Jinsi Ya kutengeneza Utajiri
“Yule ambaye hamfundishi mtoto wake jinsi ya kufanya biashara ni sawa na anamfundisha kuwa mwizi”
“Hakuna mtu atakayekufanya ushindwe pasipo ruhusa yako mwenyewe”
Wadau walikuja na msemo usemi usemao; “Kushindwa kupanga ni sawa na kupanga kushindwa”. Hii ni kwa sababu kufeli huja kama matokeo ya moja kwa moja kwa mtu asiye na mipango maishani.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye hupanga kushindwa, bali kuna mtu ambaye hupanga kwanza ili afanikiwe!
Hata hivyo, katika dunia hii tuliyonayo sasa kila mtu ana ndoto za kuwa Tajiri na ndoto za kuufikia uhuru wa kifedha, lakini ni watu wachache tu kati ya hao wengi ambao wanajua jinsi ya kutengeneza utajiri ili wafikie hatua ya uhuru wa kifedha.
Hata hivyo, katika uumbaji wa kitu chochote hapa duniani, huhitajika kwanza malighafi zitakazohitajika kwenye uumbaji huo pamoja na michakato kadha wa kadha itakayopelekea uumbwaji huo uwe halisi.
Kwa kusema hivyo, hata utajiri ni sawa na uumbaji mpya. Hii ni kwa sababu mtu unatakiwa uumbe kitu kipya ambacho hujawahi kuwa nacho hapo awali katika maisha yako.
Kwa maneno mengine ni sawa na kusema, ili kufanikiwa kutengeneza utajiri ni lazima ujue malighafi zitakazohitajika ikiwa ni pamoja na michakato yote utakayotakiwa kufanya ili uweze kuwa Tajiri!
Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kwamba, kujua malighafi pamoja na michakato hiyo siyo kigezo cha kutimiza ndoto za kifedha, bali lazima ufanyie kazi michakato hiyo.
Ukweli ni kwamba hakuna jambo ambalo hutokea pasipo kichocheo, kwa kusema hivyo yule atakayefanyia kazi michakato hiyo, ndiye atakayefanikiwa kifedha.
Hivyo basi ili uweze kuumba utajiri, yafaa uzingatie hatua zifuatazo:-
1. Gundua uwezo wako/kipaji chako/hazina yako
Katika somo la maeneo kumi ambayo fedha imejificha, tuliona kuwa, moja ya eneo ambalo fedha imejificha ni eneo la kipaji au uwezo binafsi.
Ukweli ni kwamba ndani ya kila mtu kuna mgodi wenye hazina kubwa sana ambao endapo utachimbwa basi kila mtu atakuwa Tajiri.
Hata hivyo, tafiti nyingi za kisaikolojia zimeonesha kwamba hakuna mwanadamu ambaye huzaliwa akiwa tupu ndani yake.
Sote tumezaliwa na uwezo, vipaji, talenti na hazina kubwa ambavyo endapo vitagundulika basi kupitia hivyo tutaweza kutengeneza fedha za kutosha.
Unatakiwa kujua kwamba ni lazima ugundue hicho kilicholala ndani yako kwanza, baada ya hapo sasa unatakiwa uanze kukinoa na kukiendeleza hadi kikulipe.
Kinachosikitisha Zaidi ni kwamba watu wengi hawatambui hili ndiyo maana hubaki maskini maisha yao yote. Ama kweli “dunia ina watu wengi maskini wenye vipaji na utajiri ndani mwao”
Rafiki unatakiwa ugundue uwezo wako, ili kupitia huo uwe mwanzo wa wewe kutengeneza fedha. Kumbuka usichokijua kitakuangamiza siku moja.
Hata hivyo wengi wetu hushindwa kugundua vipaji au uwezo wetu kwa sababu ya mifumo iliyotutengeneza pamoja ujinga kuhusu sisi wenyewe.
Yafuatayo ni maeneo ambayo wengi wetu ni wajinga kuhusu sisi wenyewe hali ambayo imetufanya tushindwe kutengeneza fedha:-
1. Ujinga Wa Kutokujua Mimi Ni Nani…
Wengi wetu ni wajinga kuhusu sisi wenyewe. Suala hili limechangiwa na mifumo iliyotutengeneza.
Ukweli ni kwamba mifumo hiyo imetupa pigo kubwa sana, kwa maana imetufanya wengi wetu tushindwe kujijua sisi ni nani ukiachilia mbali na vile ilivyotutengeneza tuwe.
Ndiyo maana si ajabu kukutana na mtu akakwambia yeye ni askari polisi au akajitambulisha kwa mujibu wa kozi aliyoisomea au akakwambia yeye si kitu kwa vile hajasoma.
Swali ambalo nataka ujiulize kabla sijaendelea ni hili, katika hiyo kazi inayokutambulisha wewe ni fulani, vipi kama muda wa kustaafu utafika?
