Fahamu Kuhusu Hatua Kuu Tatu Za Ukuaji Wa Maisha Ya Binadamu Pamoja Na Yale Unayopaswa Uyajue Katika Kila Hatua...

Hatua za ukuaji wa maisha ya mwanadamu zinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu. 

Na katika makundi haya matatu mwanadamu huyo hana budi kuwa na ufahamu kulingana na kundi la hatua alilopo! Hii inamaanisha kwamba ni lazima kuwe na upatanifu kati ya ufahamu wake pamoja na hatua aliyoifikia! 

Kwa mfano unapokuwa kijana kiwango chako cha uelewa hakipaswi kuwa sawa na kile kiwango cha uelewa ulichokuwa nacho ulipokuwa mtoto. 

Hata hivyo unapokuwa mzee kiwango chako cha uelewa hakipaswi kuwa sawa na kile kiwango cha uelewa ulichokuwa nacho ulipokuwa kijana! 

Sasa shida huwa inakuja pale unapojikuta wewe ni kijana na una uelewa wa mtoto mdogo au wewe ni mzee na una uelewa kijana mdogo. 

Endapo itakuwa hivyo, unatakiwa kujua kwamba huwezi kufika mbali kimaisha!

Watafiti wamebaini kwamba kuna hatua tatu za ukuaji katika maisha ya mwanadamu, na katika kila hatua mwanadamu anatakiwa awe na maarifa na taarifa sahihi hasa ukihusisha na hatua aliyopo.

Na endapo itatokea akawa hajajifunza vitu sahihi basi uelewa wake utakuwa chini kwa kusema hivyo hataweza kufanya mambo yanayolandana na hatua aliyonayo. 

Hapa ndipo pale utakuta mzee anafanya mambo aliyopaswa afanye alipokuwa kijana na wengine hujikuta wakichanganyikiwa wasijue cha kufanya!

Zifuatazo ni hatua tatu za maisha ya binadamu pamoja na yale uliyopaswa uyaelewe katika hatua husika. 

Unachopaswa kufanya ni kuhusianisha kilichoandikwa hapa pamoja na hatua uliyopo sasa. 

Na, endapo utabaini kuwa, kuna jambo haliko sawa, usiwe na shaka makala hii imeandikwa kwa ajili ya hilo. Habari njema ni kwamba huu ni wakati wa kuamka na kufanya mambo sahihi. 

1. Hatua ya kujifunza (miaka 1-25)
Hii ni hatua ya kwanza ambayo huanzia siku unayozaliwa mpaka pale utakapofikisha miaka 25.

Unatakiwa utumie kipindi hiki katika kujifunza mambo yote ya msingi yahusuyo maisha.

Kwa mfano hadi kufikia umri wa miaka 25 unatakiwa uwe na ufahamu wa kutosha kuhusu; elimu ihusuyo saikolojia, elimu ihusuyo masuala ya uchumi na fedha, elimu ihusuyo uhusiano na watu wengine, elimu ihusuyo mahusiano, uchumba na ndoa, elimu ihusuyo maendeleo binafsi, elimu ihusuyo kozi au fani Fulani, elimu ya kiroho pamoja na elimu ya utambuzi Binafsi! 

Unatakiwa kujua kwamba kiwango chako cha kujifunza ndicho kitakachopima hadhi ya maisha yako pamoja na pale utakapofika kimaisha! 

Hata hivyo kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba hata fedha imejificha kwenye maarifa, kwa kusema hivyo katika hatua hii huna budi ujifunze vitu vingi Zaidi ili utakapoifikia hatua ya pili uweze kutumia mafunzo hayo kutengeneza fedha kirahisi. 

Kwa ujumla katika hatua hii hakikisha unafahamu kanuni asilia zinazoongoza ulimwengu huu, unatakiwa uwe umehitimu elimu ya kitaaluma angalau uwe hata na shahada ya kwanza, unatakiwa uwe umeshalijua kusudi la maisha yako, unatakiwa uwe umeshapata maono kamili juu ya kule unakoyapeleka maisha yako. 

Pia katika hatua hii unatakiwa uweze kugundua uwezo uliopo ndani ndani yako pamoja na kazi ya ndoto zako utakayoifanya kutokana na uwezo ulionao. 

Vilevile katika hatua hii unatakiwa uwe umefanikiwa kujijenga kimtizamo na kiimani na kuamini katika uwezo wako. 

Na kama una miaka 25 au Zaidi na huyajui haya yote, maana yake upo nyuma ya wakati kwa hiyo huu ni wakati wa kuamka na kufanya mambo yatokee. 

Hutakiwi kusubiri mambo yatokee tena kwa sababu mpaka hapa maisha yako yapo nyuma ya wakati. 

Je, una umri gani mpaka sasa? Ndugu huenda tayari maisha yako nyuma ya wakati, hivyo basi huna budi kuamka wewe usinziaye.

2. Hatua ya kutengeneza pato (miaka 26-50)
Hii ni hatua mahususi kwa ajili ya kutengeneza fedha!

Kwa kusema hivyo kila mtu aliyopo kwenye hatua hii, hana budi kutengeneza pato la kutosha kutokea vyanzo mbalimbali halali vya mapato kama moja ya matokeo chanya ya kile alichojifunza katika hatua ya kwanza. 

Hii ni sawa na kusema kuwa mtu huyo hana budi kutumia maarifa aliyojifunza katika hatua ya kwanza ili kutengeneza pato.

Vilevile katika hatua hii unatakiwa uwe umeshaoa/kuolewa na unawalea watoto wako kwa namna bora, labda uwe umeamua kukaa bila ndoa.

Hata hivyo katika hatua hii hutakiwi tena uwe unahangaika kujifunza bali unatakiwa uwe unatumia maarifa yote uliyoyapata katika hatua ya kwanza ya ujifunzaji katika kuishi kwako hapa duniani.

Mbali na hilo katika hatua hii unatarajiwa uwe umefanikiwa kutengeneza vyanzo mbalimbali halali vya mapato kama vile ulivyojifunza kwenye hatua ya kwanza. 

Hutakiwi tena uwe unahangaika kutengeneza kipato au kusumbuka na umaskini. 

Vilevile hutakiwi tena kuwa unahangaika kutafuta kazi kwa sababu maarifa uliyojifunza katika hatua ya kwanza yatakuwa yamekusaidia uweze hata kujitengenezea kazi yako mwenyewe. 

Pia hapa hutakiwi tena uwe unateseka na maisha kwa sababu mateso huletwa na ujinga wa kutokujua, maadamu umejifunza katika hatua ya kwanza hutakiwi tena kufanya mapambano ya maisha. 

Vilevile hutarajiwi uwe unapambana kuongeza kiwango cha elimu kama vile shahada ya pili kwa sababu hayo yote ulitakiwa uwe umeshayafanya katika hatua ya kwanza.

Katika hatua hii unatarajiwa uwe umejenga familia bora na unawalea watoto kwa namna bora kama vile ambavyo umejifunza katika hatua ya kwanza.

Kumbuka hatua ya kwanza ililenga zaidi katika kukufanya uyatafute maarifa yote yahusuyo kila kipengele nyeti cha maisha yako.

Na kama upo katika hatua hii na bado unatengeneza pato la chini, unahangaika kutafuta kazi, unateseka na umaskini na maisha, hujaoa/hujaolewa na una mpango wa kuwa mwanandoa na mengine mengi. 

Ndugu maisha yako nyuma ya wakati huna budi uamke wewe usinziaye ili uyaamshe maisha yako yaliyolala yawe hai. 

Ndugu sipo hapa kukuhukumu au kukufanya ufanye maamuzi haraka, na sina maana kwamba unachelewa, ila najaribu tu kukuonesha kuwa kwa umri ulionao ulitakiwa uwe wapi!

3. Hatua ya kustaafu (miaka 51 na kuendelea)

Hii ni hatua ya mwisho kabisa ya maisha ya mwanadamu. 

Hatua hii huanzia miaka 51 na kuendelea. Katika hatua hii unatarajiwa uwe unaishi maisha ya ndoto zako kwa sababu ya kutumia maarifa uliyojifunza na mbinu ulizotumia kwenye hatua ya pili katika kuweka maarifa uliyojifunza kwenye hatua ya kwanza katika vitendo, ili uzae matunda kwa hayo.

Hapa unatakiwa uwe umeshafikia uhuru wa kuishi kila aina ya maisha utakayoyataka, maadamu hayawadhuru wengine wala hayavunji sheria na taratibu! 

Vilevile katika hatua hii unatakiwa uwe unaishauri jamii yako na kugusa maisha ya wengi kwa kutumia maarifa uliyojifunza.  

Hapa unatakiwa usimamame kama mzee wa busara, ambaye utasimama katika kuwafundisha vijana wadogo kanuni za maisha na namna ya kuishi kiutu. 

Vilevile katika hatua hii unatakiwa uwe umeshastaafu na unapumzika kwa sababu ya kazi kubwa uliyofanya kwenye hatua ya pili katika kuyaweka maarifa yote kwenye vitendo.

Mambo ambayo si ya kawaida kabisa na hutakiwi kabisa kuyafanya katika hatua hii ni; 

Hautarajiwi uwe una mtoto mdogo unamlea, hautarajiwi uwe unatafuta kazi, hautarajiwi uwe unasoma labda uwe unasoma kwa burudani tu, vilevile katika hatua hii hautarajiwi uwe maskini.

Kwa ujumla hii ni hatua ambayo unatakiwa utumie kudhihirisha ukuu wako, hii ni hatua unayotakiwa uzifikie ndoto zako, hii ni hatua ambayo unatakiwa ufurahie uwepo wa maisha yako hapa duniani. 

Na endapo imetokea wewe ni mzee au upo katika hatua hii na haujafanikiwa katika mambo tajwa hapo juu, nipo hapa kukufahamisha kuwa upo nyuma ya wakati na unaweza ukaishia kubaki na hali dumavu maisha yako yote!

Sijajua upo katika hatu gani, lakini mtu mwenyewe na ujipe tathmini binafsi. 

Mimi nimekuonesha tu lakini sikuamuru ufanye nini kwa sababu una wajibu wa kuchagua kuhusu maisha yako.

Na kama ulikuwa hujui haya yote na upo kwenye hatua mojawapo kati ya hizi, nipo hapa kukufahamisha kuwa huu ni wakati wa kuamka na kuanza kufanya mambo yatokee. 

Na ifahamike kwamba kama kwa muda wote huo ulioishi na katika safari yako ya kujifunza bado hujayajua haya yote, basi huna budi kujua kwamba umejifunza yasiyofaa kwa hiyo makala hizi zinaandikwa kwa ajili yako na huna budi kuzisoma zote ili upate maarifa muafaka!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...