jinsi Ambavyo Kazi Za Fasihi Na Baadhi Ya Mafundisho Ya Dini Hupelekea Watu Wajifunze Vitu Visivyo Sahihi...
Pasi na shaka una uelewa Fulani hivi kuhusu kazi za fasihi. Hata hivyo miongoni mwa tafsiri nzuri sana ninayoipenda ya fasihi ni ile inayosema; “fasihi ni kazi ya Sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii iliyokusudiwa”
Ukweli ni kwamba kwa kipindi cha muda mrefu, fasihi imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kufikisha ujumbe kwa jamii hususani kuhusu masuala Fulani Fulani hivi yanayoendelea kwenye jamii inayohusika!
Habari mbaya na za kuhuzunisha zaidi ni kwamba, fasihi ya leo imeacha desturi yake ya muda wote! Yaani kutoka kwenye kuikomboa jamii kifkira kwa kuionya, kuielimisha na kuiasa hadi kufikia hatua ya kuanza kuipotosha jamii!
Na hii ndiyo sababu kubwa jamii imeweza kupotezwa na kuanza kushangilia uozo na uovu! Na ndiyo maana siku hizi nyimbo zisizo na maudhui yanayojenga zimekuwa zikikubalika zaidi ukilinganisha na zile nyimbo zenye maudhui yanayojenga na kumkomboa mtu Kifikra!
Hebu jaribu kuvuta picha mambo yanayooneshwa kwenye video mbalimbali zinazofanywa na hawa wasanii! Je, ni halali kwa ajili ya watoto wako na jamii yetu? Vipi kuhusu mavazi pamoja na matendo wanayofanya, je yanapendeza?
Vipi kama wewe mwenyewe au mtoto wako mtaendelea kuangalia hayo yote kila siku, je, tutegemee nini baada ya miaka kumi ijayo?
Bila shaka tutegemee uharibifu utakuja kutokea si ndiyo ee... Huo ndiyo ukweli mchungu unaotakiwa uupokee!
Mpenzi msomaji ni vema tukawa umakini katika hili kwa maana tendo la kujifunza hufanyika pasipo hiari, kwa kusema hivyo akili yako itakichukua kila kitu pamoja na kukihalilisha, hata kama kitu hicho siyo kweli na siyo sahihi kufanyika!
Kutokana na hilo, ndiyo maana jamii yetu ya leo imejaa watu wanaoshangilia na kufurahia maovu yakiwa yanafanyika. Jamii imekuwa ikiyafurahia hayo yote kwa sababu ndiyo mambo wanayoyasikia na kuyaona kwenye baadhi ya kazi za kifasihi.
Kibaya zaidi ni kwamba jamii yetu imeshaamini kuwa; msanii ni kioo cha jamii, hii ni sawa na kusema, msanii anaweza kutumika kama kioo cha kujitazamia na watu wa jamii yote wakafanya kile kile ambacho yeye anakifanya!
Unachopaswa kuchukua hapa ni kwamba, msanii ana nguvu sana ya kushawishi ikiwa ni pamoja na kuwafanya watu wampe umakini mkubwa kutokana na kazi zake za kisanaa!
Tatizo linakuja pale ambapo unakuta huyu msanii anakuwa siyo kioo sahihi, kwa kufanya mambo yasiyo sahihi pamoja na kutoa tungo zilizo kinyume na maadili, na kwa vile yeye ana ushawishi, na ni maarufu, basi ataweza kuwapotosha wanajamii kupitia tungo zake na kuwafanya wanajamii wajifunze vitu visivyo sahihi.
Kwa mfano sasa hivi watu wanafanya sana zinaa, siyo kwa sababu wanatakiwa wafanye ila ni kwa sababu wamejifunza kwenye baadhi ya kazi za fashihi. Na hii ni kwa sababu tungo nyingi zimekuwa zikisifia sana mapenzi. Pamoja na kueneza propaganda za biashara ya ngono!
Hata hivyo sasa hivi kuna watu wanatumia madawa ya kulevya pamoja na kutumia pombe kali si kwa sababu wanatakiwa kufanya hivyo bali ni kwa sababu wamejifunza kwa baadhi ya wasanii. Hali hii imesababishwa na baadhi ya wasanii kuwa vinara wa kuvuta sana na kulewa sana!
Kwa kusema hivyo hata wanajamii wamehalalisha na kuanza kufanya hivyo kwa sababu ni kitu walichojifunza kutoka kwa wasanii wao wanaowakubali.
Ukiachilia mbali hilo nyakati hizi kuna watu wanavaa nusu uchi, huku wakiacha maungo yao wazi, si kwa sababu wanatakiwa kuvaa hivyo bali ni kitu walichojifunza kutoka kwa baadhi ya wasanii! Hii imesababishwa na baadhi ya wasanii kuvaa nguo zisizo na adabu wala staha mbele za watu!
Hata hivyo leo hii kuna watu wanazaa/kuzalisha Watoto na kuwaacha wake zao au waume zao kwa sababu wameona na wanawaiga wasanii wanaofanya hivyo.
Sasa hivi kuna watu wanajiuza huku wengine wakiwanunua kwa sababu ni mambo yanayosifiwa, kushangiliwa pamoja na kutukuzwa kwenye baadhi ya tungo za kifasihi.
Unaweza ukaendelea na orodha ya madhara mengine lakini mimi naishia zangu hapa! Huna budi kuwa makini sana na kile kinachosemwa na kuimbwa kwenye baadhi ya nyimbo, kwa sababu hupokelewa na kuaminiwa moja kwa moja kwenye mfumo wako wa ubongo.
Na ifahamike kwamba, kilichoingia hupima kinachotoka, kwa Kusema Hivyo ukiingiza upumbavu kwenye ubongo wako utatenda upumbavu kwenye maisha yako ya nje!
Hata hivyo sina maana kwamba fasihi ni kitu kibaya lahasha! Lakini mtu mwenyewe unatakiwa ujipe tathmini kwa kujiuliza unamsikiliza nani, kwanini, ukiwa wapi na ili iwe nini!
Rafiki, fasihi ni kama panga lenye makali kuwili ambalo hukata kote kote. Kwa kusema hivyo unaweza ukajifunza au kuharibiwa kwa kujifunza vitu visivyo sahihi.
Unatakiwa kujua kwamba, ubongo wako una uwezo wa kuchukua na kuamini kila linalosemwa kutoka kwa hawa wasanii. Na hii ni kwa sababu wao ni watu maarufu na wanasifika sana!
Hivyo basi ni muhimu kuchuja taarifa zote kabla hujaziruhusu zizame kwenye ubongo wako. Kamwe usinywe maji machafu ukauchafua ubongo wako.
Unatakiwa kujua kwamba hayo yote huimbwa, huoneshwa na hufanyika ili kuifanya akili yako ione kuwa ni kawaida tu, kiasi kwamba hata wewe ujihesabie haki kuwa ni halali yako kufanya hivyo!
Na ndiyo maana kuna watu ambao huiga kila kitu kinachofanywa na wasanii kwa sababu akili zao zimetengenezwa zione hayo yote ni kawaida tu kufanywa na kufanyika kwenye jamii yetu!
Rafiki, siyo kila anayesema unatakiwa umsikilize na siyo kila linalosemwa ni sahihi. Vilevile siye kila aliye maarufu unatakiwa ushawishiwe naye wengine huwa maarufu hata kwa mambo ya kipumbvu tu kwa hiyo unatakiwa uwe makini ndugu yangu!
2. Mafunzo Ya Dini
Kwa habari za hapa duniani hakuna mtu asiyeamini, kwa maana hata yule ambaye haamini, anaamini kuwa haamini kwa hivyo hata yeye anaamini pia!
Angalizo: sipo hapa kupingana na imani ya mtu na sina maana kwamba mtu uachane na imani yako lahasha!
Baada ya kusoma makala hii fanya tathmini fupi kuhusu maisha yako ya imani pamoja na uhusiano uliopo kati yako na Mungu kama uko sawa!
Kama Muelimishaji jicho langu limepita huko likabaini dosari kadhaa ambazo hata mimi zilinikumba, kwa hiyo fuatana nami ili ujue kiundani kivipi mafundisho ya baadhi ya dini yamefanya watu wengi wajifunze yasiyofaa!
Kitu cha kwanza, hata biblia yenyewe inatambua kuhusu uwepo wa walimu wa uongo, manabii wa uongo na kikundi cha watu ambacho kiliingia kwa siri kikabadilisha kweli ya Mungu.
Yuda 1:4 "kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mwenyezi, na Bwana wetu Yesu Kristo ".
Kutokana na hilo si haba endapo utakuwa umekuwa ukipokea mafundisho ya uongo kwa muda wote, kutoka kwa hao watu tajwa kama vile wanavyotambuliwa na biblia yenyewe!
Ukweli ni kwamba wengi kati ya hao wanaofundisha Neno la Mungu, wamepokea mafundisho ya kibinadamu na kinachofundishwa huko ni hekima ya kibinadamu na siyo hekima ya Mungu tena wala Kweli ya Mungu! Isaya 29:13
Kwa kusema hivyo Kweli ya Mungu imekuwa haifundishwi tena. Ndiyo maana waamini wengi fahamu zao zimefungwa na hawamjui Mungu halisi wanayemuabudu ni yupi.
Na ifahamike kwamba, Mungu ndicho chanzo halisi cha busara, hekima na akili. Na elimu ya Mungu ni tofauti kabisa na elimu ya dunia hii. Tatizo linakuja pale ambapo unakuta mtu ambaye ana elimu ya kidunia anataka kufundisha ELIMU ya Kimungu!
Hili ni jambo ambalo haliwezekani, na ndiyo maana wengi miongoni mwa hao wanaofundisha wamekawakaririsha waumini wao kuwa, wasiulize maswali na wasichunguze sana kuhusu Mungu bali wawe watiifu tu!
Wakasahau kwamba mantiki ya kutii ipo kwenye kukitii kile kitu unachokijua, sasa kama muumini mwenyewe hamjui Mungu vizuri atakuwaje mtiifu?
Hali hii imefanya waumini wengi washindwe kushika amri za Mungu, na ndiyo maana wengi wao wanaaishia kufanya mambo ya ovyo mbali na kuwa ni waamini!
Vile vile kuna baadhi ya watumishi utawasikia wakiwaambia waumini wao kuwa, "usichunguze sana maisha yangu wala usifanye kile ninachokifanya Mimi, bali sikiliza pamoja na kutii kile ninachokuambia".
Wakasahau kwamba moja ya sifa kuu ya binadamu ni kujifunza kwa kuiga, kwa kusema hivyo ni ngumu sana muumini Kwenda kinyume na kile kinachofanywa na yule anayemfundisha.
Sasa hivi kweli ya maisha imekuwa haifundishwi tena, na ifahamike kwamba Mungu ndiye hiyo kweli yenyewe, kwa maana maisha yamekuwepo kupitia yeye na kabla hata maisha hayajakuwepo yeye alikuwepo.
Lakini cha ajabu ni kwamba kweli hii haifundishwi tena, cha kushangaza zaidi ni kwamba kwenye baadhi ya ibada jina la shetani linatajwa zaidi kuliko Mungu utadhani shetani ndiye anayeabudiwa na kutukuzwa!
Hii inastaajabisha sana! Haya siyo mafundisho sahihi kwa maana inafaa muumini afundishwe kweli ya Mungu tu! Hutakiwi kukesha kumkemea shetani, wewe mtii Mungu, shetani atakukimbia. Yakobo 4:7.
Leo hii kuna waumini wameambiwa kuwa, wanatakiwa wasifanye chochote kile kwa madai eti wasubiri mpaka wakati wa Mungu ufike, naye atawaamuru kitu cha kufanya!
Swali linakuja wakati wa Mungu ni upi ilihali majira, miaka na nyakati zote ni za Mungu?
Na, kama Mungu kasema kuwa atababriki kazi ya mikono yako. Inakuwaje ufundishwe kuwa usifanye chochote kile? Je, fundisho hili ni halali kama siyo linafunga fahamu zako na kukufanya uzidi kuwa maskini?