Je, utatambulika kama nani? Na je, ni kweli unastahili kufanya kazi hiyo tu?
Kutokana na hilo unakuta watu wengi tunatambulika kupitia vyeo vyetu na kazi zetu, pasipo kujiuliza Mungu alituumba kwa kusudi gani.
Yaani tumejiona sisi ni wa kimfumo zaidi kuliko hata kusudi la Mungu kutuumba na kutuleta hapa duniani.
Hata hivyo ili kujiepusha na mtego huu, huna budi kuanza kujiuliza maswali yafuatayo:
Hivi mimi ni nani? Nimetokea wapi? Niko wapi? Ninaenda wapi? Na, je ingetokea sifanyi hii kazi au sijasomea hii kozi ningekuwa nani? Maswali haya yataanza kukutoa kwenye mifumo ya kutengenezwa.
Unatakiwa ujiulize maswali hayo kwa sababu mifumo haijakufundisha juu ya wewe ni nani bali imekufundisha vitu vingine ambavyo unapaswa uvifanye na huenda haviendani na maisha yako na jinsi wewe ulivyo.
Je, mpaka kufikia hapa wewe ni nani? Au bado unataka uendelee kutambulika kutokana na kazi unayofanya au kozi uliyosomea? Haupaswi kutambulika kwa namna hiyo, usiwe mjinga wa mifumo huenda hata chuo ungechagua kozi nyingine usingekuwa huyo unayejitambulisha leo.
Hivyo usiruhusu kabisa mifumo ikuamlie unapaswa ujue na utumie nguvu ya wewe kuwa wewe.
2. Ujinga Wa Kutokujua Kile Unachomiliki…
Thamani ambayo haijagundulika haiwezi kutumika. Kila mtu kaumbwa akiwa na hazina, kipaji, karama, kipawa na uwezo fulani ndani yake.
Tatizo ni kwamba umeshindwa kugundua hili kwa vile mifumo imekutengeneza uwe mtu mwingine kabisa, na huku lengo kuu likiwa ni kukuficha usijue kile kilichopo ndani yako.
Nawe pasipo kudadisi umejikuta ukiingia mazima kwenye mifumo na kuamini zaidi katika kutumia uwezo wa kitaalamu kuliko kuamini zaidi kuutumia uwezo uliozaliwa nao.
Kutokana na hilo wengi wetu tumejikuta tukilalama hali ngumu, hasa pale ambapo uwezo tuliofundishwa umeshindwa kutusaidia. Ilihali ndani yetu tunamiliki uwezo mkubwa sana ambao endapo ungetumika vyema ungetusaidia tutatue changamoto zote.
Ndugu unapaswa ugundue uwezo uliopo ndani yako sasa.
Hata hivyo kwa mujibu wa tafiti za kisaikolojia kuwahi kufanyika zimeonesha kuwa kila binadamu huzaliwa akiwa na kipaji fulani. Mbali na hilo hakuna mtu ambaye anazaliwa akiwa hana kipaji.
Kwa ujumla sote ndani yetu tumeumbwa na kile kitakachotufanya tuishi maisha yenye furaha, amani na mafanikio, sema mifumo imetuficha.
Leo ukweli umefahamika jiulize unamiliki uwezo gani ndani yako na unaweza ukautumiaje uwezo huo kujinufaisha.
Hata hivyo huna budi kujua kuwa kila binadamu anazaliwa na uwezo wa zaidi ya maeneo kumi, suala hili tutakuja kujadili katika somo lijalo !
3. Ujinga Wa Kutokujua Kile Unachoweza Kufanya…
Hapa unakuta mtu anakwambia nimejaribu kila njia lakini imeshindikana. Kumbe hajafanya kitu sahihi na amefanya kwa namna isiyo sahihi.
Ukichunguza kwa undani suala hili utagundua kwamba limesabishwa na mifumo ambayo imekupangia kile unachoweza kufanya pasipo kuangalia uwezo uliopo ndani yako juu ya kile unachoweza kukifanya.
Hii ni kwa sababu unakuwa umepewa maarifa na taarifa zisizokamilika/zisizo sahihi, hivyo basi inakuwa ni ngumu sana kuweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto unazokutana nazo.
Kwa mfano badala ya nyani kufundishwa namna ya kukwea miti anafundishwa namna ya kuogelea.
Katika maisha yetu mfano huu unaweza kufanana na mtu anayetumia mbinu za kuogelea katika kukwea mti lazima atashindwa tu.
Na hivi ndivyo mifumo inavyotukosesha uelewa juu ya kile ile tunachoweza kukifanya pamoja na mbinu sahihi za kukifanya.
Mbali na hilo utamsikia mtu akisema hakuna njia mbadala tena. Tatizo siyo njia tatizo ni kwamba mifumo imemfunga kwa kumtengenezea njia moja ya kuona mambo pamoja na kuendesha maisha yake.
Kutokana na hilo kesho ya mtu huyo inakuwa kitanzini. Kwa mfano kuna wale akina sisi tunaoamini kuwa njia kuu ya kuishi maisha mazuri pamoja na kutatua tatizo la umaskini ni kupata ajira zitolewazo serikalini, huku ukweli ukiwa wengi waliopo ajirani siyo matajiri.
Ndugu yangu kabla sijafunga aya hii naomba ujiulize hili, je unaweza ukafanya nini maisha mwako mbali na kazi unayoifanya pamoja na hiyo kozi uliyoisomea?
Je, unaweza ukafanya nini nje na hapo? Kumbuka kesho yako inategemea sana kile unachokifanya leo.
4. Ujinga Wa Kutokujua Kile Unachoweza Kukidhibiti…
Hapa unakuta mtu hujui udhibiti nini kwenye maisha yako. Suala hili linachangiwa na mifumo ambayo imekufanya uone mambo kikawaida sana hata kama mambo hayo ni hatari sana kwako.
Kwa mfano kuna watu ambao hawafanyi chochote kile maishani mwao kwa kile wanachodai kuwa wanasubiri bahati na wakati wa Mungu ufike.
Hebu jaribu kuangalia jinsi mifumo ilivyowafanya watu wengi wawe na fikra mgando. Yaani mifumo imefifisha uelewa wao kiasi kwamba hawajui maisha ni kama kitu tu ambacho ili kibadilike kinahitaji kusukumwa.
Na, hawatoi msukumo wowote ule maishani mwao, wanasubiri mifumo ije isukume maisha yao, kibaya zaidi ni kwamba mifumo hiyo hakuna chochote inachokifanya kwenye maisha yao zaidi ya kupotezewa muda tu.
Kwa mfano watu wengi wameshindwa kudhibiti mtindo wao wa maisha kuanzia: tabia wanazofanya, hulka zao, imani zao, uvivu, kughairisha mambo pamoja na kudharau mambo madogo.
Unachopaswa kujua ni kwamba ukicheka na nyani utavuna mabuwa. Kadri unavyoendelea kuuchekea na kutokudhibiti mtindo wa maisha ambao hauna tija ndivyo unavyofanya maisha yako yapate matokeo yasiyo na tija.
Kwa ujumla ili uweze kubadili kesho yako huna budi kujua kipi unatakiwa ukidhibiti maishani mwako.
Hata kama kuna mifumo imekufunga basi jinasue kwa kujiuliza haya : Je, ni tabia gani ambazo nazifanya sasa ila sitazifanya tena huko mbeleni?
Na je, ni mtindo gani wa kuishi utakaobadili maisha yangu pamoja na kesho yangu? Kumbuka kadri unavyoruhusu ujinga uendeshe maisha yako ndivyo unavyoonekana mjinga…
5. Ujinga Wa Kutokujua Kanuni Asilia Za Maisha…
Wengi wetu ni wajinga sana hasa linapokuja suala la kujua kanuni asilia za maisha.
Unachopaswa kujua ni kwamba maisha yetu yanaongozwa kwa kanuni ambazo hupima kila kinachotokea. Kwa kusema hakuna kitu ambacho hutokea kwa bahati mbaya.
Unatakiwa kujua kwamba linapokuja suala la kanuni asilia, yafaa ujivunje mwenyewe kuliko kuvunja kanuni hizi, kwani pindi ukizivunja zitakupa pigo kubwa sana.
Hata hivyo endapo utatumia vema kanuni hizi utapata matokeo mazuri, na endapo utazitumia vibaya utapata matokeo mabaya.
Kwa mfano kuna kanuni ya kupanda na kuvuna, kuna kanuni ya uvutano, kuna kanuni ya matokeo na kichocheo, kuna kanuni ya uakisi wa mambo, kuna kanuni ya mwitikio na vitendo, kuna kanuni ya kuamini, kuna kanuni ya matarajio, kuna kanuni ya mlimbikizo pamoja na kanuni ya inertia.
Uelewa wa kanuni hizo ni wa msingi sana. Na, ndiyo maana hata kwenye hesabu kuna kanuni ya kupata jibu sahihi lakini hakuna kanuni ya jibu la uongo !
Hata kwenye maisha yako ili kufanikiwa unahitaji kutumia kanuni, na endapo utatumia kanuni hizi vibaya zitakuadhibu kwa kukupa pigo kubwa sana.
Kwa mfano ukipanda juhudi utavuna mafanikio lakini ukipanda uvivu utavuna umaskini.
Unachopaswa kujua ni kwamba fanya yote katika kuishi kwako ila usivunje hizi kanuni.
Leo kabla hujaweka matini hii chini naomba ujiulize unafanya nini juu ya maisha yako na kesho yako? Je, unapanda mbegu gani kwa ajili ya kesho?
Usiruhusu ujinga wa kutokujua kanuni asilia za maisha uendelee kuendesha maisha yako kwa maana nimeshakupa siri zote.
Comments
Post a Comment