Je Ushawahi Kujiuliza Juu Ya Haya?
Kwanini mtu mmoja ana furaha ilihali mwingine ana huzuni?
Kwanini mtu mmoja anapona ugonjwa ambao unasadikika hauwezi kuponywa ilihali mwingine haponi?
Kwanini mtu mmoja ana hofu, wasiwasi, hana amani, hana tumaini ilihali mtu mwingine ana furaha, amani na matumaini?
Kwanini mtu mmoja anafanikiwa katika jambo Fulani ilihali mtu mwingine anashindwa kufanikiwa katika jambo hilo?
Kwanini mtu mmoja anafanikiwa kujibiwa katika sala juu ya jambo Fulani ilihali mwingine anashindwa kujibiwa katika jambo hilo?
Kwanini watu wengi wanaosali sana hupitia mitihani, mateso magumu akilini mwao na maishani mwao mwote?
Je, kuna majibu yoyote juu ya haya?
…muda siyo mrefu utaenda kuujua ukweli.
Yohana 8:32 “tena mtaifahamu kweli, na hiyo kweli itawaweka huru”.
Huenda ukawa unapitia nyakati ngumu sana kiasi kwamba umeshakata tamaa na huna tumaini lolote lile…
Na, huenda unapitia hali ngumu kama alivyopitia mwandishi wa Zaburi 6:6, ambapo Neno la Mungu linasema;
“Nimechoka kwa kuugua kwangu,
kila siku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro kwa machozi yangu”
Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye huwa hapitii nyakati ngumu.
Unatakiwa kujua kwamba katika kuishi kwetu kila mtu hupitia nyakati ngumu.
Na, hakuna mtu mwenye furaha asilimia mia moja vilevile hakuna mtu mwenye huzuni asilimia mia moja.
Hii ni sawa na kusema maisha tunayoishi hapa duniani ni mbadilishano wa nyakati ngumu na nyakati za furaha. Lakini mwitikio utakaoonesha katika nyakati hizo ndiyo utapima kila kitachotokea katika maisha yako.
Unaposoma ujumbe huu unatakiwa kujua kwamba kuna mtu yupo huko saa hii anateseka na ugonjwa, kuna mtu mwingine anataseka na umaskini, kuna mwingine ambaye katengwa na ndugu, kuna mwingine ambaye ndoa/mahusiano yake yamevunjika, kuna mtu ambaye hana kazi kabisa huku mwingine akiwa kafukuzwa kazi, kuna mtu ambaye saa hii anateseka na upweke huku mwingine akiwa anakabiliwa na msongo wa mawazo juu ya mapito ya maish yake.
Mpenzi unaweza ukajiona una tatizo lakini ukiona tatizo la mtu mwingine ukaona la kwako siyo tatizo bali ni dharura tu imekupata.
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba unapopitia nyakati ngumu hutakiwi kuwa mtu wa lawama sana pamoja na kujutia sana, kiasi kwamba ukawaza mpaka kujidhuru au kuhatarisha uhai wako, kwa kuona kama maisha yako hayana maana tena!
Rafiki huna budi kujua kwamba kila tatizo unalolipitia lipo ndani ya uwezo wako, ndiyo maana hata Mungu kaliruhusu ulipitie, na anatambua fika kabisa kwamba lipo ndani ya uwezo wako na utaweza kulimudu.
1 Wakorintho 10:13 Neno la Mungu linasema; “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”
Unatakiwa kujua kuwa, jibu la kila tatizo lipo ndani ya uwezo wa Mungu wako, hivyo basi badala ya kuangalia ukubwa wa tatizo ulilo nalo, unatakiwa kuangalia ukuu wa Mungu wako dhidi ya tatizo hilo.
Rafiki, hutakiwi kujilaumu, kumlaumu mtu, kumlaumu Mungu, badala yake sasa muendee kwa unyenyekevu na huo mzigo uliokulemea naye atakupumzisha.
Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya matatizo tunapitia lakini majibu anayo Mungu wetu pekee, hivyo ni muhimu kumuendea yeye aliye na uwezo ulio mkuu sana!
Mbali na hilo hutakiwi kulaumu juu ya pito unalopitia badala yake sasa unatakiwa ujifunze jambo Fulani kuhusu pito hilo.
Ukweli ni kwamba siyo kila pito lipo kwa ajili ya kukuangamiza, mengine yapo kwa ajili ya kukupeleka kwenye ukuu!
Sizungumzii baadhi ya mapito ambayo unakumbana nayo lakini uliyasababisha mwenyewe, nazungumzia baadhi ya mapito ambayo hujahusika nayo na yametokea pasipokutarajia!
Hata hivyo kuna wakati mwingine mtu unapitia baadhi ya nyakati ngumu kwa sababu hutambui agano ambalo mwenyezi kaweka juu yako na maisha yako.
Kutokujua agano ambalo Mwenyezi Mungu kaliweka juu ya maisha yetu kimekuwa ndicho kimekuwa chanzo kikuu cha matatizo, dhiki, shida pamoja na majanga ya hapa na pale kwa watu tunaoishi kwenye kizazi hiki.
Ukweli ni kwamba hakuna sehemu ambayo inamuonesha Mungu kakusudia kumtesa mwanadamu, bali mwanadamu hujitesa mwenyewe kutokana na ujinga wa kutokujua kile ambacho Mungu kaahidi kuhusu yeye na maisha yake!
Na, ndiyo maana katika kitabu cha Hosea 4:6 Neno la Bwana linasema;
“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa umekataa maarifa mimi nami nitakukataa wewe”
Hivyo basi badala ya kulaumu kuhusu shida au tatizo Fulani unalokumbana nalo jaribu kujiuliza, Mungu kasema nini kuhusu jambo hilo na wewe umefanya nini kuhusu jambo hilo. Kama utakuwa umefanya kinyume chake, basi ni rahisi kukumbana na hali ya sintofahamu.
Je unafahamu agano ambalo Mungu kaliweka dhidi ya maisha yako? Kama jibu ni hapana basi fuatilia mwendelezo wa makala ijayo!
Lengo la kutoa somo hili ni kukupa mwanga juu ya kile Mungu kasema kwenye neno lake kuhusu pito lako na wewe umefanya nini juu ya kile kilichosemwa na Mungu!
Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment