Kama Unataka Kugundua Uwezo Utakaokusaidia Uliishi kusudi Lako Soma Hii..
Habari yako rafiki yangu, ni matumaini u mzima wa afya!
Karibu kwenye mwendelezo wa somo letu linaloangazia namna gani mtu unaweza ukajifunza vitu sahihi!
Na ifahamike kwamba makala iliyopita ilidokeza kuhusu mbinu ya kujiuliza maswali ya kidadisi kama njia ya kujifunza vitu vipya, hali ambayo inaweza ikakusaidia uweze kugundua kusudi la maisha yako!
Na kama ulifanikiwa kugundua kwa nini uliumbwa, na upo hapa duniani kwa kusudi gani, basi leo niko hapa kukuletea mwendelezo wa somo letu!
Makala yetu ya leo inalenga zaidi katika kudokeza jinsi gani unaweza ukagundua uwezo utakaokusaidia uliishi kusudi Lako...
Ukweli ni kwamba kila kusudi ulinalo, kuna uwezo ambao umeumbiwa nao ili ukusaidie kuliishi kusudi hilo, na usipoweza kugundua uwezo huo hutaweza kuliishi kusudi hilo!
Na ifahamike kwamba, kugundua kusudi lako ni kitu kingine, na kuliishi kusudi hilo ni kitu kingine.
Unatakiwa kujua kwamba, kugundua kusudi la kuumbwa kwako siyo kigezo cha kuliishi kusudi hilo bali kuna jambo lingine unatakiwa ulifanye!
Na, Mungu hajawahi kukosea katika uumbaji wake, kwa sababu kila mtu aliyeumbiwa kusudi fulani, ndani yake ameumbiwa uwezo utakaomsaidia aliishi kusudi hilo!
Na, ifahamike kwamba kusudi hilo huwa ni kwa ajili ya watu wengine! Na, endapo ikatokea umegundua kusudi la kuumbwa kwako pasipo kugundua uwezo utakaokusaidia uweze kuliishi kusudi hilo, hiyo ni kazi bure!
Sikiliza rafiki, kwa mfano kama kusudi langu lilikuwa niwe muelimisha jamii kama ambavyo huwa nafanya.
Maana yake lazima niutambue uwezo wangu utakaonisaidia nilishi kusudi hilo. Kwa upande wangu nilipojifanyia tathmini niligundua kwamba nina uwezo wa kuandika.
Kwa kusema hivyo, kusudi langu linakamilishwa kupitia uwezo wangu wa kuandika niliozaliwa nao!
Na mpaka sasa nimebadilisha kusudi langu na kuwa kama kazi ambayo sijasomea kitaaluma, lakini nafurahia kuifanya kwa maana ninaponya fahamu za watu wengi na kupitia kufanya hivyo ninatengeneza maokoto...
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba somo la uwezo wa maeneo ambayo kila mwanadanu huzaliwa nayo, hata shuleni huwa halifundishwi!
Kwa kusema hivyo kuna watu wengi ambao wanatambua kusudi lao, lakini hawatambui uwezo walionao ili uwasaidie waliishi kusudi hilo!
Lakini kwa vile hili huwa halizingatiwi ndiyo sababu kubwa watu wengi huhitimu shule wakiwa wamesomea vitu visivyohusiana hata na kusudi la kuumbwa kwao, na visivyohusiana kabisa hata na uwezo walionao!
Je, unajua kusudi lako ni lipi? Kama jibu lako ni ndiyo nakusogezea maeneo kumi ya uwezo ambao kila mwanadanu huzaliwa nayo, baada ya hapo angalia kusudi lako ni nini, halafu uhusianishe na uwezo katika eneo mojawapo utakaokusaidia katika kuliishi kusudi lako!
Mnamo mwaka 2012, Charles Handy pamoja na Howard Gardner walifanya utafiti uliolenga kuchunguza maeneo ya uwezo ambao kila mwanadamu huzaliwa nao...
Kwa mujibu wa utafiti huo, maeneo kumi ya uwezo ambao kila binadamu huzaliwa nayo yalipatikana.
Na, katika kufafanua zaidi WATAALAMU hawa walidokeza kuwa, kila mwanadamu anamiliki eneo moja au hata maeneo mawili ya uwezo, sema wengi wetu huwa tunashindwa kugundua hili kwa sababu ya ujinga uliosababishwa na mifumo iliyotulea...
Kwa kusema hivyo kila eneo la uwezo ni mahususi katika kukusaidia uweze kuliishi kusudi lako kwa urahisi zaidi!
Kwa mfano kama kusudi lako ni kuwa mwimbaji Mungu atakuwa amekuumba na sauti nzuri kama kinanda, kiasi kwamba ukiimba hata mbingu zinaweza kufunguka!
Nakupelekea kwa haraka haraka kwenye maeneo haya ya uwezo wa maeneo kumi ambayo kila mwanadamu huzaliwa nayo, ili yakusaidie ujue namna gani unaweza kuliishi kusudi la kuumbwa kwako!
1. Uwezo Wa Kuzungumza: Hawa ni watu ambao wanapenda sana kuzungumza, wanafurahia sana kusimulia stori mbalimbali, ni wazuri sana katika kuzungumza na wanajua kutumia lugha kimamlaka.
Watu wanaomiliki uwezo huu wanaweza kuwa: wanasiasa, walimu, watangazaji, waigizaji, waandishi, washehereshaji, wahubiri, watoa huduma kwa wateja, wahariri, n.k
2. Uwezo Wa Kuchezesha Viungo Vya Mwili: Hawa ni watu ambao wana uwezo wa kutumia viungo vya mwili pamoja na mijongeo ya kimadaha.
Bila shaka katika kuishi kwako, umekutana na wanamichezo mbalimbali.
Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba, wanamichezo wote unaowajua wewe wanamiliki uwezo huu!
Watu wanaomiliki uwezo huu wanaweza kuwa: wanamichezo, waigizaji, walimu, madansa, kocha wa timu, mafundi simu, n.k
3. Uwezo Wa Kimuziki: Huu ni uwezo kutunga nyimbo pamoja na kuimba kwa sauti nzuri kama kinanda.
Unatakiwa kujua kwamba siyo kila anayetoa sauti huwa anaimba, kuna watu ambao wako talented kiasi kwamba akiimba hata mbingu zinaweza zikafunguka!
Endapo una sauti nzuri na unapenda sana kuimba basi huenda unamiliki uwezo huu, ila kutokana na kukosa taarifa sahihi umejikuta ukijiuza kwa hasara na kutokutumia kabisa uwezo huu!
Watu wanaomiliki uwezo huu wanaweza kuwa: waimbaji, watunzi wa nyimbo, waandaa muziki, walimu wa muziki, waimba kwaya, wadhamini wa muziki, n.k
Kutokana na uhaba wa nafasi naishia hapa, kesho utapewa mwendelezo wa makala hii...
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Comments
Post a Comment