Jinsi Ambavyo Kujiuliza Maswali Ya Kiudadisi Humfanya Mtu Ajijue Kiundani Na Kugundua Kusudi La Kuumbwa Kwake...
Habari yako rafiki yangu, ni matumaini yangu u mzima wa afya!
Karibu sana kwenye mwendelezo wa somo letu linaloangazia kuhusu jinsi ya Kujifunza Vitu Sahihi...
Makala iliyopita ilidokeza hoja moja tu, juu ya namna gani unaweza ukaanza kujifunza vitu vipya kwa kuweza kufuta mambo yote uliyojifunza huko nyuma ambayo yameonekana kutokukusaidia!
Baada Ya kufanya yale yote uliyoshauriwa katika hatua ya kwanza, sasa Unakaribishwa kwenye hatua ya pili ambayo ni kama ifuatavyo:-
2. Jiulize Maswali Mbalimbali Ya Kidadisi...
Mara baada ya kufuta kila kitu katika hatua ya kwanza bila shaka utakuwa umepoteza hadi historia yako na utambulisho wako.
Kwa mantiki hiyo ili uweze kujijua vizuri wewe ni nani, ndipo sasa utatakiwa uanze kujihoji maswali mbalimbali ya kidadisi!
Ukiwa katikati ya tafakari nzito, anza kuiona dunia yako kwa namna nyingine tofauti na vile ulivyokuwa unaiona mara ya kwanza, huku ukijiona ukifanya jambo Fulani hivi tofauti na vile ulivyokuwa ukifanya hapo awali...
Anza kujiona ukifanya mambo yatokee, jione ukiibadilisha dunia yako, jione ukiifanya dunia yako kuwa sehemu nzuri na ya kupendeza!
Hata hivyo ukiwa bado katika hali ya tafakari jaribu kujiuliza hili; "hivi kwa nini niliumbwa na nikazaliwa nikiwa hivi nilivyo?"
Baada ya kujiuliza hivyo anza kutafakari kuhusu kusudi la kuumbwa kwako...
Ukweli ni kwamba kila mtu kaumbwa kwa kusudi Fulani.
Unatakiwa kujua kwamba, mbali na kuwa umesoma mpaka elimu ya juu au umefikia kiwango fulani cha elimu, siyo uthibitisho wa wewe kuliishi kusudi lako kwa sababu unaweza ukawa umesomea kitu ambacho hakiendani kabisa na kusudi la kuumbwa kwako!
Huenda hii ndiyo sababu ambayo imekufanya ushindwe kubadilisha maisha yako hata kama wewe ni msomi...
Unatakiwa kujua kuwa; kama vile mtu aliyetengeneza simu alivyokuwa na kusudi la kutengeneza kifaa hicho yaani matumizi yake, vivyo hivyo ndivyo na Mungu alivyokuwa na kusudi la kuachilia uumbwaji wako!
Kumbuka kuna kusudi la kuumbwa kwa kila mtu, na kupitia kuliishi kusudi lake, mtu huyo atatengeneza kipato pamoja na kurahisisha maisha yake!
Swali linakuja, ikiwa sijafundishwa chochote kile kuhusu kusudi nifanye nini ili nigundue kusudi la kuumbwa kwangu?
Rafiki, usijali ni rahisi sana! Ili kugundua kusudi la kuumbwa kwako fanya jambo moja kati ya haya yafuatayo:-
Jaribu kuangalia ni jambo gani ambalo unapenda kulifanya pasipo kutimia nguvu, hata kama kwa mwingine jambo hilo linaonekana ni gumu sana, maadamu unalipenda na unafurahia kulifanya basi hilo linaweza kuwa ndiyo kusudi la kuumbwa kwako!
Je, ni jambo gani ambalo unaweza ukalifanya kwa ufasaha na kwa uweledi pasipo hata kujifunza? Bila shaka lipo, kama umelibaini jifunze jinsi gani unaweza ukalifanya jambo hilo ili utengeneze kipato!
Vilevile unaweza ukagundua kusudi la kuumbwa kwako kwa kujiuliza ni tatizo gani uliumbwa uje ulitatue.
Unatakiwa kujua kwamba kila tatizo lililopo ni fursa ya kusudi la mtu Fulani. Kwa mfano tatizo la ujinga ni fursa yangu mimi kama muelimisha jamii kulitatua na kulipwa kupitia kufanya utatuzi wake!
Je, wewe unaweza ukatatua tatizo gani katika jamii yako?
Kumbuka fedha ni zawadi anayopewa mtu mara baada ya kutatua matatizo ya watu, hata wewe unaweza kufanya maisha yako yawe na kusudi kwa kutatua matatizo ya watu!
Mbali na hilo unaweza ukagundua kusudi lako kwa kuangalia ni jambo gani ambalo limekuwa lilikukera sana na pengine labda hata sasa unatamani lingeweza kuondolewa.
Ukweli ni kwamba kila mtu ana jambo ambalo huwa linamkera sana na anatamani lingeondolewa, unatakiwa kujua kwamba huenda kusudi lako lipo kwa ajili ya kuondoa jambo hilo ndiyo maana hilo jambo linakukera sana!
Habari njema ni kwamba, endapo utaweza kuliondoa tatizo hilo, watu watakulipa kwa sababu umewaondolea kikwazo.
Hata hivyo unaweza kugundua kusudi la kuumbwa kwako kwa kujenga mahusiano mazuri na Mungu wako.
Unatakiwa ujiunganishe kwa Mungu wako ili akuoneshe kusudi la kuumbwa kwako kwa maana yeye ndiye aliyekuumba.
Lakini ili uweze kufanya hivyo yafaa uzaliwe mara ya pili, kwa maana pasipo kuzaliwa mara ya pili huwezi kuwa na mahusiano na Mungu wako!
Ukiachilia mbali hilo unaweza ukagundua kusudi lako kwa kuangalia ni jambo gani ambalo upo tayari hata kulifanya bure!
Bila shaka mbali na kuwa umejifunza mengi kuna jambo huwa unapenda sana kulifanya, kama lipo anza kulifanya kwa mwendelezo mpaka lianze kukulipa!
Pia unaweza kugundua kusudi la kuumbwa kwako kwa kujenga utaratibu wa kufanya tafakari, unatakiwa ujipe muda wa kutosha ili ujijue vizuri wewe ni nani na unaweza ukafanya nini...
Ukweli ni kwamba ukijijua vizuri utaweza kutambua ubora wako na udhaifu wako, hali ambayo itakusaidia uweze kujisimamia, kujitawala pamoja na kujiongoza pindi ukiwa unaliishi kusudi lako!
Hata hivyo unaweza ukagundua kusudi la kuumbwa kwa kusoma vitabu mbalimbali, kumbuka vile utakuwa kimaisha miaka mitano ijayo itategemeana na vitabu utakavyosoma.
Mbali na hilo mambo mengi kuhusu vile ulivyo yamefichwa kwenye vitabu, kwa kusema hivyo kupitia kusoma vitabu unaweza ukagundua mtu mwenye sifa kama zako anaweza akafanya nini, hali ambayo itakusaidia hata wewe uweze kujua kile ambacho unaweza ukakifanya.
Ukiachilia mbali hilo unaweza ukagundua kusudi la kuumbwa kwako kwa kujifunza kwa watu wengine, hii ni kwa sababu kama wao wameweza kufanya maana yake hata wewe unaweza.
Kumbuka moja ya kithibitisho kwamba hata wewe unaweza ukafanya jambo Fulani, ni kwa sababu wengine wameweza kufanya jambo hilo!
Mwisho kabisa unaweza kugundua kusudi lako kwa kuwa mtu mwenye fokasi, yaani kuangalia kwa umakini na uchunguzi kila kinachotokea katika maisha yako.
Ukweli ni kwamba kusudi ni kufanyika kwa jambo Fulani. Kwa kusema hivyo kuna kila sababu za kufanyika kwa maisha yako, unachotakiwa kufanya katika hatua hii ni kuhakikisha unatumia kila mbinu mpaka ugundue kusudi la kuumbwa kwako na uwepo wako hapa duniani.
Kumbuka maisha pasipo kusudi ni uhai unaochezewa, unatakiwa uwape watu sababu ya uwepo wako hapa duniani.
Rafiki usiishi kwa sababu uko hai bali ishi kwa sababu kuna kusudi linalokufanya uishi!
Hakikisha hauvuki hatua hii pasipo kugundua kusudi lako, kwa sababu endapo itakuwa hivyo mwendelezo wa makala ijayo hautakuwa na msaada kwako!
Ukitaka kujifunza Zaidi kuhusu namna ya kugundua kusudi la kuumbwa kwako, nakushauri utafute kitabu changu kiitwacho; “Sikuja Duniani Kwa Bahati Mbaya, Bali Nilizaliwa Kwa Kusudi Maalumu”.
Habari njema ni kwamba kinatolewa bure kabisa hata sasa unaweza kujibu ujumbe huu kwa kuandika Neno KITABU kwenda Whatsapp No 07 44284329/0673184329.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri...
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho.
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment