Hii Ni Kwa Watu Wanaotaka Kujifunza Vitu Sahihi Lakini Hawajaanza Bado....
Kwa mujibu wa nadharia ya blank slate (tabura lasa) iliyoasisiwa na mwanafalsafa David hume inasema; “hakuna mwanadamu ambaye huzaliwa akiwa ana uelewa wa jambo lolote lile, kwa kusema hivyo vile mwanadamu atakuwa ni jumla ya mambo yote aliyojifunza na kuhifadhiwa kwenye ubongo wake”
Ukweli ni kwamba umekuwa hivyo ulivyo kwa sababu ya vitu ulivyojifunza tokea udogoni mwako.
Unatakiwa kujua kwamba, kuna vitu umejifunza kutoka kwa wazazi wako na huenda havikusaidii, kuna vitu umejifunza kwenye mazingira yako lakini havijakusaidia, kuna vitu umejifunza kwenye jamii yako lakini havijakusaidia na kuna vitu umejifunza shuleni na pengine labda havijakusaidia.
Hata hivyo huna budi kufahamu kuwa, kila mtu ni zao la kile alichojifunza, kwa kusema hivyo kama hutajifunza kitu sahihi huwezi ukawa mtu sahihi atakayeleta matokeo muafaka kwa sababu kilicho ndani ya ubongo wako hakijakufanya uwe mtu sahihi.
Fahamu Kuhusu Aina Za Watu Kwa Mujibu Wa Kile Walichojifunza!
Watu waliohitimu pamoja na kupokea mafunzo katika ngazi mbalimbali wanaweza kugawanywa katika makundi yafaatayo:-
1. Wale Waliochanganywa Kutokana Na Kile Walichojifunza…
Mbali na kuwa watu hawa huwa wameelimika, lakini bado huwa wamechanganyikiwa kwa sababu kile walichojifunza kimefunga fahamu zao na hawaelewi wafanye nini.
Ukweli ni kwamba, hali hii huchangiwa na watu hao kujifunza vitu visivyoendana na wakati uliopo ikiwa ni pamoja na uwezo wao binafsi.
Mtu huyu anakuwa kachanganywa kwa sababu anashindwa kutumia kile alichojifunza ili kutatua matatizo yanayomkabili.
Na ndiyo maana dunia ya sasa inastaajabisha sana, kwa maana, mbali na kuwa ina wasomi, wabobevu na wataalamu wengi lakini bado ina ujinga mwingi.
Na hii ndiyo sababu kubwa ambayo imepelekea hata wasomi wengi kushindwa kujikwamua kimaisha, kwa sababu kile walichojifunza kimeishia kuwachanganya na siyo kuwasaidia.
Na, ifahamike kwamba lengo kuu la kujifunza huwa ni kutumia kile ulichojifunza kujikwamua kimaisha ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo mbalimbali.
Rafiki, unatakiwa kujua kuwa elimu hutolewa ili kutatua tatizo la ujinga, na endapo itatokea mtu kahitimu kutoka ngazi za juu na akaonekana bado yu mjinga maana yake kile alichojifunza hakijamsaidia, badala yake sasa kimemchanganya na kumpotezea uelekeo!
Ukija shuleni utabaini ni kwa namna gani hawa Watoto wamekuwa wakichanganywa, unakuta kila mtoto ana ndoto zake tofauti kabisa na mwingine lakini wote wanapitishwa kwenye mfumo mmoja, ilihali kila mtu anatakiwa kupitishwa kwenye mfumo wake hususani ukihusisha na ndoto zake.
Ubaya unakuja pale unapokuta hata mwalimu mwenyewe anayemfundisha hajui anamuandaa nani.
Na ifahamike kwamba, raha ya kufundisha iko kwenye kumjua mwanafunzi wako anataka kuja kuwa nani.
Endapo mwalimu huyo atajua anamuandaa nani atajua ni aina gani ya mafunzo ampe, apunguze nini na aongeze nini kwenye mafunzo hayo.
Lakini kwa vile hakuna anayejua kuhusu hili ndiyo maana mwalimu pamoja na mzazi, humshinikiza mtoto asome kwa bidi aje apate ufaulu wa kiwango cha juu, pasipo kudadisi huo ufaulu wa juu ni wa nini na utamsaidia nini huyo mtoto hapo baadae!
Ikumbukwe kuna maisha baada ya ufaulu, yafaa Watoto wapitishwe kwenye mifumo tofauti tofauti hasa ukihusisha na wale wanaotaka kuja wawe hapo baadae!
Kumbuka huwezi kuwa mtu sahihi, mwenye kuleta matokeo sahihi kwa wakati sahihi ikiwa hujafundishwa kitu sahihi. Rafiki kila mtu ni zao la kile alichojifunza.
Kwa kusema hivyo kuna watu wamehitimu mpaka ngazi za juu lakini wameishia kuchanganyikiwa kwa kuwa wamejifunza vitu visivyo sahihi!
2. Wale Waliojifunza Vitu Sahihi
Hawa wamejifunza vitu sahihi, na wanaleta matokeo sahihi kwa wakati sahihi, kutokana na kupokea mafunzo sahihi.
Wana uwezo wa kutatua matatizo, wana uwezo wa kukabiliana na hali mbalimbali vilevile wana uwezo wa kufanya mambo yatokee na siyo kusubiri mambo yatokee.
Ukweli ni kwamba kuna makundi matatu ya watu linapokuja suala la kufanya mambo yatokee.
Kuna wale wanaofanya mambo yatokee hawa ndiyo wazuri, kuna wale wanaosubiri mambo yatokee (hawafai), na kuna wae wanaotangaza mambo yakitokea na kuwasifia wale waliofanya mambo hayo yatokee (hawa nao hawafai vilevile).
Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kwamba, kila mtu lazima afanye mambo yatokee kwa mujibu wa kile alichojifunza.
Kwa mfano mara baada ya kujifunza uandishi nimeweza kufanya mambo yatokee kwa maana nimeweza kuandika vitabu kadhaa, makala kadhaa ikiwa ni pamoua na hii unayoisoma!
Je, kutokana na kile ulichojifunza una uwezo wa kufanya mambo yatokee? Kama jibu lako ni Hapana fuatilia makala zote za SoMo Hili!
3. Wale Ambao Hawajaelimika
Hawa ni wajinga kuhusu mambo Fulani Fulani hivi katika maisha yao ambayo ilitakiwa wawe wameshayajua tayari.
Hawajijui wao ni nani, wako wapi, wametoka wapi na wanaenda wapi.
Kilichopo kwenye fahamu zao ni giza na kwa vile pale palipo na giza ndipo kifo kilipo, basi watu hawa hujikuta wakijiuza kwa gharama ndogo kwa sababu hawana maarifa ya kutosha.
Hawa ni wale watu ambao ni waumini wakubwa wa falsafa isemayo; “liwalo na liwe”
Ukweli ni kwamba watu hawa hawana uelewa wowote ule kuhusu maeneo mbalimbali kama vile: eneo la kiroho, eneo la kiuchumi, eneo la kujua kanuni asilia ikiwa ni pamoja na eneo la maendeleo binafsi.
Kutokana na ujinga huo watu hawa huishi maisha ya kujishukuru, huku wakiwa watu wa lawama, majuto, simanzi na masikitiko wasijue kwamba hakuna kiwango cha lawama ambacho hubadili kile kilichotokea!
Rafiki, aliye gizani huwa hajui aendako, na kwa vile watu hawa fahamu zao zipo gizani basi hujikuta wakishindwa kubadili maisha yao kwa sababu hawana maarifa na taarifa sahihi zitakazowasaidia ili wabadili maisha yao!
Endapo itatokea hata wewe kuna vipengele vingi katika maisha na huvijui basi unatakiwa utambue kwamba huna tofauti na mtu asiyeelimika.
Kwa kusema hivyo huna budi ufuatilie makala za somo hili mpaka mwisho ndipo sasa utagundua ufanye nini!
Je, unajua Kwanini Watu Wengi Hujifunza Vitu Visivyofaa?
Usikose Kufuatilia Mwendelezo Wa Makala Hii!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Unatutoa porini nakutuleta mjini, kazi yako njema
ReplyDelete