Fahamu jinsi Kasumba Ya Kutaka Kukubalika Huwafanya Watu Wajifunze Vitu Visivyo Sahihi...


Kisaikolojia inaaminika kwamba karibu kila jambo ambalo mwanadamu hulifanya maishani mwake, huwa limelenga Zaidi kumfanya akubalike na watu wengine. 

Na hii ndiyo sababu ambayo huwafanya watu wengi wasome shule nzuri, hata kama elimu wanayopokea haiwasaidii katika kuwafungua kiufahamu na kifikra, wahitimu kutoka vyuo vikuu maarufu na vizuri duniani, n.k

Unatakiwa kujua kwamba haya yote hufanyika ili kumfanya huyo mtu akubalike na wengine kutokana na hadhi yake, ikiwa ni pamoja na kumfanya aonekane yu mtu mkuu mbele ya wenzake.

Na ndiyo maana watu waliosoma hujisifu sana na hujiona kama wanajua vitu vyote, kumbe wanavyovijua ni vichache tena visivyowasaidia na wasivyovijua ni vingi tena vilivyo na msaada mkubwa sana maishani mwao!

Ngoja nikuulize swali la kizushi, hivi lengo lako la Kwenda shule kwa ajili ya kusoma lilikuwa ni nini, je, kukombewa kifkira ama Kukubalika?

Unaweza ukawa hujui vilevile, kwa sababu wengi walienda shule kutokana na msukumo uliotoka kwa wazazi wao pamoja na serikali lakini wao kama wao hawajui…

Kwa mfano mimi hapa nilienda shule nikasome, ili nifaulu na nikishafaulu, nije nipate ajira serikalini, cha ajabu ajira yenyewe sijapata, badala yake sasa naambiwa nikajiajiri, 
ilihali hata mwalimu mwenyewe aliyenifundisha ujasiriamali alikuwa kaajiriwa na hakuwa amejiajiri, nina mashaka na alichonifundisha hahaha...

Umeona jibu langu lilivyo? Sikwenda shule nikakue na kuongezeka, kimaarifa, kiufahamu na kiuelewa, bali nilienda ili nikapate elimu itakayonifanya niajiriwe serikalini ili nipate mshahara mzuri, haijalishi nitatumikia ajira gani na itakayoleta matokeo yapi kijamii na kitaifa, lakini kwa wakati huo ajira ndicho kilikuwa kipaumbele changu!

Naweza nikakiri kwamba nimetumia muda mwingi sana Kujifunza ili nikubalike, lakini hadi nahitimu chuo kikuu nilikuwa ni mjinga mmoja hivi niliyekuwa sijijui na sikujua kama sijijui, kwa maana mjinga ni mtu ambaye hajui na hajui kama hajui!

Kinachosikisitisha ni kwamba mbali na kuwa nilijiona ni mjinga, lakini elimu niliyokuwa nayo ilikuwa inawafanya watu wengi wanikubali!

Hata hivyo mara baada ya kutafuta maarifa na taarifa sahihi ndipo sasa nikabaini kuwa nilikuwa nimepotea! 

Ninachelea kusema hivyo kwa sababu nilihitimu chuo lakini sikujua chochote kile kuhusu kweli ya maisha, na sikujua hata nifanye nini ili niweze kutengeneza fedha na kuishi maisha mazuri ijapokuwa watu walikuwa wananikubali kuwa mimi ni msomi...

Unaweza ukawa unajiuliza kwa hiyo kwa muda wote nilikuwa nafanya nini? Jibu ni dogo tu nilitumia muda wangu mwingi kujifunza mambo yasiyo na msaada ili nikubalike kuwa mimi ni msomi...

Siyo kwamba napingana na mfumo lahasha! Lakini kwa vile mimi uliniathiri ndiyo maana nipo hapa kukusanua ili na wewe upate njia ya kuchomoka kiwepesi!

Simaanishi uache shule lahasha! Simaanishi udharau unachofundishwa lahasha! Lakini unatakiwa uendelee kujifunza na kutafuta taarifa sahihi juu ya namna gani unaweza ukatumia hicho ulichofundishwa kubadili maisha yako...

Hata hivyo lengo kuu ambalo huwafanya wazazi wawasukume Watoto waende shule ni kuwataka Watoto hao wafanye vizuri kwa kufaulu alama za juu na kuhitimu elimu ya juu ili wapate vigezo vya kukubalika kupata ajira serikalini.

Na huwamaanisha Watoto wao kwa kuwaambia kuwa; nenda shule, kasome kwa bidi, faulu kwa alama za juu, uhitimu elimu ya juu baada ya hapo utakubalika kupata kazi nzuri serikalini pamoja na kulipwa mshahara mnono na marupurupu ya kutosha hali itakayokufanya uishi maisha yaliyojaa mafanikio tele.

Hali hii imeathiri fikra za watu wengi na ndiyo maana kila mtu aliyehitimu kutoka chuo, kwenye fahamu zake anachojua ni kwamba ajira za serikalini ni haki yake ya kuzaliwa na asipopata hujikuta akiwalaumu viongozi kuwa hawaajiri kumbe tatizo siyo kiongozi kutokuajiri bali tatizo ni mfumo uliomtengeneza...

Lakini cha ajabu kuna watu waliishi kabla hata serikali hazijaanzishwa, na kuna watu wanaishi bila kuajiriwa serikalini, sasa kama mtu ambaye hajasoma anaishi na halalamiki wewe na usomi wako unalaumu nini? 

Hapo sasa itabidi ukubaliane na mimi kwamba, ulifundushwa ili ukubalike na siyo ukombolewe kifikra!

Unatakiwa kujua kuwa, hoja ya kutaka kukubalika ndiyo imefanya watu wengi wajifunze vitu visivyofaa, kwa maana hawajasoma kwa sababu wanavitaka, bali wamejifunza ili wafikie vigezo vya kukubalika, na mara baada ya kukubalika huona kama ndiyo lengo lao limetimia. 

Sawa umesoma na vigezo vya kuajiriwa unavyo na ajira hazipo, je, utaendeshaje maisha yako? 

Je, utatumiaje kile ulichojifunza kubadili maisha yako ilihali ulijifunza ukubalike ajirani?

Unatakiwa kujua kwamba maana ya elimu ni kumfungua yule anayejifunza ufahamu na kumfanya awe na uwezo wa kufanya mambo yatokee kupitia kile anachojifunza.

Sina maana kwamba hutakiwi kusoma lahasha! Lakini mtu mwenyewe huna budi uangalie matokeo unayoyaleta kwenye jamii na taifa lako kama matunda yanayotokana na kazi unayofanya kutokana na kile ulichosomea! 

Kwa maana kuna watu wameajiriwa na wanapokea mishahara lakini matokeo ya kazi zao hayaonekani na hata kama yapo yanawanufaisha wao zaidi kuliko taifa lao na jamii yao! Watu hawa kwangu huwa nawaona ni sawa na wanapokea mshahara bure!

Je ulisoma ili ukubalike? Au ulisoma ili ujikomboe kifkira hali itakayokufanya ulibadili taifa lako na jamii yako?

Jibu unalo! Baki nalo mwenyewe, lakini ukweli umeshasogezewa hapa!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant! 

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...