Hii Ni Kwa Wale Waliogundua Uwezo Wao Tu, Fahamu Kuhusu Maandalizi Unayotakiwa Uyafanye Ili Uuishi Uwezo Wako...
Habari yako rafiki yangu, ni matumaini yangu u mzima wa afya!
Karibu kwenye mwendelezo wa somo letu, kwa siku ya leo tunaenda kuangalia juu ya kipi ufanye kama maandalizi ya kukusaidia uweze kuuishi uwezo wako!
Ikumbukwe makala iliyopita ilidokeza kuhusu maeneo kumi ya uwezo ambao kila mwanadamu huzaliwa nao!
Bila shaka uligundua uwezo wako lakini hujui juu ya kipi ufanye ili uuishi uwezo huo, kama iko hivyo soma makala hii kwa maana inaenda kukuonesha aina ya maandalizi unayopaswa kuyafanya!
Ukweli ni kwamba, hakuna mtu ambaye huwa bora katika jambo fulani pasipo kufanya maandalizi. Hii ni sawa na kusema kuwa, kiwango cha maandalizi ndicho kitapima kiwango cha mafanikio utakachofikia katika kuuishi uwezo wako.
Na maandalizi unayopaswa kufanya ni yale yanayoenda kwa vitendo, ndiyo maana ilishawahi kusemwa kuwa; “ni kupitia kufanya kwa vitendo tu ndiko hutufanya tuwe wakamilifu”
Kwa mantiki hiyo, hata wewe ili uweze kufanikiwa katika kuuishi uwezo wako lazima ujiandae vya kutosha.
Na usipofanya maaandalizi huwezi ukawa bora katika kuuishi uwezo wako. Hivyo basi unatakiwa kila siku ufanye jambo Fulani linalokusogeza kwenye kuuishi uwezo wako.
Unaweza ukawa unajiuliza kuwa katika hatua hii ya kujiandaa ili niuishi uwezo wangu ninatakiwa nifanye nini?
Yapo mengi ya kufanya ikiwa ni pamoja na haya yafuatayo: kufanya tafiti za kutosha kuhusu watu waliofanikiwa kuuishi uwezo kama wako, kwamba walikuwa ni watu wa aina gani, walikuwa na sifa zipi na walikuwa wanafanya nini.
Ukishafanya hivyo na wewe fanya kama wao, kumbuka kuwa endapo utafanya kitu kilekile na kwa namna ileile kama watu waliofanikiwa walivyofanya nawe utaishia kupata matokeo kama yao!
Mbali na hilo moja ya kithibisho tosha kwamba, hata wewe unaweza kufanya jambo Fulani ni kwa sababu wengine wameweza kufanya jambo hilo!
Vilevile katika kufanya maandalizi ili uweze kunoa uwezo wako huna budi kutafuta maarifa sahihi na taarifa sahihi.
Rafiki unatakiwa kujua kwamba taarifa hizi zitakuwa ni kama njia zitakazokuongoza ili uweze kuuishi uwezo wako.
Kumbuka kama hutakuwa na taarifa sahihi utapitwa na wakati, na kama haujui kipi ufanye utatolewa kwenye mfumo!
Unatakiwa kujua kwamba watu wengi ni wajinga kuhusu wao wenyewe kwa kuwa siyo wajifunzaji.
Na mjinga ni mtu ambaye hajui na hajui kama hajui. Hii ni sawa na kusema kuwa, mtu huyo anakuwa hana taarifa sahihi juu ya kipi afanye ili aishi uwezo wake na hajui kama hana taarifa sahihi.
Ukweli ni kwamba endapo utakosa taarifa sahihi huwezi ukauishi uwezo wako.
Rafiki unatakiwa utafute maarifa na taarifa sahihi kwa sababu, kila uwezo ambao umezaliwa nao una maarifa fulani unayotakiwa uyazingatie ili uuishi!
Na maarifa hayo yapo kwenye maandiko mbalimbali, kwa kusema hivyo kama hutakuwa msomaji huwezi ukagundua jinsi gani utumie uwezo wako ili utengeneze kipato.
Vilevile hatua hii ya maandalizi inakutaka uiandae akili yako vizuri kwa kujiona tayari unauishi uwezo wako. Hii ni kwa sababu yule unayemuona ndiye utakayekuwa.
Unatakiwa kujua kwamba endapo utajiona ukifanya jambo Fulani kwa ufasaha na ukatengeneza na hisia kuhusiana na jambo hilo utapata utayari wa kulifikia jambo hilo.
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba hisia kuhusu jambo Fulani zikiwa kubwa, maana yake utakuwa unapata msukumo usiokuwa wa kawaida kabisa ambao utakuchochea ili uuishi uwezo wako!
Na, endapo itatokea haujaanza kuuishi uwezo wako, utajikuta ukipata hisia kali zinazokuuliza kuwa kwanini bado hujaanza kuuishi uwezo huo!
Rafiki unatakiwa kujua kwamba huwezi kuwa bora bila kujiandaa, na busara inatutaka tubaki huku tukiwa tumejiandaa kwa ajili ya fursa zinazotokana na uwezo wetu, kuliko kutokujiandaa kabisa halafu fursa zikaja tukashindwa kuitumia, tukabaki kuwa na manung’uniko na masikitiko eti kisa tu hatukujiandaa.
Jiandae kiakili, jiandae kiroho, jiandae kimwili, jiandae kihisia. Na hata ikitokea umeamshwa usiku wa manane ili utumie uwezo wako katika kufanya jambo fulani unatakiwa uweze kufanya jambo hilo.
Kama unaweza kuimba fanya maandalizi ya kuimba kila leo, kama uwezo wako ni kuandika huna budi kuandika kila leo, kama uwezo wako ni wa kimichezo huna budi kufanya mazoezi ya kutosha.
Haijalishi utakuwa una uwezo gani, hakikisha unajiandaa vya kutosha, kwa kufanya jambo Fulani kila siku.
Rafiki, kama huwezi kupaa basi kimbia, kama huwezi kukimbia basi tembea na kama huwezi kutembea basi tambaa. Haijalishi utakutana na nini lakini hakikisha unajiandaa na unasonga mbele katika kuuishi uwezo wako.
Kumbuka kuwa unapokuwa unarudia kufanya jambo Fulani kila leo na kwa mwendelezo ndivyo unavyokuwa bora katika jambo hilo kadri siku zinavyozidi Kwenda mbele!
Jaribu kuwaza kila siku ukawa unafanya mazoezi ya kuimba, je, kiwango chako kitakuwaje mara baada ya siku 365?
Au jaribu kuwaza kila siku ukawa unafanya mazoezi ya kuandika, je, kiwango chako kitakuwaje mara baada ya siku 365?
Ndugu jiandae! Jiandae! Jiandae! Na usipojiandaa kwa ajili ya kuuishi uwezo wako hakuna atakayefanya kwa niaba yako!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment