Kama Unataka Kujua Uhalisia Wa Mwanaume Dhidi Ya Dai lisemalo; "Hakuna Mwanaume Anayeridhika Na Mwanamke Mmoja" Soma Hii...

Hivi una Habari kuwa karibu robo tatu ya dunia nzima imehalalisha kuwa ngono kwa mwanaume ni kitu cha kawaida sana kukifanya, kiasi kwamba mwanaume kamili hawezi kukaa bila kufanya ngono haijalishi yupo kwenye mahusiano halali au laaah?

Dai hili huungwa mkono na nadharia tete ya kisayansi inayodai kuwa; "kwa mwanaume ngono ni lazima kwa sababu ya maumbile yake ya kibaiolojia yalivyo". 

Hivyo huona si kawaida mwanaume kukaa bila kufanya ngono kwa muda mrefu, na katika kufanya makadirio yao, wengi huishia kukadiria kwamba mwanaume hawezi kukaa miezi mitatu bila kufanya ngono. 

Kinachostaajabisha Zaidi ni kwamba, hakuna uthibitisho juu ya dai hilo, huenda kuna mtu mmoja alikaa tu mahali na wazinzi wenzake. Wakabuni hilo wazo, baadae akaja na wazo hilo akawauzia wanaume, na wanaume nao wakalipokea na wakalihalalisha iwe ni falsafa inayoongoza na kuyasimamia maisha maisha yao! 

Na ifahamike kuwa mwadamu huwa vile anavyojifikiria, kwa hiyo basi endapo itatokea mwanaume akajiona kuwa hawezi kuishi bila ngono na wanawake ndivyo anavyokuwa, lakini haimaanishi kuwa hawezi kweli, maadamu ameamini kuwa hawezi, basi hataweza kweli. 

Na ndiyo maana hata BIBLIA TAKATIFU imeandikwa kuwa; “maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo”

Binafsi siliamini dai lisemalo kuwa "mwanaume hawezi kuishi bila ngono" kwa sababu mimi nimeweza. HABARI njema ni kwamba, nina uwezo wa kuishi bila kufanya ngono mpaka wakati nitakaona kwamba huu ni wakati muafaka kwangu mimi kufanya hivyo!

Namaanisha kwamba Kwa wakati huo, mimi mwenyewe nitakuwa mtu muafaka huku nikishiriki na mtu muafaka, ili nipate matokeo halali ya tendo la ndoa yaani uzazi! Upate kujua kwamba tendo la ndoa ni maalumu kwa ajili ya "wanaume wanaojielewa" na siyo "wavulana".

Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kwamba, chini ya mwamvuli wa wengi wape, wanaume wengi wamelipokea na wameamini dai lisemalo; "hakuna mwanaume ambaye hawezi kuishi bila kufanya ngono". 

Na, ndiyo maana ni mara chache sana kumpata mwanaume ambaye haamini katika hilo. Wengi wanaendekeza ngono na kuona kuwa ngono ni halali yao kwa sababu ya imani potofu isiyo na uthibitisho wowote ule...

Binafsi huwa siamini katika wengi wape, kwa sababu mbali na kuwa wao ni wengi wanaweza kuwa wapumbavu vilevile. 

Je, ni halali mimi kuhalalisha upumbavu wa watu wengi chini ya mwamvuli wa wengi wape? Lahasha! Busara zangu ndogo zinaniambia hili siyo kweli.

Ukweli ni kwamba falsafa ya wengi wape ndiyo imewafanya wanaume wengi, wajihesabie haki na kuona kuwa ni halali yao: kufanya ngono na kila mwanamke watakayekutana naye, wawasaliti wenzi wao, wawe na wanawake wengi, waone ni halali tu kununua wanawake wanaojiuza, waanzishe mahusiano kwa sababu ya ngono huku wakiwa hawana mpango wa kuoa, wasiwe watu wenye mapenzi ya dhati kwa familia zao kwa sababu wanao uwezo wa kupata ngono popote pale, wahalalishe misemo inayosema mwanaume hawezi kuishi bila ngono pamoja na kujihalalishia kuwa hakuna mwanaume ambaye hutosheka na mwanamke mmoja.

Nayaandika haya kwa sababu nina uthibitisho, na nimeyapitia haya katika kuishi kwangu! 

Kuna siku nilikutana na mwanaume-mvulana mmoja hivi, katika maelezo yake alidai kuwa: “mwanaume kama utaishi bila mwanamke utakufa”. 

Nikamuuliza; “kwa hiyo kabla hujamjua mwanamke ulikuwa mtu mfu, na ukawa mtu hai baada ya kumjua mwanamke?” 

Akasema, "nilikuwa hai", nikamuuliza kwa hiyo hoja yako iko wapi? Ndipo nikabaini kuwa hata yeye ni miongoni mwa wale watu ambao huamini vitu pasipo kuvifanyia uthibitisho!

