nyumbu, walio hawana akili…”

Bila shaka unataka kumjua Mungu Zaidi pamoja na kujua Neno lake, kama jibu lako ni ndiyo na ungependa kujifunza Biblia, jibu ujumbe huu kwa kuandika neno BIBLIA.

Ubaki na amani ya Bwana, nakutakia wakati mwema!

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...