Jinsi ambavyo Umaskini Huwafanya Watu Wajifunze Vitu Visivyo Sahihi...

Katika safari ya kuishi kwangu na kujifunza nimekuja kugundua kuwa, maskini huwa hana chaguo! Ukweli ni kwamba maskini ni sawa kabisa na yatima ambaye huwa hadeki! 

Kwa kusema hivyo hapa duniani kuna elimu maalumu kwa ajili ya matajiri na kuna elimu maalumu kwa ajili ya watu maskini.

Hii ni sawa na kusema Tajiri atapokea elimu nzuri kwa sababu ana uwezo wa kuimudu kwa kulipa gharama, kwa maana hakuna kitu kizuri ambacho hupatikana bure au hupatikana kwa bei rahisi. 

Na elimu hiyo ambayo matajiri hupokea huwa inalenga kufundisha mambo halisi yaliyopo kwenye mazingira waliyopo ili watumie taarifa hizo katika kutengeneza utajiri! 

Kwa mfano elimu hiyo hufundisha masuala ya uwekezaji pamoja na ugunduzi na uvumbuzi.

Kwa mantiki hiyo ni ngumu sana kuona Tajiri akipitishwa kwenye mitaala ya zamani ambayo haimpi taarifa sahihi zinazoihusu dunia tuliyonayo sasa! 

Nakusanua tu nenda kapitie kwenye mitaala ya nchi zilizoendelea ndiyo utagundua uhalisia wa kile ninachozungumza hapa.

Kwa upande mwingine maskini huwa hana chaguo linapokuja suala la kupokea elimu, kwa kusema hivyo, mtu huyu hujikuta akiingia mazima kwenye mfumo wa elimu inayotolewa haijalishi hicho anachojifunza kitamsaidia aepukane na umaskini au kitamfanya awe maskini wa kutupwa!

Aina hii ya mitaala ipo kwenye nchi zinazoendelea, hata kwenye nchi yetu tuna hii elimu, ambayo kwa asilimia kubwa haifundishi mambo yanayolenga kumfungua mwanafunzi kiufahamu.

Badala yake inaua hata uwezo wa mjifunzaji kufanya ugunduzi na uvumbuzi kwa sababu mambo mengi yanayofundishwa anatakiwa ayakariri na siyo ayaelewe!

Lakini jambo hili linachangiwa na umaskini, kwa Sababu kama huna hela huwezi ukapata elimu nzuri itakayokusaidia uweze kuishi maisha mazuri, na siyo tu kuishi kwa sababu uko hai! 

Ukweli wa mambo unaotakiwa kufahamika kwa wengi ndiyo huu; "elimu yoyote ile ni gharama". 

Kutokana na hilo ndiyo maana tukapata usemi maarufu usemao; “kama unaona elimu ni gharama basi kajaribu ujinga kwa maana utakugharimu Zaidi”. 

Mantiki yake ikiwa elimu yoyote ile ni gharama na hii ni kwa sababu, kile utakachojifunza kitakuja kubadili maisha yako mara baada ya kukitumia!

Lakini kwa sababu wanajamii wengi ni watu wa kawaida basi wameshindwa kuwasomesha Watoto wao kwa kuwapa elimu bora kwa sababu hawana uwezo wa kusomesha. 

Matokeo yake mjifunzaji huyo huishia kupitishwa kwenye mitaala ya kizamani ambayo haina msaada kwake. Kwa mfano mwanafunzi anaambiwa achore Samaki, achore panzi, achore michoro ya hatua za ukuaji wa chura, achore baiskeli. Badala ya kufundishwa kutengeneza yeye anafundishwa kuchora...

Swali linakuja, ikiwa haya yote yanafundishwa, je, yanamsaidiaje huyo mwanafunzi kwa karne hii?

Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kuhusu historia, ukweli ni kwamba historia inayofundishwa huko shuleni imemuweka mwafrika kama mtu duni sana. 

Kwa kusema hivyo hata mwanafunzi anayejifunza anatengenezewa fikra hasi kuhusu rangi nyeusi pamoja na mababu zake, hali ambayo humfanya ajidharau pamoja na kuidharau Afrika!

Kumfundisha mwanafunzi kuwa mwanadamu alikuwa ni sokwe ni kumharibu kimtizamo na kiakili! Hata kama ni elimu bure sasa ndiyo mwanafunzi afundishwe hili?

Kumfundisha mwanafunzi kusema kwamba hakuna chochote kilichokuwepo Afrika kabla ya kuja kwa wakoloni ni kumharibu mwanafunzi kiakili. Afrika ilikuwa imeendelea tu hata kabla wakoloni hawajaja!

Kwa upande wangu ninachokifahamu ni hiki, ni vizuri kuijua historia, lakini muhimu Zaidi kwangu siyo kuijua historia bali ni kujifunza kwenye historia hiyo. 

Kwa sababu usipojifunza kwenye historia, historia hiyo itajirudia kwenye maisha yako! 

Kwa mfano mwanafunzi kajifunza kuhusu kuanzishwa kwa ukoloni barani Afrika, lazima aoneshwe ni wapi wenzetu walifeli na kiliwakuta nini baada ya kuuruhusu ukoloni!

Baada ya hapo afundishwe jinsi ya kuziba mianya yote ili asiruhusu ukoloni mamboleo! 

Ukweli ni kwamba ukoloni mamboleo upo, lakini kwa sababu mwanafunzi anafundishwa ili ajibie mtihani, akishajibu afaulu na akishafaulu vizuri, aje apate ajira serikalini ili apambane na umaskini, ndiyo maana ukoloni mamboleo bado upo mbali na kuwa kwenye mitaala anafundishwa kuwa apambane nao!

Mbali na hilo kuna vitu vinafundishwa kwenye historia lakini ni historia iliyopitwa na wakati na isiyo na msaada kabisa kwa mjifunzaji!

Kwa mfano unakuta mwanafunzi anafundishwa kuwa seyyid said alihama na mtaji kutoka Oman hadi Zanzibar mwaka 1840. 

Swali linakuja huyu mwanafunzi anajifunza nini kwenye hilo fundisho?

Ukweli ni kwamba umaskini umefanya watu wengine wakose chaguo. Hali hii ndiyo sababu imepelekea watu hawa wajifunze yale yasiyofaa kwa sababu ndiyo mfumo walioukuta na hawana uwezo wa kumudu gharama za kumpeleka mwanafunzi akasomee elimu nyigine.

Na ifahamike kwamba siyo kwamba wanajamii wote wa tanzania wameshindwa kuona madhaifu ya elimu yetu, wengi wanaona lakini kwa sababu ya umaskini hawana chaguo tena. 

Hata hivyo elimu inayotolewa nchini kwetu siyo ya viwango vya juu katika eneo la sayansi na teknololojia kwa sababu ya umaskini.

Kwenye somo la sayansi wanasisitiza matumizi ya kompyuta lakini ukienda shuleni kwenyewe kompyuta hazipo za kutosha kwa sababu ya umaskini wa kiwango cha kitaifa.

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com


Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...