Nikamuuliza tena swali jingine; “mbona mimi sijafa na ninaishi bila wanawake, na tena nina Mawazo yanayoiishi lakini wewe una Mawazo yaliyokufa mbali na kuwa unatembea na hao wanawake wako?” 

Hapa hakunijibu kitu. Nikahitimisha kuwa hii ndiyo aina ya wale wanaume wanaoamini mambo mengi kuwahusu lakini hawana uthibitisho nayo, ambapo MWISHO wa siku huishia kunyongwa na mambo hayo!

Unatakiwa kujua kwamba, hayo ni Mawazo ya kipumbavu ya mtu aliyekosa hoja! Hili siyo kweli dunia imekupoteza ndugu mwanaume.

Hujaumbiwa ngono tu, kuna kusudi uliloumbwa uje ulikamilishe hapa duniani, nakushangaa tu kila wakati upo umetingwa kuhangaika na ngono kana kwamba itakupa uzima wa milele! Huo ni upumbavu wa kiwango cha hali ya juu, nakusanua tu...

Mpenzi msomaji, huhitaji shuhuda nyingi sana kulithibitisha hili, fanya uchunguzi wako kwa utaratibu utagundua kuwa, katika siku hizi za usoni, ngono imekuwa ikihalalishwa kuwa ni jambo la kawaida tu, na wanaume nao hawana budi kuhakikisha kuwa wanakuwa na wanawake wengi kadiri watakavyo kwa sababu hakuna mwanaume ambaye hutosheka na mwanamke mmoja…

Kwa upande wangu huwa sishawishiki na wazo potofu kama hili kwa maana kile kitendo nitakachokifanya na mwanamke wangu ndicho nitakachofanya na wanawake wengine.

Nilipopata funuo hilo nikasema "waoh! Huu ni wakati wa mimi kuishi kweli ya maisha" 

Na ndiyo maana, mpaka sasa huwa ninaamini kuwa mwanamke mmoja ananitosha na nitatosheka na mwanamke mmoja tu. 

Na moja ya ushauri ambao huwa nawapa watu, na endapo hata wewe utakuja kwangu kuomba nikushauri nitakuambia hivi; "katika kila jambo utakalotaka kulifanya angalia neno la Mungu limesemaje kuhusu jambo hilo, halafu ufanye kama vile ambavyo neno limesema, na siyo vile ambavyo wewe unataka"

Kwa hiyo hata suala la ngono kwenye biblia limezungumziwa na Mungu ameonekana akiweka zuio, si kwa lengo la kukunyima starehe, bali kwa lengo la kukutaka ujenge mahusiano sahihi ili ndoa yako ije iwe kama mbinguni na siyo ya mateso kama kuzimu!

Swali linakuja kwako wewe uliyehalalisha ngono na kila siku unajitwalia wanawake tena hata wake za watu, kwa madai kwamba huwezi kukaa bila kufanya ngono na huwezi kutosheka na mwanamke mmoja, je, ni kwamba umekuwa kipofu kiasi hicho? 

Je, unajua neno la Mungu ambalo ndilo msingi wetu linasemaje? 

Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu?” 

Wengi mnaiitii dunia ndiyo maana mmekuwa adui wa Mungu na mnamchukia Mungu, na si ajabu mtanichukia na mimi ninayewaletea Habari hii kwa sababu nawanyima starehe yenu! Sipo hapa kukunyima starehe zako tafadhali! Niko hapa nikufundishe kitu!

Ukweli ni kwamba siogopwi kuchukiwa na wala sihitaji upendo wako wa kinafiki, kwa maana upendo wa Mungu kwangu unatosha, na ni kupitia upendo huo ndiyo umenisukuma nikuletee Habari hii njema. Ili utoke gizani, ukafanye matendo ya nuruni kwa maana aliyopo gizani huwa haoni pale alipo na kule aendako.

Ndugu mwanaume hutakiwi kunichukia nipende tu, halafu ufuatane nami kwa makini tukalijadili suala hili kiundani. Unatakiwa kujua kwamba dunia inakutaka na Mungu anakutaka.

Ni upendo wa Mungu leo umepata ujumbe huu, unatakiwa kujua kwamba mbali na kuwa upo hapa duniani hutakiwi kuipenda sana dunia. 

1 Yohana 2:15 “Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake”.

Unaweza ukawa unajiuliza sasa kama nipo duniani inakuwaje nisiipende dunia na huko kupenda dunia ndiyo kufanyeje? 

Ni kuyapenda mambo ya gizani yanayofanyika duniani ambayo yanakataa nuru. Uasherati, zinaa pamoja na uzinzi. Haya yote hayana umuhimu wowote ule maishani mwako Zaidi ya kukuharibia heshima yako na kukupunguzia thamani yako.

Na ifahamike kwamba, mwanaume KAMILI hapimwi kwa kuangalia idadi ya wanawake aliolala nao. 

Bali hupimwa kupitia kuangalia ule ukuu alioubeba na pale alipofika kimaisha pamoja na jinsi anavyogusa maisha ya wengine katika hali chanya! 

Ukweli ni kwamba mwanaume-mvulana huhangaika na wanawake maisha yake yote, ilihali mwanaume KAMILI humchagua mwanamke mmoja kati ya wengi na kuanza naye safari ya maisha ya ndoa.

Mimi mwenyewe kabla sijawa mwanaume, enzi za uvulana nilikuwa naamini kwamba, mwanamke mmoja hanitoshei na ninatakiwa niwe na wanawake wengi, na kweli niliishi maisha ya mtindo huo.

Lakini mara baada ya kubadilii imani yangu na kukua kiufahamu na kiuelewa na kuwa mwanaume komavu ndipo sasa nikabaini kuwa nilikuwa nimepotea. 

Nikagundua kwamba ninatakiwa niwe na fokasi kwa kumchagua mwanamke mmoja tu nitakayempenda na kuwa naye maisha yangu yote. 

Mpaka sasa nimefanikiwa kudumu katika imani yangu hiyo na ninaendelea kufukuzia ndoto zangu! Kwa kusema hivyo hata wewe unaweza ukakaa bila kufanya ngono ukajipanga kwanza, mpaka muda ambao utakuwa tayari umejipanga kwa ajili ya hilo. 

Hata hivyo ninachokijua ni kwamba tendo la ndoa ni tendo takatifu kwa kusema hivyo halina budi kufanyika kwa kufuata taratibu za Kiungu pamoja na utakatifu. 

Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”. 

Kumbe Mungu kaweka zuio ili kutufanya sisi tushiriki katika hali ya utakatifu na siyo kufanya uharibifu kama tulivyozea kufanya!
 
Kwa maana kutembea na kila mwanamke anayekatiza mbele zako, huo ni uharibifu na siyo utukufu kwa Mungu mwenye vyote!

Ndugu mwanaume hebu staarabika basi. Ukweli ni kwamba, dunia imekuharibia sana wasifu wako, unaonekana wewe ni kicheche na Fahari yako ni wanawake pamoja na kufanya ngono. 

Binafsi huwa sipendezwi sana na mtizamo huu uliopo dhidi ya wanaume! Unachotakiwa kujua ni kwamba, huwezi kupata tuzo kwa kutembea na wanawake wengi Zaidi ya kuchukua mikosi, laana, mabalaa pamoja na kupoteza uelekeo thabiti. 

Leo hii dunia imeharibu wasifu wako na kukufanya uonekane wewe ni mpenda ngono na ngono ni kila kitu kwako na usipofanya ngono utakufa. Kumbe uhai chanzo chake ni Mungu na mauti chanzo chake ni dhambi, na kufanya zinaa ni dhambi!

Sijajua nyie wenzangu mnamwabudu Mungu yupi lakini ninachojua ni kwamba Mungu kakataza hili!
Leo hii mnazalisha na kutelekeza familia zenu, huku mkiwaacha wanawake na Watoto wa damu zenu kwenye mateso makali pamoja na maisha magumu kisa ngono! Inaumiza na kusikitisha sana kwa kweli! 

Leo hii kuna ongezeko la mama wenye Watoto pasi na mume kwa sababu ya kuendekeza kwenu ngono. 

Hata hivyo, leo hii mnaonekana kuwa hamtosheki na mwanamke mmoja kwa sababu ya tamaa zenu. Binafsi sipendezwi sana na hili na sijivunii kuwa mwana! 

Huenda ukawa unafikiri huyu kijana mdogo ananifokea au, mimi sikufokei hata, najaribu tu kukueleza ukweli unaopaswa kuujua. Ishi kwa kuongozwa na utashi! Simamia akili na utashi Katika kuishi kwako. 

Zaburi 32:9 “Msiwe kama farasi wala nyumbu, walio hawana akili…”

Sijui kwanini unasoma makala hii, lakini nikuhakikishie kuwa uamuzi ulioufanya wa kusoma makala hii, ni uamuzi mzuri sana kuwahi kuufanya, na hii kwa sababu uamuzi huo unaenda kubadili mitizamo yako kuhusu uhalishia uliopo kati ya mwanaume na ngono nawe utaenda kuudhihirisha uanaume wako.

Katika mwendelezo wa Masomo Haya utajifunza: mamlaka na ukuu wa mwanaume, kwanini wanaume wengi huendekeza ngono, athari za kuendekeza ngono pamoja na nini ufanye ili uishi pasipo kutumikia ngono.

Nimekuombea kwa Mungu ili ukimaliza kufuatilia mwendelezo wa Masomo Haya, ukaudhihirishe uanaume wako na siyo kuutumia uanaume wako kwa ajili ya zinaa tu…

Karibu sana, fuatilia masomo haya mpaka mwisho, ama hakika hutajutia kabisa.

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e: Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...