Kama Huna Malengo Sahau Kabisa Kujifunza Vitu Sahihi Maishani Mwako...


Hivi unafahamu kwamba asilimia kubwa ya watu wengi hapa duniani huishi pasipo malengo maishani mwao hali ambayo huwafanya washindwe kutofautisha mafunzo sahihi na mafunzo yasiyo sahihi?

Ukweli ni kwamba kujifunza ni jambo ambalo huenda sawa na lengo la kujifunza, kwa hiyo inapotokea mtu akawa anajifunza lakini hana lengo lolote lile katika kujifunza kwake, maana yake mtu huyo ataishia kujifunza vitu visivyo na msaada maishani mwake!

Hata mimi hapo awali kabla sijajitafuta nilikuwa ni mtu ambaye sikujua maana halisi ya lengo, na sikuwahi kuazimia lengo lolote lile maishani mwangu, kwa maana sikuwa na uelewa wowote ule kuhusu lengo!

Kwa kusema hivyo nilikuwa naishi tu kwa vile niko hai, ila kule nilikokuwa naongoza maisha yangu nilikuwa sikujui, kutokana na hilo nikajikuta nikijifunza karibu kila jambo si kwa sababu ninatakiwa kujifunza ila ni kwa sababu sikuwa nimelenga chochote kile kwenye ujifunzaji wa mambo hayo!

Matokeo yake sasa nilijikuta nikisoma hata vitu ambavyo sikuvihitaji kwa wakati huo kwa kuwa sikuwa na malengo yoyote yale kuhusu kesho yangu ijayo...

Ninaandika hili si kwa ajili yangu tu, na si kwamba jambo hili limenikumba mimi pekee lahasha!

Fahamu zangu ndogo zinasikitika juu ya mamilioni ya wanafunzi waliopo shuleni kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimbali! 

Binafsi sipingani na mfumo, lakini shida inakuja kwa kile ambacho huyo mwanafunzi anajifunza na kufundishwa, lazima tujue ni nini kinafundishwa na kinamsaidiaje huyo mjifunzaji! 

Kwa mujibu wa tafiti Binafsi ambazo nimezifanya, nimekuja kugundua kuwa, wanafunzi wengi wapo shuleni na wanajifunza kwa sababu ya msukumo wa serikali pamoja na wazazi wao, lakini wajifunzaji wenyewe hawajui kwanini wapo shuleni, kwanini wanajifunza na kibaya zaidi ni kwamba hawana lengo lolote lile katika kujifunza kwao!

Na ndiyo maana huwa wanakubali na kupokea kila wanachofundishwa haijalishi ni cha kweli au laah!

Pia, ndiyo maana wamekuwa siyo wadadisi kabisa juu ya kile kinachofundishwa kama kina mantiki au laah, kwa sababu hawajalenga kupata chochote kile kutokana na kujifunza kwao! 

Sina maana kwamba wanafunzi wote hawajui kwanini wapo shule lahasha! Wachache wanajua, lakini miongoni mwa hao wachache wanaojua wengi wao wanaishia kusoma vitu visivyowasaidia kabisa kwenye maisha yao ya sasa na hata baadae! 

Kwa mfano kipengele kinachodai kuwa chimbulo la mwanadamu alikuwa sokwe kinamjenga nini mwanafunzi kifikra zaidi ya kumdunisha na kuzalilisha utu wa binadamu? Je, maandiko yanasemaje juu ya hili? Rejea mwanzo 1:26

Au mwananafunzi kukaririshwa majina ya wapepelezi, wamisionari na wafanyabiashara kama vitangulizi vya ukoloni, watu waliokuwa waharibifu, walioleta ukoloni Afrika, uliopelekea unyonywaji wa bara la Afrika na mateso kwa babu zetu, kunamsaidia nini mwanafunzi kwenye ulimwengu huu wa sasa?

Au mwanafunzi kufundishwa na kukaririshwa majina ya magavana wote walioitawala Tanganyika enzi za utawala wa serikali ya kikoloni ya waingereza kunamsaidia katika kupanua fikra zake na kumfanya awe mvumbuzi? 

Au mwanafunzi kufundishwa sekta za uchumi wa serikali ya kikoloni zinamsaidia nini kwenye maisha yake ikiwa hata uchumi wa nchi yake na uchumi wake mwenyewe haujaimarika, sasa badala ya kufundishwa afanye nini ajijenge kiuchumi mwanafunzi anafundishwa sekta za uchumi wa kikoloni, je hii ni halali?

Au unakuta mwanafunzi kufundishwa kuhusu ukoloni barani Afrika enzi za miaka ya 1800 huko kunamsaidia nini Zaidi ya kumharibu kifikra na kumfanya awaone waafrika walikuwa wanyonge na wapumbavu!  

Si vibaya kuijua historia, lakini kujifunza kwenye historia ndiyo muhimu zaidi! Kwa Sababu usipojifunza kwenye historia, historia hiyo itajirudia maishani mwako!

Hiki ndicho kinachotokea sasa, kwa maana mbali na kuwa watanzania wengi kujifunza kuhusu mada ya ukoloni, tokea enzi wamepata uhuru mpaka sasa, wameshindwa kuuzuia ukoloni uliostaarabika ali maarufu kama ukoloni mamboleo!

Hii inamaanisha kuwa tokea uhuru watanzania wamekuwa wanasoma historia ya ukoloni lakini hawajajifunza chochote kile, hususani kuhusu makosa yaliyofanywa na babu zetu hadi kupelekea kuwaruhusu wakoloni hatimaye wakawatawala!

Kadhalika na watanzania wa leo wamejikuta wakiruhusu makosa yaleyale yaliyofanywa na babu zao kwa kutokujifunza kwenye historia! Na hii ndiyo sababu kubwa, ukoloni mamboleo umeota mizizi nchini!

Je, hili nalo ni uzushi? Ukoloni mamboleo si upo? Na kama watanzania wengi wamejifunza historia kuhusu ukoloni walijifunza ili iweje? Mbona wameshindwa kuuzuia ukoloni mamboleo?

Ukweli ni kwamba Kilichotokea huko nyuma ndicho kinatokea sasa, na hii ni kwa sababu watu wanajifunza historia lakini hawajifunzi kwenye historia!

Nimetaja kwa ufupi tu ili ujue kwamba sawa Watoto wapo shule lakini kwa vile hawana malengo yoyote yale, ndiyo maana wanakaririshwa na kufundishwa mambo yaliyopitwa na wakati, hali ambayo huwafanya hata wao wapitwe na wakati ikiwa ni pamoja na kuzalisha mawazo yaliyopitwa na wakati! 

Hata hivyo wengi hujifunza yasiyofaa kwa vile huwa hawana lengo jingine tofauti na lengo la kuhitimu kwa ufaulu mzuri ili waweze kupata ajira serikalini, na ndiyo maana mtu huwa haoni shida kupoteza muda shuleni kufundishwa baadhi ya mambo yasiyo na msaada ili afikie tu kigezo cha kupata ajira serikalini! 

Sina maana kwamba ajira ni kitu kibaya lahasha! Mimi mwenyewe ni mwajiriwa tena wa sekta binafsi japo sitatumikia maisha yangu yote, lakini nimeandika hili kukusanua ili ufikiri nje ya boksi! 

Hata hivyo nikiwa kazini kwangu kama mwalimu huwa nadadisi kipengele ninachomfundisha mwanafunzi kama kinamsaidia mwanafunzi huyo, na endapo nitabaini kuwa hakimsaidii huwa namuambia kuwa hiki soma kwa lengo la kujibia na kufaulu mtihani, ila kumbuka kuwa kuna maisha baada ya kujibu na kufaulu mtihani.

Ukweli ni kwamba elimu yetu ni ya kujibia mtihani tu na siyo kumsaidia mwanafunzi awe na uelewa mpana na kufunguka kiakili kiasi kwamba awe na uwezo wa kufanya mambo yatokee.

Unaweza ukawa unajiuliza kama iko hivyo kwanini watu hawa huendelea Kujifunza? Jibu ni fupi tu ni kutokana na wengi wao kukosa malengo maishani mwao!

Kutokana na hilo hujikuta wakienda na mfumo huo wa elimu huku wakiwa hawajui ni wapi unawapeleka, hatimaye sasa hufika chuo kikukuu ambapo huwapasa kuchagua kozi, wengi huchagua kozi kwa ajili ya urahisi wa kupata ajira na siyo kwa ajili ya kuleta matokeo yenye tija kwenye taifa na jamii yetu!

Swali linakuja, kwa hiyo kwa muda wote aliokuwa shuleni alikuwa anajifunza nini? Je, ni wapi pameandikwa kwamba mtu achague kozi anayoipenda akifika chuo kikuu tu? Vipi kama kila mtu angekuwa anapewa elimu sawa sawa na malengo yake?

Unatakiwa kujua kwamba endapo ingekuwa hivyo tungefika mbali kimaisha na hii Tanzania ya leo isingekuwa hivi ilivyo. 

Ukweli ni kwamba ukikosa malengo utaona kama kila fundisho linalotolewa ni sawa tu, lakini ukishaweka lengo siyo rahisi kujifunza kila jambo linalofundishwa!

Nimejifunza vitu vingi visivyokuwa na msaada wowote ule maishani mwangu kwa kuwa sikuwa na malengo yoyote yale! 

Hata hivyo baada ya kuja kugundua kuhusu kuweka malengo ndipo sasa nikaanza kujifunza vitu sahihi kwa maana nilikuwa naweka lengo na kutafuta maarifa na taarifa sahihi kuhusu lengo hilo.

Hii ni sawa na kusema kukosa malengo kumewafanya watu wegi sana wajifunze vitu visivyowasaidia, kutokana na hilo wengi wamegeuka na kuwa watii wa mfumo uliopo hata kama mfumo huo hauwasaidii kwa chochote kile!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...