Vilevile kuna watu wanafundishwa mafundisho ya kupokea baraka pasipo sababu. Utasikia wakiambiwa pokea baraka za Ibrahim, pokea baraka za Yakobo, pokea baraka za Isaka, pokea baraka za Yusufu.
Ni kweli hawa walibarikiwa, lakini kuna sababu iliyopelekea kubarikiwa kwao. Swali linakuja; je, unafanya kile walichokifanya mpaka wakabarikiwa au unadanganywa tu? Ndugu, kumbuka kwamba, kila kitu hutokea kutokana na sababu.
Sasa hivi kuna watu wanawafundisha waumini wao mafundisho ya kupokea gari, nyumba na fedha. Hivi na wewe kwa akili zako timamu unaamini kwamba unaweza ukapokea fedha, gari na nyumba?
Hata kama unatakiwa uwe na imani thabiti juu ya jambo fulani lijalo, lakini hii siyo imani bali huu ni uwazimu kabisa!
Ukweli ni kwamba hakuna maombi ambayo huleta gari, nyumba na fedha, kama unataka haya yote unatakiwa uchakalike katika kutafuta! Tafadhali amka wewe usinziaye huku ukichukuliwa na mafundisho ya uongo, nenda kapambane hakuna muujiza kama huo!
Sasa hivi kuna viongozi wa dini wanawafundisha waumini wao kuwa wasipotoa sadaka hawatapata uzima wa milele, hebu mtueleze Kuna uhusiano gani kati ya sadaka na uzima wa milele! Ukweli ni kwamba hakuna uhusiano wowote ule!
Kwa habari za watu watakaopata uzima wa milele wapo kwenye KITABU cha ufunuo, wameandikiwa humo lakini cha ajabu kitabu hiki kimekuwa hakifundishwi kabisa! Rejea Ufu 14, uf 15.
Mbali na hilo kuna wengine huwafundisha waumini wao kuwa kama wanataka kufanikiwa kifedha hawana budi kupanda mbegu za kutosha wakitafsiri mbegu kama sadaka kitu ambacho siyo kweli, kwa maana kibiblia neno mbegu linaamaanisha neno la Mungu. Luka 8:11.
Vilevile chini ya mwamvuli wa dini kuna watu wanakanyagishwa mafuta, huku baadhi ya waumini wakiuziwa: maji, chumvi, udongo, chupi zenye upako wa kuleta mume ikiwa ni pamoja na kufanyiwa udhalilishaji wa kimwili kwa mfano wanawake kuogeshwa makanisani! Huu ni ushetani wa wazi wazi kabisa! Rejea Mathayo 24:24.
Kuna watu wanafundisha waumini wao kuwa wao kama viongozi huwa hawakosei katika maamuzi, na kila jambo wanaloliamua liko sawa kwa sababu wao ni watumishi wa Mungu! Sasa mtu anakuletea sera za ushoga halafu anasema huwa hakosei! Hili lipo sawa?
Hata hivyo ukifuatilia kwenye baadhi ya mafundisho Mungu utagundua kwamba, Mungu amekuwa akioneshwa kama ni katili sana, kitu ambacho siyo kweli, kwa maana yeye ni mwingi wa rehema na si mwepesi wa hasira!
Lakini kwa namna baadhi ya wahubiri wanavyolitumia jina hili TUKUFU katika mafundisho yao wanalifanya lionekane ni jina katili sana!
Ukweli ni kwamba Mungu yupo na ndiye chanzo halisi cha busara na hekima. Tunajifunza kwa Habari za mfalme Suleimani ambaye alikuwa na busara kuliko wafalme wote, lakini chanzo cha busara hizo alikuwa ni Mungu.
Vilevile tunajifunza kwa Yesu Kristo ambaye alikuwa na hekima akiwa mdogo sana, kiasi kwamba alikuwa akiwashangaza mpaka wazee wote waliokuwepo Yerusalemu! Huyu naye busara hizo zilitokana na Mungu.
Hii ndiyo hekima inayotakiwa kufundishwa kwenye dini. Kwamba aliye na Imani katika Mungu awe na hekima za kutosha kiasi kwamba jamii iokolewe kupitia yeye.
Lakini sasa hivi hali imekuwa kinyume chake, badala ya wao kuwaokoa wengine basi wamekuwa na hali mbaya kiasi kwamba wanahitaji kuokolewa na watu wasioamini! Ha ha ha ha ha! Hii ni hatari sana, nacheka kama Mazuri vile...
Sasa hivi kuna walimu wa dini wa uongo, kuna wachungaji wa uongo, kuna manabii wa uongo, kuna waonaji wa uongo.
Hawa wote lao moja yaani kufanya uharibifu, kwa maana wanapotosha ile kweli ya Mungu!
Isaya 5:20
Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!
Kwa kusema hivyo waumini hawafundishwi chochote kuhusu Mungu badala yake wanafundishwa mafundisho ya utoaji wa sadaka na kupokea.
Yaani wewe utoe sadaka ili yeye akanunue gari, halafu wewe ufanyiwe maombi ya kupokea gari. Huu ni uwendawazimu wa kiwango cha juu sana.
Na, ndiyo maana sasa hivi wakristo wengi wamekuwa wavivu wa kufikiri, hawafanyi kazi, hawafanyi mambo yatokee bali wanasubiri muujiza wa kufanya mambo yatokee, wanataka miujiza sana, wanakesha kumkemea shetani, wamebaki wakizunguka kutoka kanisa moja Kwenda kanisa jingine.
Hivi huyo unayemtafuta ni Mungu yule ninayemjua mimi au ni Mungu mwingine nisiyemjua? Huoni kuwa unateseka sana?
Siku hizi kuna watu wanawaamini manabii wao, wachungaji wao pamoja na MAKANISA yao na siyo Mungu! Utasikia nina nabii wangu... Nina mchungaji wangu. Ujumbe wako upo hapo nenda kasome, Yer 17:5
Vilevile kuna Baadhi vitabu vya biblia vimekuwa havifundishwi kabisa, hususani vitabu vya manabii kwa mfano kitabu cha Danieli, Ezekieli, Yeremia, pamoja na KITABU cha agano jipya yaani ufunuo!
Wengi wanasema vitabu hivyo vimeandika mambo ya kutisha ndiyo maana huwa hawavisomi wala kuvifundisha! Swali linakuja, je, huyo Mungu wanayemuabudu anatisha?
Na, kama vitabu vyote vinamzungumzia Mungu na vingine havisomwi wala kufundishwa je huyo mtu atamjua Mungu anayemwabudu kikamilifu?
Yapo Mengi sana ya kuzungumza hapa, hususani kwa nyakati tulizonazo, kwa maana tunaishi kwenye nyakati za utimilifu wa agano jipya lakini mafundisho mengi yanayotolewa bado yanadhihirisha utimilifu wa AGANO la kale ambalo lilitimizwa na Yesu miaka 2000 iliyopita!
Katika tafiti zangu nimekuja kugundua kuwa shida siye anayefundishwa bali shida ni yule anayemfundisha, inawezekanaje kipofu amuongoze kipofu mwenzake?
Ama hakika wote watatumbukia shimoni! Sasa unayefundisha huijui biblia yote, ni nini hicho unawafundisha hao waumini?
Na wewe muumini jipe tathmnini kwa kujiuliza haya: je, unafundishwa kweli ya Mungu au unapokea hekima ya kibinadamu?
Je, unamwabudu Mungu Ibrahim, Isaka na Yakobo? Je, unajua Kwanini yeye hujiita kuwa ni Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo?
Sasa kama hujui haya yote umekuwa ukifundishwa nini kuhusu Mungu kwa muda wote uliotumia kufanya maisha yako ya imani?
Swali la mwisho, je, unajua neno la Mungu kutoka mwanzo hadi ufunuo? Kama jibu lako ni Hapana tafadhali nitafute nikuelekeze ufanye nini!
Mpenzi ukitaka uwe na busara nyingi za kutosha ijue biblia! Wala usisubiri mtu akusomee, kwa maana mtu mwingine atakusomea ili ajinufaishe kupitia wewe, yafaa ujifunze biblia ili uwekwe huru!
Yohana 8:32
"Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru".
Je, unataka uifahamu kweli uwekwe huru? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo tafadhali Jibu ujumbe huu kwa kuandika BIBLIA!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44294329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment