Kama Una Kiu Ya Kufanikiwa Na Kufika Mbali Kimaisha Huna Budi Kuepuka Falsafa Ovu Zifuatazo..
Jambo moja la msingi unalopaswa kujua ni kwamba falsafa ni somo ambalo huchambua ukweli uhusuo maisha ya binadamu.
Hivyo basi endapo ukweli huo utatumika vibaya au ukweli huo ukawa hauna kweli ndani yake, inamaanisha kwamba watu watautumia ukweli usio kweli kuongoza maisha yao, hali itakayosababisha wapate matokeo yaliyo kinyume na matarajio yao!
Hii ndiyo sababu kubwa utakuta mtu anafanya vitu vingi, anapambana sana, ana matumaini makubwa kuhusu maisha yake na anaamini kwamba ipo siku atafanikiwa, lakini hapigi hatua kimaisha!
Kumbe shida siyo mapambano anayoyafanya bali shida ni aina ya falsafa alizozichagua na kuziamini katika mapambano yake!
Ukweli ni kwamba, katika kuishi kwetu wengi wetu tumejikuta tukiongozwa na falsafa za uongo, hali ambayo inakwamisha maendeleo yetu na kusababisha tushindwe kuzifikia hatima nzuri za kesho zetu!
Ili kubadili maisha yako ya kesho pamoja na kufanikiwa maishani, kuna baadhi ya falsafa na imani unatakiwa uziondoe na kuzitupilia mbali!
Na, ndiyo maana awali nilisema kwamba endapo utafanikiwa kubadilisha mfumo wako wa kuamini utakuwa umepiga hatua kubwa sana.
Kuna wakati mwingine unashindwa katika maisha yako siyo kwamba unatakiwa ushindwe, ila ni kwa sababu kuna falsafa ovu umeziamini ambazo zinapelekea kushindwa kwako.
Hivyo basi ili kuepeuka kujiweka hatarini pamoja na kuharibu kesho yako, huna budi kujiweka mbali na falsafa ovu zifuatazo:
1. Liwalo Na Liwe…
Liwalo na liwe…. Halitakuwa…! Unatakiwa ufanye liwe kweli! Kwanza kabla hujajitamkia jiulize swali hili ni lipi hilo unataka liwe?
Je, vipi kama halitatokea? Ni kipi kitafuatia maishani mwako? Kwanza hii falsafa inatumika na watu ambao hawajipendi wao na maisha yao, ndiyo maana kwao wanaona kila kitu ni sawa tu.
Kwani na wewe kaka, dada, mama na baba hujipendi? ...na kama unajipenda kwanini uamini katika falsafa potofu kama hii?
Kwanini uamini katika liwalo na liwe? Jambo moja unalopaswa kujua ni kwamba katika maisha yako una uwezo wa kufanya mambo yatokee.
Kwa mantiki hiyo ili kubadilisha kesho yako huna budi kutupilia mbali falsafa hii. Badala ya kusema liwalo na liwe njoo na jawabu sahihi kuhusu jambo lililopo mbele yako!
Namaanisha kwamba, tafuta vichocheo vitakavyopelekea matokeo unayoyataka kwenye maisha yako na siyo kuishia kusema liwalo na liwe! Hivi ndivyo ambavyo kanuni ya matokeo na kichocheo ilivyonifundisha!
Unachopaswa kujua ni kwamba liwalo na liwe nalo halitakuwa...
Achana na falsafa ya uongo, hebu wajibika maishani mwako kwa kufanya kesho yako iwe bora kuliko Leo!
2. Wakati Wa Mungu Ndiyo Wakati Sahihi…
Kwani mungu anatumia saa gani kuona huo wakati? Au unampangia mungu wakati? Je wakati wa Mungu ndiyo upi?
Kwani wakati wote si ni wa Mungu au kuna wakati usio wa Mungu?
Vipi kama wakati wa Mungu ndiyo sasa? Tumia angalau dakika mbili kutafakari juu ya hili...
Unachopaswa kufahamu ni kwamba endapo utaruhusu falsafa hii iongoze maisha yako utajikuta katika hali unazopitia kama ni sawa tu, hivyo hata usipofanya kitu utajipa tumaini ya kwamba upo wakati wa Mungu ulio mzuri unakuja!
Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba wakati uliokubalika ndiyo sasa, hivyo huna budi kuwajibika kwenye maisha yako.
Endapo utaamini katika falsafa hii utajipa haki kwa kuona kuwa hayo yote unayopitia ni sawa tu, kwa sababu ule wakati ulio wa Mungu ulio mzuri sana bado haujafika.
Hata hivyo utajikuta muda unazidi kusonga tu na hakuna kinachobadilika maishani mwako. Hebu jifunze kukomboa wakati, kumbuka wakati wote ni wakati sahihi endapo kutakuwa kuna kipaumbele ulichopanga kukitimiza.
Wazo limenijia, naona rohoni mwako unajiuliza hivi huyu mwandishi hajaona andiko lilolopo kwenye Mhubiri sura ya tatu?
Lahasha! Hilo andiko nalijua, tena laanza kwa kusema; "Kwa kila jambo kuna majira yake,
Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
Unatakiwa kujua kwamba mara nyingi Mungu huwa anazungumzia mambo yahusuyo ufalme wake na kile atakachokifanya nyakati hizo, na huenda kwenye hizo nyakati wewe ukawa hauhusiki na chochote kile!
Ukweli ni kwamba mambo mengi yaliyoandikwa kwenye biblia hayamlengi mtu mmoja mmoja kama wengi tunavyodhani!
Hata hivyo huna budi kufahamu kuwa, biblia imewagawa watu katika makundi mawili yaani; wana walio wa ufalme wa Mungu na wana walio wa ufalme wa yule mwovu!
Shida inakuja pale upo kwenye ufalme wa yule mwovu halafu unasubiri wakati wa Mungu ufike!
Ndugu huna tofauti na mtu anayesubiri embe chini ya mnazi, kwa hiyo huna budi kuchakarika huku ukimuomba Mungu abariki kazi ya mikono yako!
Zaburi 127:1
[1]BWANA asipoijenga nyumba
Waijengao wafanya kazi bure.
BWANA asipoulinda mji
Yeye aulindaye akesha bure.
Ukitaka kujua kundi la ufalme ulilopo, karibu inbox nitakuunganisha ukajifunze biblia bure kabisa!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentaship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Nmejifunza kitu hapa
ReplyDelete